Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Corona yashusha kasi ya uchangiaji damu nchini

MNH1 Ed Corona yashusha kasi ya uchangiaji damu nchini

Sun, 26 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

MLIPUKO wa virusi vya corona umetajwa kuwa chanzo cha kupungua kwa idadi ya wachangiaji wa damu na kusababisha uhitaji wake kuwa mkubwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), hasa kwa watoto wenye saratani.

Meneja Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kuthibiti Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Omary Ubuguyu, aliyasema hayo jana katika maadhimisho ya saratani za watoto ambayo yalitanguliwa na matembezi ya hisani na baadae michezo mbalimbali.

Maadhimisho hayo ambayo yalitawaliwa na ushuhuda wa waliopona ugonjwa huo, yaliandaliwa na Idara ya Watoto kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Tumaini la Maisha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS).

Dk. Ubuguyu alisema matatizo makubwa wanayokutana nayo sasa ni kuwapo kwa idadi ndogo ya watu wanaojitokeza katika hospitali mbalimbali kuchangia huduma hiyo.

Alisema kabla ya janga la corona, wachangiaji wengi ambao walikuwa wanawategemea wachangie walitokana na matamasha mbalimbali yaliyokuwa yakiandaliwa na kuwekwa huduma hiyo ya kuchangia damu.

"Kwa kuwa tumepunguza matamasha, tumepunguza sehemu ya wachangiaji wa damu waliokuwa wanajitolea huko, tatizo hili wakati huu wa corona limeongezeka zaidi ndiyo maana tunahamasisha watu wachanje," alisema.

Alitolea mfano maadhimisho hayo ya saratani kwa kueleza kuwa wameshindwa kuita idadi kubwa ya watu kwa kuwa bado nchini inapambana kukabiliana na maambukizo mapya ya virusi vya corona.

Dk. Ubuguyu aliwataka Watanzania wajitokeze katika hospitali mbalimbali kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa.

“Kuna jamii za watu wa Asia na madhehebu ya dini, wana jumuiya ambazo kwa pamoja huchangia damu lakini Watanzania wengi hamasa ni ndogo, tunawahamisha wajitoe,” alisema.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani na Damu kwa Watoto kutoka MNH, Khadija Mwamtemi, alisema moja ya matatizo wanayokutana nayo wakati wakitoa huduma, ni uhaba wa damu.

"Matibabu ya saratani yanahitaji damu, wito wangu kwa jamii tunaomba wasiwe na hofu kuja kuchangia, ukitoa utakuwa umetoa mchango mkubwa kwa sababu katika kutibu hawa watoto, tunapata changamoto kubwa, kuna saratani nyingine hasa za damu unashindwa kumpa mtoto dawa kwa sababu damu yake ipo chini.

“Mfano chembe sahani zikipungua mtoto anatokwa na damu ili uzipate lazima kuwe na damu, tunaomba tuunge mkono Mpango wa Taifa wa Damu Salama, uhitaji wa damu ni mkubwa, tukizungumzia matumizi ya damu sehemu kubwa inakwenda kwa wanaojifungua na watoto wakiwamo wa saratani," alisema.

Dk. Mwamtemi alitaja vikwazo vingine ni suala la miongozi kwa wagonjwa wa saratani, akifafanua kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwaondoa watoto hospitalini inapofikia hatua ya matibabu kwa mionzi kwa kudhani watakufa.

Kelvin Kashaija, mwanafunzi anayeingia mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akichukua Shahada ya Sanaa katika Elimu, alisema kuwa mwaka 2009 akiwa na umri wa miaka 10, aligundulika kuwa na saratani ya damu.

Alisema ilianza kama uvimbe kichwani na alipopelekwa Muhimbili, waliutoa wakijua ni wa kawaida lakini baadaye uvimbe mwingine ukaota pembeni ya kidonda.

Alisema Taasisi ya Saratani Ocean Road kwa kushirikiana na daktari wa kigeni ambaye ni miongoni waliopo katika Taasisi ya Tumaini la Maisha, walichukua kinyama na kukiotesha nchini kwao na majibu yakaonyesha ana saratani ya damu.

“Nilianza rasmi matibabu ya saratani mwaka 2010, Ocean Road na baadaye tukahamishiwa Muhimbili, nilikaa wodi ilikuwa inaitwa Ujasiri na Tumaini la Maisha, ugonjwa huu niligunduliwa nikiwa darasa la nne mwishoni, nililazwa mwaka mzima wodini na baadaye nikawa ninahudhuria kliniki mpaka nikapona,” alisema.

Chanzo: ippmedia.com