Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Corona yaibua hofu mpya Afrika Mashariki

99124 Corona+pic Corona yaibua hofu mpya Afrika Mashariki

Mon, 16 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigali, Rwanda. Serikali ya Rwanda imethibitisha kuwa na mgonjwa mmoja aliyeambukizwa virusi vya corona (covid-19).

Mgonjwa huyo raia wa India aliingia nchini humo Jumapili iliyopita akitokea mjini Mumbai, India ameibua hofu mpya kwa nchi za Afrika Mashariki baada ya Kenya na Sudan nazo kuwa na mgonjwa.

Kupatikana kwa wagonjwa katika nchi hizo kumezifanya nchi jirani kuongeza nguvu ya kujilinda na ugonjwa huo ambao awali ilionekana ungeishia China na mataifa jirani ya Asia lakini umekuwa ukisambaa Ulaya, Marekani, Afrika na sasa Afrika Mashariki.

Wizara ya Afya ya Rwanda imethibitisha kupokea mgonjwa huyo ambaye sasa amewekwa katika karantini.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, mgonjwa huyo hakuwa na dalili zozote za virusi vya corona wakati anawasili Rwanda lakini baada ya kukaa siku tano nchini humo alipata homa kali na kuamua kwenda katika kituo cha afya kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Taarifa ya wizara hiyo ilisema kwa sasa mgonjwa huyo anaendelea na matibabu na kwamba hali yake inazidi kuimarika. “Tunaendelea kutafuta watu wote waliokutana na mgonjwa huyo baada ya kuingia nchini na kuwapima ili wasisambaze kwa wengine,” ilisema taarifa hiyo.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Taarifa hiyo iliwatahadharisha raia wote wa Rwanda kufuata sheria zilizotolewa na Wizara ya Afya hasa kuosha mikono kila mara ili kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.

Kufuatia maambukizi hayo, Shirika la Ndege la Rwanda limetangaza kusitisha kwa muda safari zake zote za ndege nchini India hadi Aprili 30.

Shirika hilo lilisema kuwa abiria wote waliokata tiketi watarudishiwa fedha zao bila malipo ya ziada.

Wakati huo huo, Wizara ya Afya nchini Sudan imesema mgonjwa aliyekuwa ameambukizwa virusi hivyo amefariki dunia.

Mgonjwa huyo mwanaume aliyekuwa na miaka ya 50 alifariki dunia Alhamisi iliyopita mjini Khartoum.

Taarifa ya wizara hiyo ilisema kwa sasa Sudan imesitisha utoaji viza kwa nchi nane ikiwamo Italia yenye wagonjwa wengi wa corona pamoja na Misri.

Misri ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuthibitisha maambukizi ya corona na hadi sasa watu wawili wameripotiwa kupoteza maisha kutokana na virusi hivyo.

Ijumaa iliyopita, Wizara ya Afya ya Kenya ilithibitisha kuwapo kwa maambukizi ya corona nchini humo baada ya kupatikana mgonjwa wa mmoja.

Waziri wa Afya Kenya, Mutahi Kagwe alisema mtu huyo alithibitishwa kuwa na maambukizi hayo Alhamisi iliyopita.

Mapema jana asubuhi Serikali ya Ethiopia ilitangaza kuwa na maambukizi ya corona baada ya kupatikana mgonjwa mmoja. Wizara ya Afya ya Ethiopia ilimtaja mgonjwa huyo kuwa ni raia wa Japan ambaye aliingia nchini humo mwishoni mwa wiki.

Kwa upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), mgonjwa wa pili wa virusi vya corona amethibitika kupatikana nchini humo.

Katika hatua nyingine, Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza hali ya dharura kutokana na kuenea kwa virusi vya corona na kwamba Serikali yake ina mpango wa kutoa dola bilioni 50 kupambana na virusi hivyo.

Trump alitoa tangazo hilo katika mkutano na waandishi wa habari na kusema hali nchini humo inaweza kuwa mbaya zaidi na hata yeye atafanya vipimo haraka iwezekanavyo ingawa kwa sasa hawezi kujiweka karantini kwani hana dalili zozote.

Watumishi UN kufanya kazi wakiwa nyumbani

Wafanyakazi wote wa makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN), wametakiwa kufanya kazi zao wakiwa nyumbani kwa wiki tatu kutokana na mlipuko wa corona.

Katibu Mkuu UN, Antonio Guterres alisema mpango huo una lengo la kupunguza wingi wao katika ofisi hizo wakati wakiendelea kufanikisha majukumu kama kawaida hasa ukizingatia kuwa afya za wafanyakazi na ustawi wa maisha yao ni muhimu zaidi.

Chanzo: mwananchi.co.tz