Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Corona yaathiri ukusanyaji damu

DAMU Corona yaathiri ukusanyaji damu

Fri, 1 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MLIPUKO wa virusi vya corona, umetajwa kushusha kiwango cha damu iliyokuwa ikikusanywa katika hospitali ya rufani ya Mkoa wa Kagera.

Akizungumza na Nipashe mshauri wa Kituo cha Damu Salama katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Kagera, Amos Bashweka, alisema kabla ya shule na vyuo kufungwa kituo hicho kilikuwa kikikusanya zaidi ya chupa 400 kwa mwezi, lakini kwa sasa kinakusanya chupa 200.

"Uhaba huu unatokana na wananchi wa mkoa wa Kagera kutokuwa na utamaduni wa kujitolea kuchangia damu katika hospitali, na hii damu tunayokusanya ndiyo inategemewa kuvigawia vituo vingine vya afya na hospitali," alisema.

Bashweka alisema kabla ya shule na vyuo kufungwa, changamoto ya ukusanyaji damu haikuwa kubwa kama sasa, na kutumia fursa hiyo kuwaomba wananchi kubadilika na kujitokeza kwa wingi kujitolea damu, kwa kuwa inapokuwapo damu inayotosheleza mahitaji, inasaidia kuokoa maisha ya wanaohitaji huduma hiyo.

Hata hivyo, alibainisha kuwa kufungwa kwa shule kutokana na tishio la corona kumechangia hali hiyo kwa kuwa kundi la wanafunzi ni muhimu katika ukusanyaji damu.

Kwa mujibu wa Bashweka, asilimia kubwa ya wanafunzi wachangiaji wanakuwa hawana maambukizi ya magonjwa yanayosababisha damu isitumike.

"Damu tunayokusanya tunaipeleka maabara ya kanda iliyoko jijini Mwanza, inapimwa ili kubaini kama ina maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwamo virusi vya Ukimwi, homa ya ini na kaswende, lengo ni kuhakikisha inapotumika inakuwa salama," alisema Bashweka.

Aliwashukuru baadhi ya wanafunzi na wanachuo wanaoishi katika Manispaa ya Bukoba ambao licha ya shule na vyuo kufungwa, wamekuwa wakifika katika kituo hicho kujitolea kuchangia damu, na kuwaomba kuendelea na moyo huo, kwa kuwa damu wanayojitolea inaokoa maisha ya wananchi wenzao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live