CHUO cha Kijeshi cha Sayansi na Tiba kimepanga kuanzisha hospitali yake kwa ajili ya kuimarisha tafiti na itakayojihusisha zaidi na kuchunguza na kutibu magonjwa ya kuambukiza.
Chuo hicho ni chuo pekee cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kinachotoa mafunzo ya stashahada ya uuguzi na stashahada ya uafisa tabibu nchini.
Hayo yalisemwa jana chuoni hapo Lugalo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa chuo hicho, Brigedia Jenerali Charles Mwanziva, wakati akizungumza kwenye mahafali ya pili ya chuo hicho.
Kwenye mahafali hayo, wanafunzi 29 walihitimu stashahada ya uuguzi na wengine 20 stashahada ya afisa tabibu.
Brigedia Jenerali alisema hivi sasa wanategemea hospitali ya Lugalo kwa ajili ya mafunzo ya vitendo na tafiti mbalimbali hivyo kuanzishwa kwa hospitali ya chuo itakuwa hatua kubwa tangu kianzishwe mwaka 1972.
Aidha, alisema wataalamu watakaohudumu kwenye hospitali hiyo mpya watatoka kwenye hospitali ya Jeshi Lugalo na kwenye chuo hicho kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya tafiti na mafunzo ya vitendo.
Alisema chuo hicho pia kinatarajia kuanzisha maabara kubwa na ya kisasa kwani hivi sasa wanategemea maabara ya hospitali ya Lugalo na pia wataanzisha maktaba ya chuo hicho.
“Hivi sasa tuna uhusiano mzuri na vyuo vingine lakini kwenye mpango mkakati wetu tunataka kuimarisha zaidi uhusiano huo ili tuweze kunufaika na utaalamu wa wenzetu ili chuo kiendelee kuimarika kwa sababu tunapata wanafunzi wa nje pia,” alisema Brigeria Jenerali Mwanziva
Alilishukuru Baraza la Ithibati Tanzania (NACTE) kwa kuwapatia miongozo mbalimbali na iliyokisaidia chuo kupata uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi kutoka 500 tangu kuanzishwa kwa chuo hadi kufikia zaidi ya 400 waliopo sasa.
Mkufunzi Mkuu wa Chuo hicho, Luteni Kanali Miraji Mawaka, alisema wanatarajia kuongeza kozi ya mamacheza (physiotherapy) na tiba ya meno ili kuongeza wigo wa udahili kwa wanafunzi wanaohitaji kusomea masomo ya afya nchini.
Luteni Kanali Mawaka alisema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1972 kwa ajili ya kutoa mafunzo kupata wataalamu wa kuwahudumia askari wanapoumia vitani na kwenye makambi yao lakini ikaonekana kuna uhitaji wa kupanua wigo.
“Tulianza kutoa mafunzo haya kwa maaskari lakini baadaye tukapanua wigo kwa raia naokujiunga na chuo hiki na hivi sasa ni kama nusu kwa nusu kuna wanafunzi ambao ni wanajeshi na wengine raia,” alisema