Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chuo Kikuu Mount Meru chakumbwa na majanga

27225 Chuo+pic TanzaniaWeb

Thu, 15 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Wakati Chuo kikuu cha Mount Meru, kikiwa hatarini kutaifishwa na Benki ya Rasilimali (TIB) kama kikishindwa kulipa deni la Sh3 bilioni ilizokopa miaka mitatu iliyopita, umeibuka mgogoro wa umiliki wa chuo hicho. Chuo hicho ambacho Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) imesitisha kudahili wanafunzi wapya  hivi sasa kinakabiliwa na ukata na kushindwa kulipa mishahara ya watumishi. Hata hivyo Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Johannes Monyo licha ya kukiri chuo kudaiwa na TIB, alisema uongozi wa Kanisa la Kibaptisti wanaendelea na mchakato wa kulipa deni hilo. Kutokana na sintofahamu ndani ya chuo hicho, Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Jerry Muro ameanzisha msako wa kutaka kuwakamata baadhi ya viongozi wa chuo hicho waliokopa fedha katika benki hiyo ili kukisaidia chuo hicho. Wakati hofu ya kutaifishwa chuo hicho ikitawala Wachungaji wa makanisa wanachama wa  Jumuiya Kuu ya Wabaptisti Tanzania, wameiomba Serikali kuwasaidia kuwarejeshea umiliki wa Chuo Kikuu cha Mount Meru kilichopo wilaya ya Arumeru mkoani Arusha. Chuo hicho  kwa sasa kinaendeshwa na Askofu Mkuu wa kanisa la Baptisti. Tanzania, Arnold Manase. Wakizungumza na waandishi wa habari, wachungaji wa makanisa ya jumuiya kuu ya Wabaptisti  Tanzania, walisema chuo kikuu hicho, kilianzishwa mwaka 2012 na taasisi tano ambazo ni jumuiya yao, jumuiya kuu wa Wabaptisti ya Kenya na Muungano wa Baptisti Uganda . Taasisi nyingine  wamiliki wa chuo hicho ni International Mission Board ya  jumuiya kuu ya Wabaptisti ya Marekani ambapo awali chuo hicho kilikuwa kikitumika kutoa mafunzo ya dini pekee. Mwenyekiti wa umoja wa wachungaji wa jumuiya kuu ya wabaptisti Arusha, Mchungaji Fredrick Mahanyo alisema, Kanisa la Baptisti Tanzania si wamiliki wa chuo hicho. “Askofu Manase ameteka uongozi wa chuo na ameanzisha hilo kanisa lake ndani ya taasisi na hivyo kusababisha chuo kuzuiwa kufanya udahili kutokana na kushindwa kufikia vigezo vya TCU,” alisema. Hata hivyo, Askofu Manase alikanusha kuteka chuo hicho na kueleza wanaomtuhumu wanapaswa kutoa vielelezo vya umikili wa chuo hicho. “Hao wachungaji ni kina nani, kuna baptisti nyingi, tuna Bible Baptisti na Baptisti Convention, hao ni nani, kama wana ushahidi wakupe nyaraka  sisi tuna taratibu zetu,” alisema. Mchungaji mwingine wa jumuiya hiyo, Justine Mollel alisema tangu Askofu huyo achukue uongozi, katika chuo hicho mwaka juzi, kumekuwepo uzembe wa watendaji ofisi ya taaluma, wizi wa vyeti vya chuo na wanachuo kupewa matokeo ya uongo. “wafanyakazi wanapolalamika wengi wameachishwa kazi lakini pia uongozi wa chuo umekuwa ukiingilia uongozi wa kanisa  la Baptisti Tanzania ambalo halijasajiliwa nchini,” alisema. Mchungaji Alphayo Michael alisema wanaomba Serikali kuingilia kati kutatua mgogoro huo, kwani sasa wanafunzi waliokuwa wanasoma chuo hicho wanataabika na wafanyakazi. “Jumuiya kuu ya Wabaptist hatuna cheo cha Askofu, lakini kuna mtu anajiita Askofu na amekiteka chuo na kukifanya ni mali yake kupitia Kanisa lake la Tanzania Baptisti ambalo halijasajiliwa nchini,” alisema. Tume ya vyuo vikuu Septemba 20, ilikifungia chuo hicho kutokana na kushindwa kutimiza masharti, likiwepo la kuongeza walimu, kurekebisha maabara na kuwalipa watumishi stahili zao. Chuo cha Mount Meru hadi kinasitishiwa usaili, kilikuwa na zaidi ya wanafunzi 200 ambao tayari wote wameondolewa na walimu 60 ambao hadi sasa wamesimamishwa kazi kutokana na chuo kufungwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz