Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chanjo ya saratani mabinti Dar kuanza leo

Mon, 23 Apr 2018 Chanzo: habarileo.co.tz

WATOTO 24,097 wa kike wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi (HPV) kwa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia leo. Idadi hiyo ni ya watoto walio shuleni na wale ambao hawapo shuleni, ilimradi wawe wamefikisha miaka 14 mwaka huu.

Awali akizungumza katika semina ya waandishi wa habari kuhusu chanjo hiyo, Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto wa Mkoa huo, Ziada Sellah alisema chanjo hiyo ni kinga dhidi ya virusi vya HPV, vinavyosababisha saratani ya mlango wa kizazi.

Alisema huduma hiyo ya chanjo, itatolewa katika vituo 270 ambavyo vitakuwa katika manispaa zote tano za Mkoa huo za Ilala, Kinondoni, Ubungo, Temeke na Kigamboni.

Kwamba chanjo hiyo inakinga virusi aina ya 6,11,16, na 18 vinavyosababisha saratani hiyo Alitaka jamii kuondoa dhana potofu kuwa chanjo hiyo siyo salama kwa matumizi ya watoto hao.

Alisema kuwa chanjo ni salama, kwa kuwa imethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA). Alisema pia chanjo hiyo itatolewa mara mbili kwa watoto, watakaokuwa hawana maambukizi ya Virusi vya Ukimwi. Lakini, watakaobainika kuwa na maambukizi hayo, watapewa dozi tatu za chanjo ili waweze kupata kinga kamili.

"Watapewa dozi ya kwanza wakifikisha miaka 14 dozi ya pili itatolewa baada ya miezi miwili kupita tangu apewe dozi ya kwanza na dozi ya tatu atapewa baada ya miezi sita tangu apewe dozi ya kwanza," alisema.

Alisema wasichana hao ambao watabainika kuwa na VVU, watapewa dozi ya kwanza shuleni dozi ya pili kituoni na dozi ya tatu watapatiwa shuleni.

Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda akifungua mkutano, uliowashirikisha wadau mbalimbali baada ya kumalizika kwa semina ya waandishi wa habari, alisema chanjo hii ni muhimu kwa wasichana hao, kwa kuwa pia itasaidia kuipunguzia serikali gharama, ambazo wangetumia kuwahudumia baada ya kukutwa na tatizo.

Makonda alitoa rai kwa wasichana walio na umri huo, kujitokeza kwa wingi na wazazi kushiriki kuwahamasisha ili lengo lililowekwa na serikali la kutoa chanjo hiyo, litimie.

Aliwataka wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wao, wajitokeze katika maeneo yao kwa ajili ya kuhamasisha umuhimu wa chanjo hiyo.

Aliwaagiza wananchi kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili wajue mapema, kama wana maambukizi na kupata tiba mapema, kabla ya ugonjwa haujafikia hatua mbaya.

Mwakilishi wa Mpango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Lotalis Gadau alisema chanjo hiyo, inatolewa kwa wasichana hao wenye umri wa miaka 14 baada ya watu wazima, kwa kuwa asilimia kubwa, bado hawajaanza kujihusisha na masuala ya mapenzi.

Chanzo: habarileo.co.tz