Kampuni ya Moderna imesema inakuja na chanjo za saratani(kansa), magonjwa ya moyo na mishipa na magonjwa yanayohusiana na kinga za mwili ambapo zitakuwa tayari ifikapo 2030 lengo likiwa ni kuokoa Mamilioni ya maisha ya Watu.
Dk Paul Burton, Afisa Mkuu wa matibabu wa kampuni ya Moderna amesema anaamini kampuni hiyo itaweza kutoa chanjo na matibabu kwa magonjwa ya kila aina ndani ya muda wa miaka mitano.
Kampuni hiyo, ambayo iliunda chanjo inayoongoza ya ugonjwa wa Corona, inatengeneza chanjo ya saratani ambayo inalenga aina tofauti za uvimbe na kwamba maambukizi mengi yanayoleta changamoto za kiafya yataweza kutibiwa kwa sindano moja ikiruhusu Watu walio katika mazingira magumu kulindwa dhidi ya virusi vya Corona, homa na virusi katika mfumo wa kupumua (RSV), pia matibabu ya mRNA yanaweza kupatikana kwa magonjwa adimu na sugu ambayo kwa sasa hayana dawa.