Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chanjo ya corona kutolewa bure

8089cbc913d9550bd18365cf7c503282 Chanjo ya corona kutolewa bure

Mon, 5 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SERIKALI imekamilisha mwongozo wa uingizaji na utunzaji wa chanjo ya Covid-19 anobainisha kuwa itatolewa bila malipo na haitaruhusu uingizaji chanjo kwa ajili ya kufanya biashara.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Abel Makubi, alisema hayo jana jijini Dodoma.

Serikali pia imetoa mwongozo wa udhibiti wa maambukizi ya Covid-19 katika shule na vyuo ambao pamoja na mambo mengine kwa shule za bweni umeelekeza umbali wa kitanda kimoja na kingine kuwa mita moja na mabasi ya shule yawe na vitakasa mikono.

Profesa Makubi aliwaeleza waandishi wa habari wizara imekamikisha mwongozo wa kuingiza na kutunza chanjo ya Covid-19. Alisema chanjo serikali imebeba mzigo wa gharama kama ilivyo kwa chanjo nyingine na utoaji wake utakuwa wa hiyari.

Profesa Makubi alisema pia kwa kuzingatia mwongozo huo, serikali hautaruhusu uigizaji wa chanjo nchini kwa nia ya kufanya biashara.

Alisema hata kama kutakuwa na chanjo za msaada zitapita kwenye mfumo wa serikali ili kuzichunguza kabla ya kutolewa kwa wananchi.

“Tutachunguza kwanza ili kujiridhisha kabla ya kuamua kama ipokelewe au isipokelewe, hivyo hatutapokea msaada wa chanjo kiholela, lazima tufuatilie imetoka wapi inatengenezwa wapi. Maana lengo kuu la serikali ni kulinda wananchi wake hata awe mmoja,” alisema Profesa Makubi.

Alisema mchakato wa kupata chanjo unaendelea na kwamba itaanza kutolewa kwa makundi maalumu wakiwemo wasafiri.

“Tunategemea labda kwenye mwezi wa 12 au Januari kuanza kutoa kwa wenye utayari,” alisema Profesa Makubi.

Akaongeza: “Pia tunahitaji kama miezi sita kwa ajili ya kufanya tafiti kadhaa za kujiridhisha maeneo fulani kabla ya kuanza kutoa chanjo, hii tahadhari ya kujiridhisha kabla ya kuzitumia tumekuwa tukifanya kwa chanjo nyingine. Tunafanya tafiti hizi ili kuhakikisha chanjo tunayoitoa ni salama, usalama wa wananchi ndio kipaumbele na si kitu kingine. ”

Alisema pia wizara imehuisha mpango wa tatu wa kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 na pia kuanza mkakati ya kujenga kiwanda cha kutengeneza chanjo ikiwemo ya ungonjwa wa Covid-19 nchini ambacho makadirio ya awali kitagharimu Sh bilioni 80.

Mwongozo wa shule na vyuo

Profesa Makubi alisema imepitia upya mwongozo wa kudhibiti wa maambukizi ya Covid-19 katika shule, vyuo na taasisi za elimu nchini iliyotolewa mwaka 2020 na umefanyiwa maboresho machache.

Alisema mwongozo huo unalenga kuweka mazingira wezeshi katika maeneo ya taasisi za elimu vikiwemo vyuo, shule za sekondari, shule za msingi na awali na vituo vya kulelewa watoto ili waendelee na masomo katika kipindi cha mlipuko.

Mwongozo umezingatia maeneo manne ambayo ni maandalizi ya mazingira na taasisi za elimu kabla ya kufunguliwa, uchunguzi wa afya, usafiri wa kwenda na kurudi shule na vyuo na mazingira ya kujifunzia.

Alisema mwongozo unaitaka wizara ya elimu, Ofisi ya Rais TAMISEMI na wizara zinazosimamia vyuo na taasisi za mafunzo wahakikishe mazingira yanakuwa salama kabla ya watoto kurejea shuleni.

“Wanatakiwa kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kunawia mikono vyenye maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono kwa ajili ya usafi binafsi katika kila chumba cha madarasa, ofisi lango kuu, kila bweni, makataba, bwalo la chakula, vyoo na maneno mengine maalumu,” alisema Profesa Makubi.

Alisema pia shule vyuo na taasisi zenye vituo vya kutolea huduma za afya watumishi wote wanaohusika wapewe elimu juu ya kuwahudumia wanafunzi, walimu na wafanyakazi wote watakao shukiwa kuwa na Covid-19 na kuondoa unyanyapa.

Profesa Makubi alisema uongozi wa shule, vyuo na taasisi wanapaswa kuweka utaratibu wa upatikanaji wa barakoa katika maeneo yao kwa gharama nafuu.

“Watoto wenye umri chini ya miaka 5, wenye ugonjwa wa moyo, selimundu, mfumo wa hewa Kama pumu na matatizo mengine ya kiafya hawaruhusiwi kuvaa barakoa,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz