Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chanjo sasa kupatikana vituo vyote nchini

5d40e8ba75ac9d4ea541c846a19a1416.jpeg Chanjo sasa kupatikana vituo vyote nchini

Wed, 22 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inahakikisha chanjo zote za kuzuia magonjwa yanayozuilika zinapatikana kwa wakati katika vituo vinavyotoa chanjo.

Mratibu wa Malaria Mkoa wa Pwani, Mhando Muya alisema juzi mjini Kibaha wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Morogoro yaliyohusu kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa huduma za chanjo.

Muya aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alisema serikali kwa kushirikiana wa wadau mbalimbali imewezesha upatikanaji wa chanjo zote za kuzuia magonjwa yanayozuilika.

Aliyataja magonjwa hayo ni kifua kikuu, dondakoo, kifaduro, polio, surua, rubela, pepopunda, homa ya ini, homa ya uti mgongo, kichomi, kuhara na saratani ya mlango wa kizazi.

Alisema mafanikio ya chanjo yametokomeza ugonjwa wa ndui, magonjwa ya dondakoo, kifaduro, polio na pepopunda ambayo yamedhibitiwa na wodi za surua zimefungwa.

"Mafanikio haya makubwa yametokana na kuwapatia chanjo asimilia 80 ya watoto umri wa chini ya mwaka mmoja nchini,"alisema.

Muya alisema kwa takwimu za mwaka 2018/ 2019, Tanzania imefikia kiwango cha uchanjaji kwa asilimia 99 na hiyo ni hatua iliyofikiwa na serikali kupambana na magonjwa yanayozuilika.

"Wizara imekusanya na kutunza takwimu kwa njia ya mfumo kutumia vishikwambi,"alisema.

Alisema ingawa kiwango cha chanjo kiko juu bado kuna watoto wasiokamilisha chanjo na wasiochanjwa katika baadhi ya maeneo, hivyo kusababisha uwezekano wa mlipuko wa surua.

Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dafrosa Lyimo alisema magonjwa yanayozuilika kwa chanjo husababisha ulemavu na kifo.

Alisema surua husababisha nimonia, degedege, mtindio wa ubongo, utapiamlo, upofu na kifo, wakati Rubella husababisha ugonjwa wa moyo kwa watoto, uziwi, figo, mtindio wa ubongo, matundu katika moyo na uti wa mgongo.

Polio huleta ulemavu wa viungo na kifo hivyo chanjo inabaki kuwa njia rahisi na sahihi ya kumlinda mtoto na kuwa na familia yenye afya.

Chanzo: habarileo.co.tz