Dar es Salaam. Ikiwa ni takriban miaka 40 ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi, matumaini yameanza kuonekana baada ya chanjo mpya ya kupambana na virusi vya ugonjwa huo (VVU) kuonyesha mafanikio.
Chanjo hiyo inayofanyiwa majaribio imeonyesha mafanikio kwa kuongeza kinga ya mwili na kuzuia virusi kumuathiri nyani.
Naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alipoulizwa na Mwananchi jana kuhusu chanjo hiyo alisema hadi sasa hakuna tiba ya Ukimwi, lakini Serikali inafuatilia kwa karibu tafiti zinazofanyika kokote duniani.
Alisema endapo tafiti hizo zitaonyesha mafanikio Tanzania haitasita kuzitumia.
Taarifa za utafiti wa chanjo ya mpya ya majaribio zilizochapishwa na Shirika la Habari la AFP zinasema kutokana na chanjo hiyo inayofanyiwa majaribio kuonyesha kuwa haina madhara kwa binadamu, wanasayansi wamepata kibali cha kuendelea na hatua ya pili ya majaribio.
Chanjo ya pili itafanyiwa majaribio kwa wanawake 2,600 nchini Afrika Kusini.
Hata hivyo, wanasayansi wanasema licha ya kuonyesha mafanikio, hakuna uhakika kwamba chanjo hiyo itafaa katika awamu ijayo.
Majaribio ya chanjo hiyo yamepewa jina Imbokodo lugha ya Kizulu ya Afrika Kusini ikimaanisha mwamba.
Matokeo ya utafiti wa chanjo hiyo awamu ijayo yanatarajiwa kutolewa mwaka 2021/22.
“Ingawa matokeo haya yanatia matumaini lakini hatuwezi kujipa uhakika katika (ile) ijayo,” alisema mkuu wa utafiti huo, Profesa Dab Barouch wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Havard kama alivyokaririwa na AFP.
“Kwa sababu iliwakinga robo tatu ya nyani hiyo haimaanishi majaribio yajayo yatatupa uhakika wa asilimia 100.” Majaribio ya awali ya chanjo ya VVU yalichapishwa katika jarida la afya la Lancet mwaka 2015.
Katika majaribio hayo watu wazima wenye umri wa kati ya miaka 18 na 50 wasiokuwa na VVU walitumika kama sampuli ya majaribio ambazo zilichukuliwa katika nchi za Afrika Mashariki, Thailand, Marekani na Afrika Kusini.
Akizungumzia mapambano dhidi ya VVU, mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Dk Leonard Maboko alisema ni muhimu zaidi watu kujua afya zao na kwamba, bado kuna idadi kubwa ya watu ambao hawajapima afya zao.
Alisema kwa sasa mapambano yameelekezwa katika kuhamasisha jamii kuhusu upimaji wa virusi.
“Ni asilimia 52 tu ya Watanzania wanaojua afya zao. Ina maana ni nusu tu ya wanaojua na zaidi ya nusu hawajui,” alisema.
Dk Maboko alisema kampeni ya kupima afya ili kujua hali iliyozinduliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mjini Dodoma hivi karibuni inawalenga zaidi wanaume.
Alisema mpango uliopo kwa sasa ni kufikia 90 tatu zikiwa na maana ya mafanikio kwa asilimia 90 ya watu kupima na kutambua afya zao; asilimia 90 ya kuanza kutumia dawa kwa usahihi na asilimia 90 ya tatu ni kupunguza idadi ya virusi mwilini.