Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chanjo mbili mpya za corona kuja

Chanjo4 Chanjo mbili mpya za corona kuja

Wed, 15 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Afya imesema kufikia mwisho wa mwaka huu mpaka mwanzoni mwa mwaka ujao, inatarajia kupokea chanj nyingine mbili za ugonjwa wa Corona.

Akizungumza katika mkutano wa wamiliki, wahariri na waandishi wa habari Dar es Salaam jana ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuhusu umuhimu wa chanjo ya ugonjwa wa corona, Mkurugenzi wa Chanjo wa Wizara hiyo, Dk. Florian Tinuga, alisema kati ya hizo chanjo itakayoanza kuletwa kati ya hizo mbili ni Modema ndani ya mwezi au mwanzoni mwa Januari mwakani.

Alisema baada ya Modema, itakayofuata ni ya Sinovac ambayo na yenyewe italetwa nchini mwanzoni mwa mwaka ujao.

"Kwa hiyo mpaka mwanzoni mwa mwaka ujao tutakuwa tumeingiza aina tano za chanjo kati ya tisa ambazo zimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa sababu mpaka sasa tumeingiza aina tatu tayari," alisema Dk. Tinuga.

1,217,628 WACHANJA

Dk. Tinuga alisema mpaka sasa idadi ya Watanzania waliokwisha kuchanja ni milioni 1,217,628 sawa na asilimia 2.11 na kwamba lengo la serikali ni kuchanja asilimia 60 ya Watanzania wote. 

Alisema asilimia 80 ya wananchi wanaougua ugonjwa wa corona hawaendi hospitali, na kwamba wanaofika hospitalini baada ya ugonjwa huo ni asilimia 15 tu, huku asilimia tano pekee ndio hubainika kuugua na kuwa mahututi kisha kulazwa katika vitengo vya uangalizi maalum (ICU).

"Kwa hiyo bado kuna tatizo la wananchi kutokwenda kwenye vituo vya afya pale wanapougua ugonjwa huu, wengi wao wanaugulia nyumbani," alisema Dk. Tinuga.

Dk. Alex Mphuru kutoka UNICEF, alisema chanjo ya Pfizer imeshaanza kutumika kuchanja watoto katika baadhi ya nchi duniani, na kwamba bado utafiti mbalimbali unaendelea kwa ajili ya chanjo upande wa kundi la watoto.

Mtaalamu wa mawasiliano UNICEF, Usia Nkhoma, alisema bado kuna haja kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa chanjo ya ugonjwa wa corona. 

Mwenyekiti TEF, Deodatus Balile, alisema kama vyombo vya habari vitaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo ya ugonjwa huo. 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS),  Prof. Deodatus Kakoko, alisema uvumi ulioenea juu ya athari za chanjo  za UVIKO -19 kwa watakaochoma ulizorotesha kwa kiasi kikubwa kasi ya utoaji chanjo  ilipoingia kwa mara ya kwanza nchini.

Alisema siku 43 za mwanzo walitoa chanjo 300,000 tu Tanzania nzima na hii ilitokana na imani potofu kuhusu chanjo hiyo na  mwitikio ulianza kuwa mkubwa baada ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu usalama wa chanjo hizo.

Alisema baadhi ya uvumi ulioenea ni  kuwa  chanjo ya UVIKO inaathiri uzazi kwa wanawake na kuwafanya wasizae, inaathiri nguvu za kiume, imelenga kumaliza wa Afrika,  inatoa taarifa za siri za mtu na kuwa waliougua  COVID -19  hawana haja ya kupata chanjo hiyo.

Akitolea majibu ya uvumi huo, Prof. Kakoko alisema si kweli kwa kuwa hakuna ushahidi wowote wa kisayansi unaothibitisha ukweli wa uvumi huo na kuwa hata kama mtu aliugua ugonjwa huo anahitaji kupata chanjo kwa kuwa kazi yake ni kuweka na kuimarisha kinga za mwili.

Mpaka sasa Tanzania imeshapokea aina tatu za chanjo ya ugonjwa wa corona ikiwamo Johnson &Johnson, Pfizer na Sinopharm.

Imeandikwa na Elizabeth Zaya na Jenifer Gilla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live