Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Changamoto ya maradhi ya moyo inavyoumiza wadau

10772 Moyo+pic.png TanzaniaWeb

Thu, 5 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Miongoni mwa maradhi yasiyoambukiza ni pamoja na ugonjwa wa moyo ambao huchangia vifo kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia 36 ya vifo nchini husababishwa na maradhi yasiyoambukiza.

Maradhi ya moyo ni pamoja na shinikizo la juu la damu, la chini, kuziba kwa mishipa ya moyo, kufunikwa na mafuta kwa mishipa hiyo na moyo kuwa mkubwa.

Katika mjadala wa kwanza wa Mwananchi Jukwaa la Fikra kuhusu maradhi yasiyoambukiza, wadau wameshauri mbinu za kupambana nayo ikiwamo kubadili mtindo wa maisha.

Mjadala huo uliandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) kwa kushirikiana na Kituo cha Televisheni cha ITV na Redio One.

Mwananchi limezungumza na wataalamu mbalimbali wa afya waliojikita katika maradhi ya moyo.

Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Pallangyo anasema kupanda kwa shinikizo la damu ni miongoni mwa ugonjwa wa moyo unaoathiri watu wengi.

Anasema ugonjwa huo unahusisha kuongezeka kwa mgandamizo wa msukumo wa damu kwenye mishipa ya damu.

Maradhi mengine ni koronari za moyo ambao husababishwa na mafuta kuganda au kuziba kabisa kwa ateri za moyo. Hali hii husababisha upungufu wa damu katika sehemu ya moyo ambayo hupata damu kupitia mishipa hiyo.

Ugonjwa mwingine ni kuganda kwa mafuta kwenye ateri za moyo.

“Hali hii ni kitendo cha mafutamafuta kuganda kwenye mishipa ya ateri. Kuganda kwa mafutamafuta huko kunaweza kuchukua miaka mingi, kadri miaka inavyosonga mbele ndivyo mafuta haya yanazidi kuwa magumu na kuzuia msukumo wa damu yenye oksijeni kwenye moyo.

“Yakiziba kabisa kwenye ateri husababisha misuli ya moyo kukosa damu yenye oksijeni, huweza kumsababishia mtu maradhi mengine yanayoitwa anjina (angina), kwa maana ya maumivu makali ya kifua na mshtuko,” anasema.

Anataja maradhi mengine kuwa ni anyurismu (aneurysm) ambapo mishipa ya ateri huvimba kama puto kutokana na kuharibika kwa mishipa au kudhoofika kwa kuta za mishipa.

Kadhalika anataja ugonjwa mwingine wa moyo ujulikanao kwa jina la rumatiki ya moyo (rheumatic) ambao husababisha kupungua utendaji kazi wa moyo kutokana na ogani hiyo kuwa na vivimbe tangu mtoto anapozaliwa na mara nyingi husababisha vifo wakati wa utotoni.

Kwa mujibu wa WHO, maradhi yasiyoambukiza yakiwamo ya moyo, kila mwaka huua watu milioni 38 duniani.

Takwimu kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania (Pat), zinaonyesha watoto 13,600 huzaliwa kila mwaka wakiwa na maradhi aina mbalimbali ya moyo, huku 3,400 kati yao wakihitaji kufanyiwa upasuaji.

Chanzo maradhi ya moyo

Dk Pedro anasema chanzo ni kutozingatia kanuni za ulaji bora, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi nyingi na lehemu nyingi.

“Unene uliopitiliza pamoja na kutofanya mazoezi ya mwili na viungo mara kwa mara huchochea pia uwezekano wa magonjwa ya moyo,” anasema.

Wakati mwingine maradhi ya moyo hutokana na historia ya ugonjwa huo katika familia.

“(Watu) wenye umri wa kuanzia miaka 50 wana uwezekano mkubwa kupata ila wanaume wapo hatarini zaidi ya kupatwa na tatizo hili mapema zaidi ikilinganishwa na wanawake,” anasema.

Anautaja uvutaji wa sigara au utumiaji wa tumbaku kwa kutafuna au kunusa (ugoro), husababisha pia sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa, hivyo kuongeza hatari ya maradhi ya moyo.

“Kemikali zinazopatikana kwenye tumbaku huharibu seli za damu. Uharibifu huo wa seli huingilia muundo na utendaji mzuri wa mishipa ya damu. Kuharibika kwa mishipa ya damu kunachochea mafuta kuganda kwenye mishipa, kitaalamu atheroskerosis,” anasema.

Anaongeza kuwa unywaji pombe kupita kiasi na utumiaji wa dawa za kulevya ni hatari akisisitiza kuwa pombe na dawa za kulevya hudhoofisha misuli ya moyo na mishipa ya damu.

Dalili kuu

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohammed Janabi anasema bahati mbaya mtu anaweza asione dalili zozote za moja kwa moja za maradhi ya moyo hadi mishipa ya damu ya moyo inapoziba kabisa au kushindwa kuruhusu damu kwa kasi na kiwango kinachotakiwa.

“Tunashauri kupima afya mara kwa mara, kwani hakuna dalili inayojitokeza moja kwa moya kwa wagonjwa wa aina hii, hadi pale moyo wenyewe unaposhindwa kufanya kazi ghafla (heart attack) au mtu anapopata kiharusi (stroke),” anasema.

Dalili kuu za maradhi ya moyo ni pamoja na maumivu ya kifua, moyo kwenda mbio na kumfanya mtu akose pumzi au kushindwa kupumua.

Nyingine ni kuvimba miguu, tumbo na mishipa ya shingoni kujitokeza nje, maumivu ya mgongo, mabega, shingo na taya, tumbo kujaa, kichefuchefu na kutapika, kukosa usingizi, kupoteza fahamu na kikohozi kisichokwisha.

Kodi ya vifaa

Akizungumza wakati wa mjadala wa Mwananchi Jukwaa la Fikra, Juni 28, Meneja Manunuzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Sylvester Maige alipendekeza kuwa ili Wizara ya Afya iweze kupambana na maradhi yasiyoambukiza, hasa katika kuzuia maambukizi ni vyema iwekeze kwenye vifaa vya mazoezi.

Anasema wizara hiyo ikishirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanapaswa kupunguza kodi ya vifaa vya kufanyia mazoezi ili viingie kwa wingi nchini na Watanzania wengi wamudu kuvinunua.

“Nina imani kama vikipunguzwa hata gharama za mazoezi zitapungua na wengi watashiriki na kuweza kujipa kinga. Tiba ya maradhi haya ina gharama kubwa, hivyo ni vyema tukapambana kwani dawa za saratani, shinikizo la damu zina gharama kubwa na mtu anatumia kwa muda mrefu, hivyo tukihamasisha watu kufanya mazoezi, kula vyakula vyenye afya, kupima afya mara kwa mara tutafanikiwa,” anasema Maige.

Chanzo: mwananchi.co.tz