Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Changamoto tano za malezi ya mtoto katika balehe

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Huu ni wakati mabadiliko mengi ya kimwili, kiakili, kihisia, na mahusiano yake kijamii hutokea. Mabadiliko ya kibailojia yanayoleta kubadilika kwa homoni hupelekea kuanza. Wavulana huanza kuota ndevu na nywele makwapani na sauti zao kuwa nzito.

Wasichana nao huota nywele makwapani, matiti kukua na huanza kupata hedhi. Mara nyingi hupatwa na wasiwasi kuhusu mabadiliko haya na jinsi watu wanavyooneka kwa watu.

Huu ndio wakati ambapo mwanao anaweza kupata shinikizo rika kutumia pombe, sigara, shisha, dawa za kulevya na hata kufanya ngono. Changamoto nyingine zinaweza kuwa kupoteza hamu ya kula, msongo wa mawazo, na kadhalika. Katika umri huu, watoto hufanya maamuzi wenyewe kuhusu marafiki, michezo wanayoipenda, vitabu watakavyo kusoma, na shule waitakayo. Uwezo wa kujitegemea huongezeka maradufu, ingawa bado uangalizi wa wazazi ni muhimu sana.

Huu ni wakati ambao watoto wanjali muonekano wao wa nje; mavazi, kimo chao, unene/wembamba – mavazi. Yaani mtoto sasa anataka kuwa na staili ya kunyoa/kusuka ya ‘kipekee’ inayomfurahisha na kumpa ‘kujiamini’. Hii ni fursa kwako mzazi kumpa majibu ya kweli kuhusu mahusiano, ngono, matumizi ya madawa ya kulevya n.k. Usimung’unye maneno – anajua.

Mwanao ghalfa tu anakuwa mkali au mkimya na ‘mkorofi’ asiyetaka ‘kukusikiliza’. Humjui tena! Usikate tamaa onyesha kujali kwa dhati mambo yanayohusu maisha yake, shule nk. Mwongoze kufanya maamuzi sahihi huku ukikubaliana na kusimamia maamuzi yake. Muhimu sana ajue kwamba unamsikiliza na unatekeleza makubaliano yenu. Vitendo.

Haonekani nyumbani na hata unapokutana naye huwa na ‘wenzake’ katika ‘mambo yao.’ Panga kukutana na wafahamu rafiki zake. Wataalamu wa malezi wanashauri uweke bidii katika kuwafahamu marafiki wa mtoto wako kwani ‘mustakabali’ wake uko juu ya maamuzi yao. Ukiweza kupenyeza na ‘kuwasoma’ basi sehemu kubwa ya wasiwasi wako imejibiwa. Wafanye sehemu ya familia na nyumbani kwako iwe ‘kijiwe’ chao.

Msongo wa mawazo unaotokana na kutojua majibu ya maswali mengi aliyonayo mtoto hupelekea kupoteza mwelekeo na hata kukata tamaa. Zungumza naye huku ukijiepusha na makaripio. Namna hii atapata faraja na kuelewa kuwa yuko katika umri wa mpito na kuwa sasa utu uzima unaingia na majukumu yanazidi kuwa mengi. Afahamu kuwa wewe ni kimbilio lake na anaweza kukueleza changamoto zake na ukakubaliana na mapendekezo ya namna kuzitatua toka kwake.

Wataalamu wa malezi wanashauri kuwa michezo inaweza kuwa sehemu nzuri ya kupunguza msongo na upweke waupatao watoto wa rika hili. Acheze shuleni na hata mtaani panapo fursa ya kufanya hivyo. Anaweza pia kufua nguo, kufyeka, kusafisha uwanja wa nyumbani – alimradi yuko katika shughuli mojawapo ya kuamsha viungo.



Chanzo: mwananchi.co.tz