Miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afya, imekuwa kielelezo cha mafanikio ya utawala wake ikiwa ni sehemu muhimu ya kuimarisha afya ya jamii na kulinda nguvu kazi ya Taifa.
Amefanikiwa kwa sehemu yake kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/25 kifungu cha 83 inayoeleza kuwa: “Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM itaendelea kutoa kipaumbele katika sekta ya afya kwa kuwa inagusa maisha ya Watanzania na ustawi wa Taifa.”
Rais Samia anatimiza miaka mitatu ya utekelezaji wa ilani hiyo tangu aapishwe kushika nafasi ya kuiongoza Tanzania Machi 19, 2021 akipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, John Magufuli.
Katika kipindi hicho, amechochea mageuzi katika utoaji wa chanjo, kuongeza ajira za watumishi sekta ya afya, kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaatiba, vitendanishi, utoaji wa chanjo, udhibiti wa magonjwa ya mlipuko, kuboresha afya ya msingi pamoja na kusaini muswada wa Sheria ya Bima Afya kwa Wote.
Changamoto nazo zipo
Pamoja na mazuri hayo aliyoyafanya wadau wa masuala ya afya wanasema bado kuna maeneo ya kufanyiwa kazi kama anavyobainisha mtaalamu mkongwe wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige.
Dk Mzige anasema bado hakuna mipango shirikishi kati ya afya Tamisemi na maeneo husika, kwani kila hospitali ya wilaya ilipaswa kuwa na wataalamu wa fani za kibingwa, upasuaji, daktari wa magonjwa ya ndani na daktari wa magonjwa ya akina mama na uzalishaji pamoja na daktari wa watoto.
“Yale magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni somo la kinga zaidi, lakini bado tumeachia matangazo ya vyakula visivyo vya lishe, dawa na vipodozi mitandaoni bila kufuatilia vinavyoathiri afya za Watanzania.
“Matangazo yetu ni batili, yaeleze madhara ya pombe, sigara, energy drinks pia. Watumishi vijijini ni muhimu kutoa elimu ya kinga na usafi wa mazingira. Tahadhali zote zichukuliwe,” anasema Dk Mzige ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya kabla hajastaafu mwaka 2005.
Hata hivyo, Mtaalamu wa maabara wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Alex Mlwisa anasema, jambo ambalo Rais Samia anapaswa kulivalia njuga ni mapitio ya vifurushi vya bima ya afya na sera kwa ujumla, ili kukidhi matakwa ya wateja wake kwani afya ni msingi wa uchumi wa Taifa.
Naye mtaalamu na mshauri wa masuala ya afya, Dk Elisha Osati anasema rasilimali watu bado ni changamoto kubwa ambayo Rais anapaswa kuishughulikia.
Anasema wafanyakazi katika sekta ya afya wanaohitajika katika hospitali za mijini na vijiini bado ni wachache, hata masilahi ya wafanyakazi nayo yako chini ukilinganisha na kazi wanazofanya.
Dk Osati anasema changamoto inayokuja nchi imewekeza kwenye miundombinu na vifaa vya kisasa lakini suala la uchangiaji fedha au uwekaji fedha katika sekta hiyo usipozingatiwa, yote yaliyofanywa yatakuwa sawa na bure.
Akijibu hoja ya suala la rasilimali watu, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji katika eneo hilo ikiwemo kuajiri watumishi wapya wa sekta ya afya na kusomesha wataalamu katika fani za ubingwa na ubobezi.
“Wataalamu 35,450 wa kada mbalimbali wameajiriwa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2023. Aidha, jumla ya ajira za mikataba kwa watumishi wa afya 2,836 kupitia miradi mbalimbali ya Serikali zilitolewa,” anasema.
Anasema kuna ongezeko la madaktari bingwa nchini hadi kufikia mwaka 2023 wamefikia 2,464 ukilinganisha na madaktari bingwa 805 mwaka 2020 na kwamba bado wanasomesha wengine kupitia Samia Scholaship ambapo mpaka sasa Sh22 bilioni zimetumika.
Anasema maboresho yaliyofanyika yamefanikisha hadi sasa taasisi za afya nchini kutoa tiba utalii kutoka nchi za Comoro, Burundi, Malawi, Kenya, Congo DRC, Uganda na Zambia.
Mafanikio
Miongoni mwa mambo yaliyoweka historia chini ya uongozi wa Rais Samia, ni kupitishwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo tayari imesaniwa na kiongozi huyo.
“Ndugu zangu, pamoja na shabaha ya Mapinduzi ilikuwa ni kutoa tiba bure kwa wanachi, tumetoka mbali, sasa ni miaka 60 tumekwenda mbele mno kuliko tulipokuwa, kule hakukuwa na mwananchi mwenye uwezo wa kuwa na bima ya afya na tumefaidi kwa muda mrefu lakini tulipofikia ili tuweze kutoa huduma endelevu, bima ya afya haiepukiki,” alisema Rais Samia baada ya kufungua Hospitali ya Mjini Magharibi Zanzibar.
Malengo makuu ya Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ni kuwawezesha wananchi wote kuwa na uhakika wa kupata huduma za afya wakati wote bila kikwazo cha fedha, hususani kwa kaya masikini.
Ununuzi wa vifaatiba kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya wagonjwa vyenye thamani ya Sh290.9 bilioni kuanzia ngazi ya Hospitali ya Taifa hadi hospitali za halmashauri nao umefanya sekta hiyo ipige hatua.
Takwimu zinaonyesha huduma za kipimo cha CT Scan sasa zinapatikana katika hospitali 27 kati ya 28 za rufaa za mikoa na hadi kufikia Machi 2024 wagonjwa 15,386 walipatiwa huduma za kipimo cha CT Scan.
Pia idadi ya vitanda vya wagonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini imeongezeka kutoka 86,131 mwaka 2021 hadi 126,209.
Hata hivyo, eneo muhimu zaidi ni dawa ambapo Serikali imekuwa ikipeleka Sh20 bilioni kila mwezi. Upatikanaji wa fedha hizo umewezesha kuimarika kwa upatikanaji wa dawa muhimu na bidhaa nyingine za afya (aina 290) katika vituo vya kutolea huduma za afya vya umma kufikia asilimia 84 mwaka 2023, ikilinganishwa na asilimia 58 mwaka 2022.
Katika huduma za dharura na ajali, ili kuboresha eneo hilo majengo wa huduma za dharura yaongezeka, baada ya kukamilisha ujenzi wa majengo 23 ya kutoa huduma za dharura katika hospitali maalumu, kanda na mikoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba.
Upande wa ngazi ya msingi, ujenzi wa majengo ya dharura 82 katika ngazi za halmashauri unaendelea, ambapo 66 yamekamilika na yanatoa huduma na mengine 16 yako kwenye hatua ya ukamilishaji.
Miaka mitatu imewezesha kuanzishwa kwa majengo mahususi ya huduma za dharura na ajali 105 kutoka 7 yaliyokuwepo mwaka 2020. Aidha, hadi sasa jumla ya wateja 262,260 wamenufaika na huduma za dharura nchini.
Huduma za msingi, hospitali
Miongoni mwa mambo yanayotajwa katika uongozi wa miaka mitatu ya Rais Samia ni uboreshaji wa huduma za afya ya msingi.
Vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka vituo 8,549 mwaka 2021 hadi kufikia vituo 9,610 Machi 2024. Hii ni sawa na ongezeko la vituo 1,061, vikiwemo 523 vinavyotoa huduma ya kumtoa mtoto tumboni kutoka 340 vya awali.
Takwimu zinaonyesha ujenzi na kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi ambapo hospitali mpya za halmashauri 127 zimejengwa na ukarabati wa hospitali kongwe 50 za halmashauri umefanyika.
Ujenzi wa nyumba za watumishi 270 katika hospitali mbalimbali nchini, pamoja na mitambo 21 ya kuzalisha hewa tiba ya oksijeni kwa ajili ya wagonjwa mahututi na wagonjwa wa dharura.
Katika kuimarisha matibabu hospitali za rufaa, kumekuwa na ujenzi wa majengo mapya, ukarabati na kukamilisha ujenzi wa hospitali mpya katika mikoa mipya mitano, uliogharimu Sh1.02 trilioni.
Fedha hizo zilikamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara na awamu ya pili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato.
Pia kukamilisha ujenzi wa hospitali za Katavi, Njombe, Songwe, Simiyu na Geita pamoja na kuhamisha hospitali tano kutoka majengo yake ya zamani na kujenga mpya katika maeneo mapya, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma, Shinyanga, Singida, Mara na Lindi.