Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama cha madaktari chamlilia Dk Marealle

04e563796289cf6e0b2c280a1fe35d1e Chama cha madaktari chamlilia Dk Marealle

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

UONGOZI na wanachama wa Chama cha Madaktari wa upasuaji Tanzania ( TSA ), umesema Dk Paul Marealle 59 aliyefariki dunia Jumanne wiki hii katika Taasisi ya Mifupa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI), atakumbukwa kwa kupambania kutambulika kwa Chama cha Madaktari wa Upasuaji Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (COSECSA).

Rais wa TSA, Dk Catherine Mung’ong’o alieleza hayo jijini Dar es Salaam jana na kuongeza kuwa TSA imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo hicho.

Dk Mung’ong’o alisema Dk Marealle alikuwa mwanachama mwandamizi TSA na alishika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye chama hicho ikiwemo ya ujumbe kwenye kamati ya utendaji kwa miaka isiyopungua 10, Makamu wa Rais na hatimaye Rais wa TSA tangu 2014 hadi 2018.

Taarifa ya Dk Mung’ong’o ilieleza kuwa Dk Mareaalle alikuwa mwakilishi wa Tanzania katika Kamati ya Uendeshaji ya COSECSA mpaka alipofikwa na mauti.

Alisema mchango wake katika kuinua na kuendeleza taaluma ya upasuaji nchini na barani Afrika utakumbukwa daima ikiwa ni pamoja na kuziwezesha hospitali za wilaya ili wagonjwa wafanyiwe upasuaji karibu karibu na wanapoishi ili kupunguza gharama na kuzuia vifo wakati wakisubiri rufaa.

Taasisi ya Mifupa (MOI) imeeleza kusikitika kumpoteza Dk Marealle. Kaimu Mkuu Kitengo cha Uhusiano MOI, Patrick Mvungi alisema Dk Marealle amekuwa daktari bingwa wa mifupa kwa miaka 11.

Dk Marealle amefanya kazi MOI kwa miaka 24 akiwa miongoni mwa waanzilishi wa taasisi hiyo mwaka 1996. “Tumepoteza mtu muhimu sana, amekuwa kiongozi katika sehemu mbalimbali ndani ya taasisi na nje na amekuwa nguzo kubwa kuwajenga madaktari vijana ili kuimarika,” alisema Mvungi.

Alisema Dk Marealle alihudumia Watanzania kwa upendo, akifanya upasuaji kwa nyakati mbalimbali, jambo ambalo hadi wagonjwa wanapiga simu kuuliza ukweli wa kifo chake.

Daktari mwenzake katika idara ya mifupa MOI, Dk Kenedy Nchimbi alisema ni Dk Marealle alikuwa miongoni mwa madaktari waliopenda kusimamia taratibu za kazi, akijali haki za wagonjwa na kufuatilia kwa ukaribu ratiba za wagonjwa.

Alisema Dk Marealle aliwafundisha madaktari wengine na wamefanya kazi kwa upendo kuhudumiwa Watanzania.

Chanzo: habarileo.co.tz