Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bunge lataka sheria kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza

Fa1ab76d14fabdfcb14c853327f871ad.png Bunge lataka sheria kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza

Fri, 11 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bunge limeshauri iundwe sheria itakayosaidia kuwekeza kwenye kinga na udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza itakayobainisha kodi ya nyongeza ya bidhaa hatarishi kama vile tumbaku, pombe, vyakula vyenye sukari na chumvi nyingi.

Ushauri huo umo kwenye taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi ya shughuli zilizotekelezwa kwa kipindi cha Januari , 2021 hadi Januari 2022 iliyowasilishwa bungeni na kupitishwa na bunge juzi.

Kupitia taarifa hiyo iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati, Fatma Hassan Toufiq, wabunge wameshauri iundwe sheria kusaidia wananchi na serikali kuwekeza zaidi kwenye kinga huku ikisisitizwa kwamba sheria itakayoundwa iendane na uanzishwaji wa Mfuko wa Afya ambapo wananchi watachangia kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.

“Aidha sheria hii ibainishe kodi ya nyongeza ya bidhaa hatarishi kama tumbaku, pombe, vyakula vyenye sukari nyingi na chumvi nyingi . Itatumika kwenye huduma za afya kama sehemu ya kurejesha kwenye jamii iliyoathirika, lakini pia mkakati wa kudhibiti uzalishaji holela wa bidhaa zenye madhara kiafya ili kupunguza uhatarishi,” ilisema taarifa.

Ushauri mwingine ni kwamba serikali itenge ruzuku maalumu ambayo ingeweza kupatikana kama tozo maalumu zitokanazo na biashara ya bidhaa, kama tumbaku, vinywaji vyenye sukari nyingi, pombe, zinazochochea magonjwa sugu yasiyoambukiza na sehemu ya bima za magari kama huduma kwa jamii, kwa kampuni au bidhaa husika.

Kamati ilielezwa kwamba serikali kwa kutumia vyanzo mbalimbali inatarajiwa kutumia Sh trilioni 12.6 ndani ya miaka mitano ijayo, sawa na wastani wa trilioni 2.3 kila mwaka kupunguza asilimia 15 ya vifo visivyotarajiwa vinavyosababishwa na magonjwa hayo.

Aidha, ilibainika kuwa, zaidi ya asilimia 55.6 ya bajeti ya Wizara ya Afya imeelekezwa katika huduma za saratani, moyo, mishipa ya damu, kisukari, figo, selimundu na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa.

Bajeti hiyo imelenga zaidi katika upatikanaji wa bidhaa za afya hususani dawa na vifaa tiba ambavyo vinaongeza gharama kwa wananchi na taasisi zinazotoa huduma hizo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya kamati, tathmini za haraka za matibabu zilizofanywa na Chama cha Kisukari nchini kutambua gharama ilibainika kuwa, zaidi ya Sh bilioni 290 zinahitajika kwa mwaka kama gharama za dawa kwa wagonjwa milioni 1.5 wenye kisukari na shinikizo la juu la damu pekee.

Gharama hizi ni karibu sawa na asilimia 20 ya bajeti yote ya Wizara ya Afya. Upasuaji wa moyo au upandikizwaji figo huhitaji zaidi ya Sh milioni 20 kwa mtu mmoja, huku gharama za usafishaji damu kwa wagonjwa wa figo zikifikia Sh 300,000 kwa awamu moja.

Mwenyekiti alisema kamati ilipokutana na Wizara ya Afya kupokea taarifa kuhusu utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza, iliambiwa serikali kwa kutumia vyanzo mbalimbali inatarajiwa kutumia Sh trilioni 12.6 ndani ya miaka mitano ijayo.

Kiasi hicho ni sawa na wastani wa trilioni 2.3 kila mwaka kwa lengo la kupunguza asilimia 15 ya vifo visivyotarajiwa vinavyosababishwa na magonjwa hayo.

Kamati ilisema magonjwa yasiyoambukiza tishio kwa kwa afya za Watanzania wengi kwa zaidi ya asilimia 73 na pengine kusababisha kupelekea vifo.

Serikali imeshauriwa kufanya uwekezaji mkubwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa (RRH) zisaidie kusogeza huduma za magonjwa sugu yasiyoambukiza karibu zaidi na wananchi na hivyo kupunguza mzigo wa matibabu kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live