Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bugando waiomba Serikali kufikiria upya kodi taasisi za afya

Nafuu BGANDO HDU Bugando waiomba Serikali kufikiria upya kodi taasisi za afya

Thu, 18 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa bodi ya Hospitali ya Kanda ya Bugando, Askofu Renatus Nkwande ameiomba Serikali kufikiria upya kodi zinazotozwa kwa taasisi zinazotoa huduma mahususi kama afya.

Hiyo ni kutokana na kile alichokibainisha kuwa licha ya kulipishwa kodi huduma zinazotolewa zinahitaji kufanyiwa maboresho kila siku.

Hayo ameyasema leo katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Bugando iliyoanzishwa mwaka 1971.

Nkwande amesema baadhi ya tozo zinaweza zisifanikishe malengo ya kutoa huduma stahiki kwa wananchi wahitaji katika Taifa.

“Unakusanya pesa lakini bado unatozwa kodi wakati mahitaji ya kufanya maboresho katika hosptali bado ni mkubwa,”

“Nikuombe Rais kwa nafasi yako na Serikali unayoiongoza uzitazame changamoto nilizozitaja hapo juu,” amesema Nkwande.

Katika hatua nyingine amesema hospitali hiyo ina upungufu wa watumishi wapatao 1300 huku akibainisha kuwa uwekezaji katika vifaa tiba na miundombinu unapofanyika na mahitaji ya rasilimali watu unakuwa mkubwa.

Pia kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wanaofika kupata huduma katika hospitali hiyo jambo linalofanya kuwepo ulazima wa kuongeza miundombinu ya kutolea huduma.

“Pia kama hospitali ina uhitaji wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambapo katika mipango yetu ujenzi wake unatarajiwa kuanza huku ukigharimu Sh5 bilioni,”amesema.

Alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa kuwapatia Sh1 bilioni kwa ajili ya kukamilisha wodi ya saratani, a wadau na watumishi wa hospitali ambao kwa pamoja walichangia Sh650 milioni kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya saratani.

Kama hospitali pia hospitali ilitoa Sh1 bilioni kutoka mapato ya ndani katika ujenzi huo.

“Hata hivyo Rais (Samia Suluhu Hassan) ili kukamilisha ujenzi huu hospitali bado inapungukiwa Sh2.4 bilioni,”

Kuhusu miradi amesema, kupitia mapato ya ndani hospitali imeanzisha miradi miwili ikiwemo ule wa taasisi ya moyo inayotarajia kugharimu Sh10.5 bilioni huku hospitali ikitenga Sh5 bilioni na Sh5 bilioni zilizobakia walimuomba Rais kuwafikiria.

Ili kukabiliana na changamoto za kina mama pia wako mbioni kujenga jingo la mama na mtoto ambalo litagharimu Sh6.5 bilioni.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live