Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bugando kufanya upasuaji wagonjwa wenye uzito uliokithiri

Bugando Pic Data Bugando kufanya upasuaji wagonjwa wenye uzito uliokithiri

Mon, 5 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hospitali ya Rufaa Kanda ya Bugando inatarajia kuanza kutoa huduma ya upasuaji wa matundu kwa ajili ya kupunguza uzito kwa watu wenye uzito uliokithiri.

Huduma hiyo inayotarajiwa kuanza kutolewa mwishoni mwa mwaka huu ni mwendelezo wa huduma ya upasuaji wa matundu kwa magonjwa mengine yanayohitaji upasuaji iliyoanza kutolewa rasmi hospitalini hapo mwezi Juni mwaka huu.

Akizungumza jana Septemba 4, 2022 katika maonesho ya biashara ya mkoa wa Mara yanayoendelea mjini hapa, Daktari bingwa wa upasuaji wa matundu kutoka hospitali hiyo, George Kanani amesema kuwa upasuaji huo wa matundu kwaajili ya kupunguza uzito utakuwa ni wa kwanza kutolewa nchini.

Amesema kuwa tatizo la uzito uliokithiri ni janga la dunia hivyo wao kama wadau wa afya wameona kuwa ipo haja ya kuwa sehemu ya mpambano dhidi ya tatizo hilo ambalo kwa namma moja ama nyingine limekuwa likichangia ongezeko la magonjwa yasiyokuwa ya kuambukizwa.

"Tatizo la uzito uliozidi ni kubwa sana hivyo zinahitajika jitihada za makusudi katika kukabiliana nalo hivyo tunaamini huu upasuaji utakuwa ni njia mojawapo tena yenye ufanisi katika kukabiliana nalo" amesema

Amesema kuwa upasuaji huo wa matundu kwa watu wenye uzito uliokithiri itakuwa ni sehemeu ya njia za kukabiliana na tatizo  hilo baada ya baadhi ya watu wenye uzito kushindwa kutumia kwa usahihi njia zinazotumika kwa sasa kama vile mazoezi na mpangilio wa lishe.

Dk. Kanani pia amewataka wakazi wa Musoma na mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kupata huduma zinazotolewa katika banda lao ikiwemo huduma za matibabu ya macho ambayo yanatolewa bure kwa muda wa siku 10 za maonesho.

Pia amewataka wakazi wa kanda ya ziwa kufika katika hospital hiyo ya rufaa kwaajili ya matibabu hasa upasuaji wa matundu  kwa magonjwa mengine yanayohitaji upasuaji huku akisema kuwa aina hiyo ya upasuaji ni wa kisasa na una faida nyingi   ikiwepo mgonjwa kupona haraka tofauti na upasuaji wa kawaida.

Baadhi ya wakazi wa Musoma wameipongeza hospitali hiyo kwa ubunifu huo ambao wamesema utasaidia kuondoa tatizo la unene ambalo wamedai libaongezeka kw akasi.

"Sio siri sasa hivi watu wengi wanasumbuliwa na tatizo la uzito mkubwa yaani vitambi vya ajabu ajabu vimekuwa vingi sana na hii inatokana na aina ya maisha tunayoishi na vyakula tunavyokula kwahiyo tiba hii ikija itakuwa ni mkombozi wa wengi" amesema Johari Magira mkazi wa Musoma

Mkazi mwingine Anna Masunga amesema kuwa kutokana na wimbi la tatizo la uzito ipo haja kwa mamlaka husika kuingilia kati hasa katika suala zima la tiba kwani tatizo hilo linaweza kutumika kusababsiha matatizo mengine makubwa kiafya kutokana na wimbi la watu wanaojitangaza kutibu uzito uliopitliza ilhali sio kweli.

"Kuna haja ya kuwaelimisha wananchi ili waweza kupata tiba sahihi kutoka katika taasisi  sahihi kama ambavyo Bugando wanataka kufanya, tumeshuhudia matangazo mengi hasa kwenye mitandao ya kijamii  watu wanasema wana uwezo wa kumaliza vitambi kwa dawa ambazo sina uhakika kama zimethibitishwa na mamlaka husika" amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live