Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

‘Boresha Lishe’ kukabili utapiamlo Singida, Ikungi

195ae446884342b4463e7d005af3b69c ‘Boresha Lishe’ kukabili utapiamlo Singida, Ikungi

Fri, 11 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MRADI wa Boresha Lishe unaotarajiwa kutekelezwa katika vijiji 85 katika wilaya za Ikungi na Singida, utasaidia kukabiliana na tatizo la utapiamlo kwa watoto chini ya miaka mitano; Imefahamika.

Meneja Mkuu wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Mpango Endelevu wa Uboreshaji Mazingira (SEMA) la mjini Singida linalotekeleza mradi huo chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Ivo Manyaku, alisema wamejikita zaidi katika kutoa mafunzo ya kilimo bora cha uzalishaji mboga, matunda na ufugaji wa wanyama wadogo ili kuboresha lishe katika ngazi ya familia.

"Kumekuwa na tatizo la utapiamlo katika mkoa wetu na moja ya sababu ni kwamba, wanaume ambao ndiyo watoa maamuzi ya fedha kwenye familia, hawaendi kliniki na wenzi wao wanapokuwa wajawazito ili kupewa elimu ya lishe bora kwa mama na mtoto," alisema Manyaku.

Kwa mujibu wa Manyaku, kutokana na changamoto hiyo, mradi huo unaotekelezwa kwa kushirikiana na RECODA, umekuwa mkombozi kwa kuwa unawafikia wanafamilia wote katika maeneo ya vijijini na kuwapa elimu ya lishe bora, namna ya kuanzisha bustani za mboga, matunda na kufuga wanyama wadogo.

Alisema utaratibu huo umerahisisha kuwafikia akina baba vijijini, badala ya kuwasubiri waambatane na wenzi wao siku ya kiliniki na umesaidia pia kuleta ufanisi katika kupunguza udumavu, utapiamlo na uzito pungufu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupitia mkoba wa siku 1000.

Alisema hadi sasa bustani za nyumbani 9,590 zimeanzishwa wilayani Singida na nyingine 7,704 wilayani Ikungi zilizolimwa mboga na matunda baada ya wananchi kupatiwa elimu na mbegu za ‘beetroot’, viazi damu, ‘chinese- spinach’, mnavu na miti ya mipapai, miembe na mipasheni.

Ofisa Lishe Mkoa wa Singida, Teda Sinde, alishukuru kwa kuanzishwa kwa mradi huo huku akiomba usambazwe katika vijiji vyote kwa kuwa vyakula hivyo ni muhimu na iwapo wananchi watazingatia matumizi yake hasa kwa wajawazito na watoto, tatizo la utapiamlo, udumavu na uzito pungufu kwa watoto litakwisha.

Takwimu za utafiti wa kitaifa za mwaka 2018 juu ya hali ya lishe mkoani Singida zinaonesha asilimia 29.8 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana udumavu, asilimia 5 ukondefu na asilimia 15 wana uzito mdogo, huku asilimia 27.9 tu ya watoto hao ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya.

Aidhja takwimu zinabainisha kuwa, asilimia 3 ya watoto walio chini ya miaka miwili, ndio hupata mlo unaokubalika katika tafsiri ya lishe bora.

Chanzo: habarileo.co.tz