Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bilioni 1/- yatengwa ujenzi jengo la saratani Bugando

Ceea25ca9350e6b93c5850408e358aeb Bilioni 1/- yatengwa ujenzi jengo la saratani Bugando

Mon, 8 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imetenga kiasi cha Sh bilioni moja katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi ya saratani, linalojengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Hayo yameelezwa jana jijini hapa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Doroth Gwajima alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara na wakazi wa jiji la Mwanza kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la saratani, linalojengwa katika Hospitali ya Bugando.

Alisema fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa miundombinu ya jengo hilo, ili litakapokamilika ili liongeze kupanua huduma za kibingwa za tiba ya saratani kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na mikoa jirani.

Katika harambee hiyo jumla ya Sh bilioni 1.34 zilichangwa, ambapo fedha taslimu zilikuwa Sh 46,750,000, ahadi Sh 1,219,216,000, mabati 20 na mifuko ya saruji 3325 vyote vikiwa na thamani ya Sh 73,150,000.

Kuhusu uboreshaji wa tiba za kibingwa kwa upande wa saratani, Dk Gwajima alisema mwelekeo wa serikali kwa sasa ni kuona huduma za tiba za kibingwa za saratani zinawafikia wananchi wote, huku akiwataka watu wajenge utamaduni wa kupima afya zao.

"Ugonjwa huu ukigundulika mapema unatibika," alisema.

Alisema serikali pia inajivunia ushirikiano mzuri uliopo baina yake na Hospitali ya Bugando, ambao umedumu kwa muda wa miaka 50.

Alimshukuru Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Bugando, Askofu Renatus Nkwande kwa kuiongoza vizuri hospitali hiyo.

Dk Gwajima ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika harambee hiyo, aliushukuru uongozi wa hospitali kwa kuchangia kiasi cha Sh bilioni moja, watumishi Sh milioni 250 na serikali Sh bilioni 1.7 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo la saratani.

"Tunachohitaji kwa sasa ili kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ni Sh bilioni 4.1 baada ya michango hii yote kutolewa," alisema.

Waziri Gwajima aliwataka watanzania na waafrika kuunganisha nguvu zao za pamoja ili waweze kuchangia kwenye sekta ya afya kwenye nchi zao.

"Kama wazungu wanaungana pamoja na kutengeneza Mfuko wa Pamoja kutusaidia waafrika kwenye sekta ya afya, inakuwaje sisi tunashindwa," alihoji.

Aliwapongeza wafanyabiashara na wakazi wa jiji la Mwanza, kwa kuonesha moyo wa uzalendo na upendo na kujitokeza kuchangia ujenzi wa jengo hilo la saratani, ambalo likikamilika litakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 120 kwa siku.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Bugando, Dk Fabian Massaga alisema Hospitali ya Bugando ni Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa, ambayo ina watu zaidi ya milioni 17 kwa mikoa yote minane ya kanda hiyo na baadhi ya mikoa jirani. Hospitali hiyo inahudumia wastani wa wagonjwa 1,000 kwa siku sawa na wagonjwa 365,000 kwa mwaka.

Alisema ugonjwa wa saratani ni janga linalosababisha maumivu na mateso makubwa na vifo kwa watanzania, hivyo kuchangia huduma zake ni muhimu.

"Neno saratani ni neno jepesi na tamu kulitamka, lakini limebeba maumivu makali na mateso makubwa sana kwa waathirika," alisema .

Alisema saratani ni miongoni mwa magonjwa yanayongoza duniani kwa kusababisha vifo, ambapo katika kila watu 100,000 kuna wagonjwa wapya 76 wa saratani. Vifo vinavyosababisha saratani hufikia 68 kwa kwa kila wagonjwa 100. Hali hii ya vifo inasababishwa na wagonjwa wengi kufika hospitalini wakiwa wamechelewa.

Alisema idadi ya wagonjwa wa saratani imeongezeka katika hospitali hiyo kutoka wagonjwa 320 mwaka 2009 hadi kufikia wagonjwa 14,900 mwaka 2020. Katika kipindi hicho cha miaka 11 jumla ya wagonjwa 73,000 wamepata huduma za matibabu ya saratani katika hospitali hiyo ya Bugando.

Akitoa ushuhuda kwa niaba ya wagonjwa waliopata tiba ya saratani na kupona, Levina Ngahyoma ambaye ni mkazi wa Biharamulo mkoani Kagera, aliiomba serikali iangalie uwezekano wa kupunguza gharama za tiba ya saratani.

"Wagonjwa wengine hawaji kutibiwa baada ya kukosa fedha na ni wengi wanakufa," alisema Ngahyoma na kuupongeza uongozi wa Bugando wa Kitengo cha Saratani kwa kumtibu na kupona saratani ya titi iliyokuwa inamkabili.

Chanzo: habarileo.co.tz