Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bil 33.5/- zatengwa kununua vifaa tiba hospitali 67

93a7a7fd0b097233f120a0cfc19ef53a Bil 33.5/- zatengwa kununua vifaa tiba hospitali 67

Sat, 13 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI katika mwaka wa fedha 2020/2021 imetenga Sh bilioni 33.5 kwa ajili ya kununua vifaa tiba vya hospitali 67 za halmashauri zilizojengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri Tamisemi, Dk Festo Dugange wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kiteto, Edward Lekaita (CCM) aliyetaka kujua ni lini serikali itapeleka vifaa tiba katika hospitali ya Kiteto baada ya hospitali hiyo kukamilika.

Dk Dugange alisema lengo la serikali ni kuboresha hospitali kwa kusambaza vifaa tiba mbalimbali katika hospitali hizo ili kuboresha huduma za tiba kwa wananchi ikiwemo hiyo ya Kiteto.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani (Chadema) aliyetaka kujua ni lini serikali itapeleka watumishi na vifaa tiba katika hospitali ya Nkasi.

Dk Dugange alisema ni azma ya serikali kuboresha huduma za afya katika hospitali zake mbalimbali, kadiri fedha zinavyopatikana itaendelea kupeleka vifaa na kuboresha miundombinu ya hospitali hizo nchini.

Akijibu swali la Mbunge wa Busega, Simon Lusengekile (CCM) aliyetaka kujua ni lini Serikali itapeleka vifaa katika Hospitali ya Wilaya ya Busega ili huduma bora za afya ziendelee kutolewa.

Alisema hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Busega ni miongoni mwa hospitali 67 za halmashauri zilizoanza kujengwa mwaka 2018/19 kwa kupewa fedha kiasi cha Sh bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba ambayo ni jengo la utawala, jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la maabara, jengo la mionzi, jengo la wazazi, jengo la kufulia na jengo la kuhifadhia dawa.

Katika mwaka wa fedha 2020/21, Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega ilitengewa Sh milioni 500 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi na katika mwaka huo huo, vilevile katika mwaka huo wa fedha, hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Busega ilitengewa Sh milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kama hospitali nyingine 67 nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz