Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bangi, mirungi; wauaji wanaoangamiza jamii

0c2df5b5acd62e4b2615abd84b0d2741.png Bangi, mirungi; wauaji wanaoangamiza jamii

Mon, 20 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JULAI 6, 2020 Rais John Magufuli alimthibitisha aliyekuwa Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, James Kaji katika wadhifa huo.

Akizumgumza katika sherehe za kuapisha wakurugenzi mbalimbali katika Ikulu ya Chamwino, Rais Magufuli alielezea utendaji bora wa kazi unaofanywa na Mamlaka hiyo chini ya Kaji huku akijata matukio kadhaa ya ukamataji wa dawa za kulevya likiwemo la hivi karibuni la ukamataji bangi wilayani Arumeru.

Aidha, hivi karibuni karibuni iliripotiwa katika kituo kimoja cha televisheni kuwa, polisi mkoani Arusha wamekamata magunia 15 ya bangi yakisafirishwa kwenda nchi jirani kwa kutumia gari aina ya Noah.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, ACP Salumu Hamduni alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo. Kimsingi kama zilivyo aina nyingine za dawa za kulevya, uzalishaji, umiliki, utunzaji, uuzaji na utumiaji wa bangi na mirungi ni janga ambalo licha ya madhara yake kuwa makubwa, bado baadhi ya watu wamenga’ng’ania.

Makala haya, yanajikita katika athari za bangi na mirungi. BANGI Nchini Tanzania bangi hupatikana kwa wingi zaidi katika mikoa ya Mara, Iringa, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, Tabora, Tanga, Kagera, Mbeya na Morogoro.

Kwa mujibu wa uchunguzi, kwa kuwa kulima (kuzalisha), kuhifadhi, kuuza, kusafirisha, kutumia au kuhamasisha matumizi au kujihusisha kwa namna yoyote na bangi ni kosa la jinai ambalo adhabu yake inaweza kufikia hata kifungo cha maisha, ili kukwepa mkono wa sheria zao hili haramu na hatari limepewa majina mengi ya bandia kama njia ya watu kujaribu kujificha na kulaghai isijulikane.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Tanzaniia, mitaani bangi iimepewa majina mbalimbali kutegemea makundi mbalimbali na jamii ya watumiaji na miongoni mwa majina hayo ni ganja, jani, ndumu, stiki, daga, msokoto na kijiti. Kutokana na baadhi ya jamii kudaiwa kuitumia zaidi, baadhi ya vijana katika makundi yao sehemu mbalimbali huiita ‘mboga za majani.

Stafu Sajenti Ched Ngatunga wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya (ADU), anasema utumiaji wa bangi una madhara mengi kwa mtu na kwa jamii kwani kwa wanawake kwa mfano, huathiri mfumo wa uzazi ikiwa ni pamoja na kumfanya mtumiaji kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo na kusababisha mabadiliko ya hedhi.

HabariLEO lilipotaka ufafanuzi wa kihabari kwenye Banda la Polisi katika Maonesho ya Biashara ya 14 ya Kimataifa (Sabasaba) yaliyomalizika hivi karibuni katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, Ngatunga kwa ruhusa ya Msemaji wa Polisi, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), David Misime, alisema matumizi ya bangi husababisha mimba kuharibika na kuzaa watoto njiti na hivyo, kuwa hasara ya kijamii.

Jeshi la Polisi Tanzania katika kipeperushi chake kiitwacho: “Athari za Bangi” linasema madhara mengine ya bangi ni pamoja na mtumiaji kuchanganyikiwa, na kuwa na tabia ya ukatili, ukorofi na uhalifu na pia, mtumiaji kujidanganya bila kujua kwa kuona, kusikia na kuhisi vitu visivyokuwapo.

Polisi katika kipeperushi hicho chenye kaulimbiu: ‘Tujenge Jamii, Maisha, na Utu Wetu Bila Dawa za Kulevya’ kilichoandaliwa na Kitengo cha Kupambana na Kupamba na Dawa za Kulevya (ADU) cha Ofisi ya DCI wanasema: “Moshi wa bangi unapoingia kwenye mapafu, hutengeneza kitu kama lami ambayo huganda na kuathiri utendaji kazi wa mapafu.”

Wanaongeza: “Humfanya mtumiaji kuridhika na hali duni aliyo nayo hivyo, kukosa mwamko wa maendeleo huku akijihisi na kujidanganya kuwa ni mtu mwenye mafanikio makubwa.”

Vyanzo mbalimbali vya habari vinavyohusu madhara ya utumiaji wa dawa za kulevya vinayataja madhara mengine ya dawa hizi za kulevya (bangi) kuwa ni pamoja na kuharibika kwa mimba kwa wanawake watumiaji na kuzaa watoto njiti; mtumiaji kupoteza kumbukumbu, kupunguza kinga ya mwili, kuumwa koo, kupata kikohozi na hatari kubwa ya kupata saratani ya mapafu.

MIRUNGI Mintarafu mirungi, nchini hapa hustawi na hupatikana kwa wingi zaidi wilayani Same katikia Mkoa wa Kilimanjaro, Lushoto mkoani Tanga na katika Mlima Meru mkoani Arusha.

Kama ilivyo bangi, mirungi nayo inayo majina mbalimbali mitaani ikiwa ni pamoja na miraa, giza, kangeta, veve, Mbaga na gomba. Jeshi la Polisi katika kipeperushi chake kuhusu mirungi linasema: “Kiasi kingi cha mirungi nchini huingizwa isivyo halali… Hutumika zaidi kwenye mikusanyiko ambayo hujumuisha zaidi wanaume ingawa katika miaka ya karibuni baadhi ya wanawake wamejiingiza katika matumizi yake.”

Mirungi nayo kama bangi, ina madhara ya kijamii, kiafya na kiuchumi kwa watumiaji na katika jamii ikiwamo kuongeza kasi ya mapigo ya moyo kwa mtumiaji na hivyo, kuongeza hatari ya mtumiaji kuongeza shinikizo la damu, kupata kiharusi na hata kusababisha kifo.

Chapisho kutoka ndani ya polisi linasema utumiaji wa mirungi hupunguza msukumo wa kufanya tendo la ndoa, kumaliza haraka na kutoweza kudumu kwenye tendo hilo kwa muda mrefu pia, hupunguza ubora wa mbegu za kiume na kuvuruga mfumo wa utokaji wake na hatimaye, kusababisha ugumba. Linasema: “Matumizi ya mirungi yanaweza kusababisha kuzaliwa kwa watoto wenye uzito mdogo ambao huweza kukataa kunyonya kutokana na ladha ya maziwa kubadilishwa na viuatilifu vinavyotumika kwenye kilimo cha mirungi.”

Katika maonesho hayo ya Sabasaba mwaka huu, Stafu Sajenti Ngatunga anasema akielezea wananchi waliotembelea banda la polisi kuwa, wanawake wanaotumia mirungi katika kipindi cha ujauzito wapo hatarini zaidi kupata maumivu ya kifua na kuongezeka kwa mapigo ya moyo.

Vyanzo mbalimbali vinaelezea madhara ya mirungi kiuchumi kuwa ni pamoja na kumsukuma mtumiaji kutumia fedha ambazo zingekidhi mahitaji ya familia kununulia mirungi hiyo na hivyo, kusababisha migogoro na pia, utafunaji wa mirungi hutumia muda mwingi wa kazi au muda ambao mtumiaji hutakiwa kujumuika na familia yake hivyo, kushusha uzalishaji na ukaribu na familia.

Katika mazungumzo ya pamoja na wanawake wawili waliowahi kutumia mirungi wanaokataa majina yao kutajwa gazetini, wakazi wa Kijiji cha Magena wilayani Tarime, wanasema mtumiaji anapokosa aina hii ya dawa za kulevya, hupatwa na uchovu, sonona, kuvamiwa na hasira za ghafla, kutetemeka, kushindwa kutulia na kukumbwa njozi za kutisha yaani majinamizi.

Aliyekuwa Mkuurugenzi wa shirika la Undugu Association Tanzania ndani ya Kanisa Katoliki nchini likiwa na makao yake katika Parokia ya Manzese, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Baptiste Mapunda wa Shirika la Wamisonari wa Afrika (White Fathers), katika moja ya mada zake dhidi ya ulevi, aliwahin kusema: “Watumiaji wa mirungi wanapokosa usingizi hujikuta wakizama katika tope la kupenda kuvuta sigara au kunywa pombe... hali hii inazidi kuwaumiza kiafya.”

Mintarafu suala hili, Jeshi la Polisi, Ofisi ya DCI kupitia kwa Stafu Sajenti Ngatunga linasema katika Maonesho ya Sabasaba: “… Mtumiaji hukosa usingizi na ulevi ukiisha, mwili husababisha usingizi mzito unaoweza kusababisha ajali hasa kwa madereva.”

Polisi katika chapisho lao wanayataja madhara mengine ya matumizi ya mirungi kuwa ni pamoja na kuchochea ukatili, fujo, ugomvi na kuona na kusema masuala ya kusadikika na kuhangaika.

“Mtumiaji hukosa kabisa hamu ya kula na hivyo, kupungua uzito na kusababisha upungufu wa maji mwilini na kuleta tatizo la kukosa choo na ugonjwa wa bawasiri.”

Ikumbukwe kuwa, kama ilivyo bangi, nchini Tanzania mirungi ni haramu na kuzalisha, kumiliki, kuhifadhi, kuuza au kutumia na kusafirisha ni kosa la jinai. Baadhi ya nchi za Ulaya ambazo awali ziliruhusu matumizi ya mirungi zimeanza kuharamisha dawa hizo baada ya kuona madhara yake kwa watu wake.

MAMBO MUHIMU KUJUA

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, utumiaji wa dawa za kulevya ikiwamo mirungi na bangi hauongezi ufanisi kazini, ufaulu katika mazomo, udereva wala nguvu za kiume kama inavyozushwa na watetezi wa dawa za kulevya hivyo, ni vyema wazazi na walezi wawasaidie zaidi vijana kujifunza na kuzingatia stadi za maisha na kujiepusha na makundi hatarishi yanayoweza kukufanya/ kumfanya mtu aingie katika utumiaji.

“Kwa waliokwisha kosea na kuingia, mtumiai anaweza kupunguza kiasi anachotumia taratibu na hatimaye kuacha kabisa. Aidha, asasi za kiraia huwasaidia watumiaji kuacha kwa kuwapa unasihi hata katika nyumba za upataji nafuu maarufu, ‘soba house’ wanakopitishwa katika hatua 12 za upataji nafuu.”

Chanzo: habarileo.co.tz