Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Baada ya figo, Muhimbili yajipanga kupandikiza ini

9526 FIGO+PIC TZWeb

Tue, 19 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salam. Baada ya kufanikiwa katika matibabu ya upandikizaji figo na vifaa vya usikivu, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) iko mbioni kutoa huduma za upandikizaji wa ini kupitia Kitengo cha Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini.

Mkurugenzi wa MNH, Profesa Lawrence Maseru alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Wiki ya utumishi wa Umma kwa kuonyesha huduma za afya zinazotolewa na hospitali hiyo.

Alisema tayari madaktari bingwa kutoka hospitali ya BLK ya India wamewasili nchini kutoa mafunzo ya uchunguzi na tiba kwa madaktari wa MNH ili waweze kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya vivimbe vya ini na kongosho.

“Hii ni miongoni mwa hatua za muhimu katika kufanikisha malengo makuu ya upasuaji mkubwa wa ini na upandikizaji wake.

“Tunazingatia kwamba huduma tunazoanzisha na kuzitoa ni salama na za uhakika kama zinavyotolewa nje na ndiyo sababu tunataka wataalam wetu wajifunze kwa nadharia na vitendo,” alisema.

Akizungumzia hilo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliitaka MNH kuweka mipango itakayowawezesha kuzifikisha huduma hizo za kibingwa kwa wananchi wa kawaida.

Alisema Serikali iko tayari kugharamia baadhi ya dawa na vifaa tiba kwenye huduma za matibabu ya kibingwa ili kuwezesha wananchi wengi kutibiwa.

Alisema lengo ni kuhakikisha wananchi wanasogezewa huduma bora karibu na ndiyo sababu imeamua kuboresha hospitali za rufaa za mikoa ili kupunguza msongamano wa wagonjwa MNH.

“Kwa kuanzia tunafanya maboresho kwa kuweka kitengo cha magonjwa ya dharura, kitengo cha uangalizi maalumu (ICU) na kitengo cha huduma za na mtoto,” alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz