Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Athari za kutoa mimba kwa mitishamba

Mitishamba Mimba Athari za kutoa mimba kwa mitishamba

Tue, 7 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati maeneo ya mjini baadhi ya wasichana hutumia vidonge vya P2 kuzuia mimba, vijijini hali ni tofauti.

Wasichana na wavulana wanaojihusisha na mapenzi katika umri mdogo hutumia nyenzo hatarishi kutoa mimba.

Rehema (si jina halisi) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Sekondari ya Itamboleo wilayani Mbarali mkoani Mbeya, aliponea chupuchupu baada ya kutoa mimba kwa kutumia majani ya mpera.

Baada ya kunywa maji ya majani ya mpera yaliyotwangwa, alianza kuumwa tumbo huku akivuja damu nyingi kabla hajapelekwa kupata huduma za kitabibu.

“Nililetewa na rafiki yangu akishirikiana na mwanaume aliyenipa mimba wakaniambia ninywe, baada ya kunywa tumbo liliuma sana ile mimba ikatoka. Kabla ya hapo tayari wanafunzi wenzangu walishatoa taarifa kwa walimu kuhusu vipimo vya ujauzito wangu,” alisema.

Rehema (15) ni miongoni mwa wasichana waliofikwa na mkasa huo baada ya kushawishika katika makundi na kujikuta ameingia kwenye mapenzi katika umri mdogo.

Advertisement “Nilishawishiwa na rafiki yangu. Alinikutanisha na kijana ambaye alikuwa akinipa fedha Sh2,000 hadi Sh10,000 na alininunulia nguo, mafuta na baadaye aliponiambia ananipenda sikuona haja ya kukataa nikamkubali” alisema Rehema.

Mkuu wa Sekondari ya Itamboleo anakosoma msichana huyo, Faraja Madembwe alisema waliwabaini wanafunzi wawili wametoa mimba baada ya taarifa walizopokea kutoka kwa wanafunzi wenzao baada ya elimu waliyoipata kupitia klabu ya shule salama.

“Tulivyopokea ile taarifa na kuletewa majibu ya vipimo, huyu mwanafunzi alikuwa nyumbani. Tulipomfuatilia wakasema hakuja shule anaumwa tumbo. Tuliongea naye kirafiki na akatuambia kila kitu, kuhusu vipimo walivipata wapi na taarifa zote kuhusu huyo kijana ambaye hata hivyo hayupo hapa kijijini kwa sasa.

“Lakini kwa kuwa mimba alishaitoa tulimsimamisha shule kwa siku 29 na baadaye alirejea masomoni baada ya wazazi na walimu kumkanya na kumuelimisha kuhusu afya ya uzazi,” alisema Mwalimu Madembwe.

Mbarali ni miongoni mwa wilaya zinazotajwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaotoa mimba kwa njia za hatari.

Mkazi wa Kijiji cha Utengule, Monica Tenga alisema yamekuwapo matukio kadhaa za wasichana kufariki kutokana na kutoa mimba kwa kutumia vijiti vya miti ya mihogo.

“Kuna msichana alikuwa akisoma Sekondari yeye alilazwa kwa muda mrefu kidogo baada ya kupata madhara wakati anatoa mimba na walisema kizazi kilioza. Lakini mwingine alikuwa ameolewa akaachwa na mumewe, yupo nyumbani akapata mimba nyingine akaamua kuitoa kwa njia za vijiti hivyohivyo alifariki,” alisema Monica.

Hata hivyo matukio hayo yanapungua kwa sasa kutokana na elimu wanayopewa wanafunzi kupitia mradi wa shule salama unaotekelezwa katika wilaya sita za mikoa ya Mbeya, Njombe na Kilimanjaro.

Mwalimu mlezi wa Sekondari ya Itamboleo, Benedicto Kabinanjila alisema wanao wanachama 38 wakiwamo wasichana 18 na wavulana 20.

“Baada ya kupata mafunzo tulianza kwa kutambulisha mradi kwa wanafunzi na tulianza kutoa mafunzo kwao nini haki zao kama watoto, wajibu wao shuleni, kwa wazazi na namna ya kujitambua.

“Zaidi tunawajenga namna ya kuibua changamoto, kukabili ukatili wa kingono, kisaikolojia na mafunzo haya tunayafanya mara moja kwa wiki,” alisema.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Rima iliyopo Kijiji cha Mrere wilayani Rombo, Mary Mrosso alisema uwepo wa klabu ya shule salama umewawezesha walimu kuwa karibu na wanafunzi wanaoleta taarifa za ukatili.

Mratibu wa Mradi wa Shule Salama kutoka taasisi ya Wildaf, Queen Assey alisema “ulianzishwa kwa ajili ya kuzuia ukatili shuleni hata majumbani kwa kuwafundisha watoto kujua haki zao na za wengine ili waweze kuzitetea na kuwatetea wenzao pindi wanapoonewa.”

Mila potofu

Licha ya jitihada za wadau kumnusuru maisha ya mtoto wa kike na mimba za utotoni, maeneo ya vijijini bado wazazi huzimaliza kesi za mimba na ubakaji nje ya mahakama jambo linalokwamisha jitihada hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Right for Social Change Organization kupitia Kituo cha Msaada wa Kisheria Mbarali, Edson Mwakyembe alisema matukio ya wanafunzi kubakwa na kupewa mimba ni mengi katika wilaya hiyo.

“Tunajitahidi kuhakikisha kesi zinaenda, lakini wanawafundisha watoto nyumbani waseme uongo hivyo ushahidi unakosekana na wao wanaamini mtoto wa kike hana thamani kuliko wa kiume. Wengi hawafuati taratibu za kisheria,” alisema Mwakyembe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live