Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Athari za kukanda wazazi kwa maji ya moto

Kukandapic Athari za kukanda wazazi kwa maji ya moto

Thu, 11 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Wakati wanawake walio wengi wanaamini kukandwa maji ya moto baada ya kujifungua ni tiba, wataalamu wa afya ya uzazi wanaonya kuwa kufanya hivyo kuna madhara zaidi ikilinganishwa na faida ambazo zimekuwa zikiainishwa.

Miongoni mwa madhara yanayotajwa ni pamoja na kumsababishia mama maumivu makali, kuharibu maumbile yake, kulegeza misuli, majeraha yanayosababishwa na maji ya moto, kuzuia uponyaji wa haraka, kusababisha maambukizi na tatizo la kisaikolojia kwa hofu ya kukandwa.

Pamoja na madhara hayo, jamii inaamini kwamba maji ya moto ni tiba ya kurejesha maumbile ya asili kwa aliyejifungua. Kati ya wanawake waliozungumza na gazeti hili, wote wanasema maji ya moto ni tiba, japo hawana ushahidi wa kitaalamu.

Mkunga wa jadi kutoka kijiji cha Minyaa kilichopo Kata ya Kinyeto, Halmashauri ya Singida, Onolata Kisaka (67) alisema kukanda maji moto ni kitu muhimu kwa mama aliyejifungua ili kuondoa uchafu uliosalia tumboni baada ya mtoto kutoka.

“Miaka mingi mama lazima akandwe na ndiyo uhai. Asipokandwa wengi walifariki kutokana na uchafu tumboni. Haya mambo ya kutokandwa yanakuja sasa hivi wakati kuna hospitali kila mahali,” alisema Onolata.

Lulu Khatibu alisema walizoea kuona wanawake wakifanyiwa hiyo mila inayoendelezwa na wanafamilia baada ya kujifungua. “Hata nilipokuwa msichana baada ya kujifungua nilikandwa na nilikuwa naona afadhali nikifanyiwa hivyo, hii ni desturi yetu sisi wanawake hasa wa Afrika.”

Hata hivyo, wapo waliopata madhara baada ya kukandwa maji moto, akiwamo Arafa Juma (26) ambaye alivuja damu nyingi na baadaye kuvimba mwili baada ya kukandwa kwa maji moto.

“Nilijifungua vizuri, baada ya siku moja nikarudi nyumbani. Nilipofika kitu cha kwanza ilikuwa kwenda bafuni kukandwa. Ghafla nilianza kutokwa damu nyingi, mabonge mabonge na bibi yangu alisema ni uchafu unatoka, lakini baada ya muda mwili ukaanza kuvimba.

“Nilirudishwa hospitali walisema ni madhara ya kukandwa maji moto, nilichomwa sindano damu ikakata na baada ya matibabu mwili ulirudi sawa,” alisema Arafa, mama wa mtoto mmoja.

Madhara ya kukandwa

Wakunga na madaktari bingwa wa kinamama na magonjwa ya uzazi waliozungumza na gazeti hili wamesema hakuna uchafu unaotakiwa kutolewa na maji ya moto kwa kukandwa na kuminywa na kwamba uke haurudi kwa kukandwa bali huharibika zaidi.

“Mara zote jamii hudhani damu zinazotoka mara baada ya kumkanda mama ni uchafu uliobaki baada ya kujifungua. Ni makosa makubwa, kwani maji moto hufungua mishipa ya damu iliyojifunga mara baada ya mtoto kutoka na pale damu huanza kuvuja upya,” alisema mkunga mtaalamu, Agnes Ndunguru.

Alisema hatua za kujifungua ni za asili na hivyo hata baada ya kujifungua kila hatua huwa ni asili, hivyo hakuna sababu ya kutumia nguvu kubwa kuurudisha mwili wa mama.

“Taarifa hupelekwa katika ubongo kwamba mtoto ameshatoka, yanahitajika maziwa kwa ajili ya mtoto na sehemu ya mji wa mimba inatakiwa kurudi na kushuka kwenye pango la nyonga kuwa ya kawaida kama mtu ambaye hana mimba,” alisema.

Agnes ambaye miaka saba ya kazi yake ameshazalisha wanawake 6,000, alisema vitu hivyo vyote vinatokea kiasili na kwamba hakuna haja ya kukanda kwa maji moto eti kutoa uchafu.

“Mjamzito akishajifungua kondo la nyuma au placenta inapotolewa tunahakikisha tunaondoa mabaki yote, hivyo hakuna uchafu anaobaki nao mama kwa sababu ukibaki husababisha kutokwa na damu nyingi sana,” alisema.

Alisema ingawaje kuna utafiti ambao unaendelea kufanyika, kina mama wengi wamekuwa wakirudi hospitalini baada ya kupata athari ya kukandwa maji moto na wengine hupoteza maisha.

Alisema wamekuwa wakiwabaini kinamama wengi baada ya kufika hospitalini kwa ajili ya kupimwa ujauzito wa pili.

“Wapo wanaokuja maziwa hayatoki, wamepata malengelenge ukeni, ukiwachunguza tayari wametanuka misuli ya uke kwa kuwa wengine anawekewa kwenye kigoda anakalia maji, hawa tunawabaini.

“Ukimuuliza anakiri alikandwa, kwani kuna utofauti kwa ambaye hakukandwa maji moto ambaye uke wake unakuwa wa kawaida, ile mikunjo mikunjo kwenye kuta za uke inakuwepo, tofauti na aliyekandwa,” alisema.

Mbali na hayo, alisema wapo kinamama ambao hubainika kupata athari za kufumuka kwa mishono na hao huwa na uwazi kwenye uke kwa chini, “kama mama aliongezwa njia, akikandwa zile nyuzi hulainika na kuachia, hivyo kidonda hakitafunga na wengine huwa hashtuki unakuja kubaini anapojifungua mtoto mwingine.”

Katibu wa Chama cha Wakunga Tanzania (Tama), Nicodem Komba alisema ijapokuwa utafiti unaendelea kufanywa, lakini athari zake zinaonekana, kwani wengine wanapoteza maisha.

Alisema maji moto hutanua mishipa ya damu na hivyo husababisha athari kubwa mpaka kwenye moyo.

“Ni hali ambayo huwa tunaishuhudia kwa wagonjwa wa aina hiyo, mama akijifungua kiasi kikubwa cha maji hupungua mwilini, hivyo kufanya mishipa kusinyaa, sasa kukandwa na maji ya moto huzidi kulainisha mishipa ya damu na kufanya itanuke, kitu ambacho husababisha presha ya damu kupungua na kusababisha tatizo la ‘postpartum carsiomypathy’ (maradhi ya moyo baada ya kujifungua),” alisema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi katika Hospitali ya Aga Khan, Manuwar Kaguta alisema kwa wazazi tiba ya maji ya moto inatia hofu inavyotumika na ndiyo maana vituo vya afya havijawahi kumshauri mama au ndugu kwamba mama akandwe kwa maji moto kutokana na madhara yaliyopo.

Dk Kaguta alisema wengine hukanda mpaka sehemu za uke na kwamba hospitalini wamekuwa wakipokea kinamama waliopata athari za kukandwa na maji moto.

Husababisha vifo

Mwaka 2019 wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilisema mtindo wa kuwakanda na maji ya moto wanawake wakishajifungua ni hatari.

Wizara iliainisha kuwa kukandwa na maji ya moto kunaweza kusababisha mama kutokwa na damu nyingi na hata kifo.

“Hatuwezi kushauri wanawake waliojifungua kukandwa maji ya moto, japo suala hilo limezoeleka kwa wengi, lakini hakuna uthibitisho wa kitaalamu wa kumponya mwanamke kwa kutumia maji hayo isipokuwa kumletea madhara,” ilielezwa.

Chanzo: mwananchidigital