Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Athari matumizi holela ya dawa za nguvu za kiume

239eff8ca13cdaaac2c91b0107cc576f Athari matumizi holela ya dawa za nguvu za kiume

Mon, 27 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Upungufu wa nguvu za kiume ni hali ya sehemu za siri za mwanaume kuwa na uwezo mdogo au kutokuwa na uwezo kabisa wa kuhimili tendo la ndoa kwa muda mrefu.

Tatizo hili limekuwa kubwa katika jamii na kwa kufuata mkumbo, kumeibuka matumizi mabaya ya dawa za aina mbalimbali zikihamasishwa kurudisha nguvu hizo.

Dawa hizi kwa kawaida hufanya kazi ya kurekebisha mzunguko wa damu ndani ya mishipa ya sehemu hizo za siri na kuongeza kiwango cha damu hivyo kuifanya ifanye kazi vizuri.

Kitabibu zinatumika kutibu wanaume wenye uwezo mdogo au wasiokuwa na uwezo kabisa wa kuhimili tendo la ndoa.

Hata hivyo, hatari ni kwamba wanaume wengi wanatumia dawa hizo bila kufuata ushauri wa daktari huku kukiwa na madhara makubwa kwa watumiaji.

WANAOTUMIA HAWAJUI MADHARA

Uchunguzi uliofanywa na HabariLEO ulibaini kuwa wanaume wanaotumia dawa hizo hawaelewi madhara yake.

Katika mahojiano na wanaume zaidi ya watano wanasema hakuna anayejali kwenda kwa daktari kupata ushauri wa namna ya kutumia.

Miongoni mwao alijitambulisha kwa jina moja la Noel anasema dawa alizowahi kutumia ni zile za tiba asili maarufu kama alkasusu.

“Mimi sijawahi kutumia dawa za kisasa ila alkasusu nimewahi kunywa wanasema inasaidia kuongeza nguvu za kiume, si kwamba nina tatizo nimekunywa kupasha tu ili niwe na nguvu zaidi,” anaeleza Noel.

Kijana mwingine, Saimon Mgonja anasema katika stori za vijana mtaani wapo wanaodai kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume kutokana na nguvu hizo kushuka.

“Hawaendi kwa daktari wala mtaalamu wa afya wengi wanasema wananunua dukani na kutumia tu bila hata kufuata dozi,” anaeleza Mgonja.

Si vijana tu hata wazee kwa idadi kubwa hutumia dawa hizo ili kuwasaidia kufanya tendo hilo kama awali.

Daktari Bingwa wa Wanaume katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dk David Mgaya anasema kadiri umri unavyosonga mwanaume anapoteza nguvu/uwezo wa kushiriki tendo la ndoa.

“Ni kwasababu mzunguko wa damu unapungua na pia mishipa inaanza kuchoka lakini uzalishaji wa mbegu unabaki palepale lakini kuna sababu zingine zaidi,” anabainisha Dk Mgaya.

Hali hiyo hufanya wanaume ambao umri umeenda kutafuta njia mbadala ya kuhakikisha wanafanya tendo hilo kama walivyokuwa vijana hasa pale wanaposhiriki na mabinti wadogo na tatizo linakuwa kubwa kwa kuwa wengi hawajui madhara yake.

MADHARA YA MATUMIZI HOLELA

Kaimu Mkurugenzi Udhibiti wa Dawa wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Dk Yonah Mwalwisi anasema dawa hizo husababisha kusimama kwa sehemu za siri za mwanaume kwa muda mrefu hali inayoweza kusababisha maumivu ya sehemu hizo kwa muda mrefu.

Anasema lisipodhibitiwa kwa haraka linaweza kuharibu mishipa laini iliyoko ndani ya sehemu hizo na kusababisha tatizo kubwa.

Madhara mengine aliyoainisha ni zikitumika sambamba na dawa zinazotibu maumivu ya moyo, husababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa shinikizo la damu, kupata kizunguzungu, kuzimia, mshtuko wa moyo, kiharusi na mengine ambayo husababisha kifo.

NANI ANAPASWA KUTUMIA DAWA HIZO?

Kwa mujibu wa Dk Mwalwisi, mwanaume aliyegundulika kitaalamu kuwa na tatizo hilo na daktari atamchagulia aina ya dawa na kumuelekeza matumizi sahihi ya dawa hiyo.

Anasema kwa kawaida dawa hizo huchukua takribani dakika thelathini ili kuanza kufanya kazi kama hakuna vikwazo vya mwili au mwingiliano na dawa zingine.

Pamoja na hayo anaeleza kuwa kitaalamu dawa hizo zina muda maalumu wa kuzitumia na wengi hupewa saa moja kabla hajakutana na mwenza wake.

“Haishauriwi kabisa kutumia dawa hizi zaidi ya mara moja kwa siku na ni muhimu kuwasiliana na mtaalamu wa afya kama kuna umuhimu wa kukuchagulia dawa yenye kufanya kazi kwa muda mrefu mfano ili kuepuka matumizi ya mara kwa mara ya dawa,” anasema Dk Mwalwisi.

DAWA ZINAFANYA KAZI KILA UNAPOTUMIA?

Kwa mujibu wa Dk Mwalwisi, dawa hizo hazitafanya kazi moja kwa moja au vizuri endapo tatizo hilo la kupungukiwa na nguvu za kiume linatokana na kuathirika kisaikolojia.

“Mfano kutokuwa na hamu ya kufanya mapenzi, kutokujiamini, woga au kuwa na hofu ya kimapenzi na mwenza wako. Tafiti zimeonesha kuwa dawa hizi hazitibu kabisa hayo na haziongezi hamu au shauku ya kufanya mapenzi,” anasema.

Anasema mhusika mwenye tatizo anapaswa kumwona daktari ili afanyiwe uchunguzi wa chanzo cha tatizo, ukubwa wake na kupewa aina ya dawa na matumizi sahihi.

AINA ZA DAWA ZINAZOTUMIKA

Dk Mwalwisi anasema dawa zinazotumika kutibu tatizo hilo zipo kwenye kundi linaloitwa phosphodiesterase type 5 (PDE5) inhibitors ambazo husababisha mzunguko wa damu kuwa mzuri ndani ya mishipa ya sehemu za siri za mwanaume.

“Mifano ya dawa hizi ni Sildenafil, Tadalafil, Vardenafil na Avanafili na kati ya dawa hizi nne, tatu zimesajiliwa na TMDA na zina majina tofauti tofauti kama vile Sindenafil majina mengine ni Evoke, Erecto, Zwagra, Silment, Njoi na Viagra, nyingine ni Tadalafil (Saheal na Cialis) na Vardenafil (Levitra).

INAWEZEKANA KUTIBU BILA DAWA

Dk Mwalwisi anabainisha kuwa upungufu wa nguvu za kiume husababishwa na vyanzo mbalimbali mfano kunywa pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi, ukubwa wa mwili, uvutaji wa sigara au dawa za kulevya, msongo wa mawazo, kuwa na vichocheo vichache na aina ya vyakula.

Dk Mwalwisi anasema kama tatizo linasababishwa na hayo aliyoeleza hapo juu linaweza kupona au kupungua kwa kiasi kikubwa endapo atafuata ushauri wa daktari na kuacha yaliyoelezwa hapo juu.

“Kama chanzo ni upungufu wa hormones za kiume, basi matibabu ya aina hiyo yatahitajika, kuacha kutumia dawa nyingine ambazo husababisha tatizo hili, kupunguza uzito, kufanya mazoezi pamoja na kubadilisha hali ya kuishi ambayo ilikusababishia tatizo hilo pia zinaweza kusaidia kutibu kabisa tatizo hili,” anasema.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), anasema mwanaume kama ana akili imejaa msongo wa mawazo (stress) anakosa uwezo wa kufanya ngono kwani ubongo unakataa kutokana na kile unachofikiri.

“Mimi naamini kupungua nguvu inatokana na uwezo wa akili, kuna mwingine akiwa na mwanamke fulani hafanyi vizuri na akikutana na mwingine anafanya vizuri kwa hiyo kinacholeta hamu ni uwezo wa mawazo,” anaeleza.

HALI ILIVYO NCHINI

Kwa tathmini za TMDA, utumiaji wa dawa hizo kwa wanaume umekuwa ukiongezeka siku hadi siku hali inayoonesha kuwa wanaume wengi wameathirika na tatizo la upungufu wa nguvu za kiume.

Utafiti unaendelea kufanywa na mamlaka hiyo ili kugundua kiwango cha utumiaji wa dawa hizo nchini.

Anasema taarifa zisizo rasmi zimeripotiwa kuwa uwepo wa madhara kiharusi, mshtuko wa moyo, kuzimia na pengine kifo kutokana na matumizi holela ya dawa hizo.

Dk Mwalwisi anasema matukio hayo yanafuatiliwa na kuchunguzwa na TMDA kupitia programu ya ufuatiliaji wa usalama wa dawa sokoni.

TMDA INASHAURI HAYA

TMDA inashauri jamii kubadilika na kuacha kutumia dawa hizo holela na kuhakikisha mtu anamwona daktari.

“Daktari atachunguza chanzo na ukubwa wa tatizo kabla ya kukupa dawa sahihi na pengine kuangalia kama unatumia dawa zingine ili kuepusha mwingiliano unaoweza kusababisha hatari za kiafya,” anasisitiza Dk Mwalwisi.

WANAOUZA WATAKIWA KUFANYA HAYA

Wamiliki wa maduka ya dawa, wafamasia na wataalamu wengine wa afya kwenye maduka ya dawa ya rejareja wanatakiwa kuacha uuzaji holela wa dawa hizo bila uwepo wa cheti cha daktari.

Aidha, anasema ni muhimu wamiliki wa nyumba za wageni kuripoti TMDA matukio yote yenye viashiria ya madhara yatokanayo na matumizi ya dawa hizo ikiwemo vifo na madhara mengine.

TMDA INAHAKIKISHA UBORA NA USALAMA

Mkurugenzi wa TMDA, Adam Fimbo anasema wanafanya tathmini stahiki ya dawa zinazoletwa wakati wa usajili ili kujiridhisha ubora, usalama na ufanisi wake kabla ya kusajiliwa.

Pia anaeleza kuwa wanafanya ukaguzi wa viwanda vya dawa ambazo zimeombewa usajili nchini ili kujiridhisha na ubora wa uzalishaji wa viwanda hivyo.

“Tunafanya udhibiti na ufuatiliaji wa dawa zote nchini na kutoa vibali vya kuingiza na kutoa dawa nchini, tunapita sokoni kufuatilia na kuendelea kujiridhisha na ubora, usalama na ufanisi wa dawa.

“Tunaweka taarifa za matumizi na lebo za dawa kwenye tovuti kwa lengo la kuwahabarisha watumiaji na kutoa elimu kwa umma ili kuleta uelewa wa dawa hizi pamoja na bidhaa zingine zinazodhibitiwa na TMDA.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live