Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 98 ya wajawazito wanahudhuria kliniki

45969 Pic+wajawazito Asilimia 98 ya wajawazito wanahudhuria kliniki

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali imesema idadi ya wajawazito wanaohudhuria kliniki imeongezeka hadi kufikia asilimia 98, huku upatikanaji wa dawa muhimu ukifikia asilimia 94 kutoka 53 mwaka 2015/16.

Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akitolea ufafanuzi juu ya huduma za afya ya uzazi nchini.

“Kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2018, jumla ya wajawazito 1,004,458 walihudhuria kliniki wakati wa ujauzito na kati ya hao 632,627 walitimiza mahudhurio manne au zaidi (ANC4+). Hii ni sawa na asilimia 59 ikilinganishwa na asilimia 51 kwa kipindi kama hicho mwaka 2015/16,” amesema.

Amesema wizara imeamua kutoa tamko hilo ili kutoa ufafanuzi tena juu ya maboresho yaliyofanyika katika kuzitatua changamoto za afya ya uzazi na mtoto nchini.

Waziri Ummy amesema huduma za afya katika kundi hilo ni mojawapo ya kipaumbele kikubwa cha Serikali ya awamu ya tano kwani zimeendelea kuimarishwa na kuboreshwa katika maeneo yote nchini zikiwemo huduma kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

“Idadi ya akina mama wanaohudhuria kliniki imezidi kuongezeka, sasa zaidi ya asilimia 98 ya wajawazito huhudhuria kliniki walau mara moja, tangu utafiti wa TDHS mwaka 2015/16. Aidha, bajeti ya Serikali ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba imeongezeka zaidi ya mara tisa, kutoka Sh31 bilioni mwaka 2015/16 hadi  Sh270 bilioni mwaka 2018/19,” amesema.

Ummy amesema ongezeko hilo la kibajeti na usimamizi imara wa rasilimali vimeongeza upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma.

“Tumetoka asilimia 53 mwaka 2015/16 hadi kufikia asilimia 94 (2018/2019). Niwaombe wananchi na viongozi wenzangu tuendelee kutembelea kwenye vituo vyetu vya huduma ili kujionea haya badala ya kuendelea kubeza kwenye mitandao ya kijamii,” amesisitiza Ummy Mwalimu na kuongeza;

“Juhudi hizi zimewezesha wajawazito wengi kupata huduma za dawa kinga zikiwemo SP, ambayo ni kinga tiba dhidi ya malaria, Fefol ambayo ni kinga au tiba dhidi ya upungufu wa damu, vipimo vya pressure, kaswende, wingi wa damu, sukari na magonjwa mengine kwa kiwango kikubwa.”



Chanzo: mwananchi.co.tz