Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 75 magonjwa ya kuambukizwa hutoka kwa wanyama

50736 Pic+ifakara

Sun, 7 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Asilimia 75 ya magonjwa anayoambukizwa binadamu yanatoka kwa wanyama na miongoni mwa magonjwa hayo ni mafua ya ndege, kichaa cha mbwa na ugonjwa wa Ebola.

Kutokana na hali hiyo, Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), imeanza kufanya utafiti katika mikoa ya Kigoma na Kagera.

Hayo yameelezwa Ijumaa Aprili 5, 2019 na Msajili wa Baraza la Veterinari, kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bedan Masuruli.

Masuruli alisema hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Elisante Ole Gabriel, wakati akifungua mafunzo ya wataalamu wa maabara kutoka idara ya afya.

"Asilimia 75 ya magonjwa anayoambukizwa binadamu yanatoka kwa wanyama, hivyo tumeanza kufanya utafiti ili kukabiliana na tatizo hilo" alisema.

Pia alibainisha kuwa asilimia 60 ya magonjwa yote yaliyogundulika katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, yalitoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Alisema mafunzo hayo yametolewa kwa wataalam hao kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa yanayoweza kutokea kutokana na mwingiliano wa nchi na nchi.

"Tunatambua juu ya umuhimu wa afya ya binadamu lakini wakati huo huo tunatambua pia umuhimu wa afya ya wanyama, ndio maana tumeamua kutoa mafunzo hayo," alisema

Awali, mkuu wa idara ya utafiti wa dawa na chanjo kutoka IHI, Dk Ally Olotu, amesema baada ya kuona magonjwa mengi yanasababishwa na wanyama, taasisi yake kwa kushirikiana na wadau wengine, wameamua kufanya utafiti katika mikoa ya Kigoma na Kagera ambayo inapakana na nchi zenye changamoto ya magonjwa yanayoenezwa na wanyama.

Alisema lengo la kufanya utafiti huo ni kubaini ukubwa wa tatizo hilo na kulifanyia kazi. "Kama maradhi yanatoka kwa wanyama ni mengi na sisi binadamu tunakuwa na maingiliano na wanyama kwa sababu tunaishi nao, hali hi ndio imepelekea sisi tuanze kufanya utafiti," alisema Dk Olotu.

Alisema utafiti huo hautaangalia sehemu moja, bali utaangazia muingiliano wa binadamu, mazingira, wanyama pori na wale wanaofugwa majumbani.

Kwa upande wake, Profesa Rudovick Kazwala, ambaye ni mtafiti mwandamizi wa Mradi wa Predict, alisema wanaangalia vimelea hatarishi hasa virusi vinavyoweza kuambukiza kutoka kwa wanyama wanaofugwa au wanyamapori kwenda kwa binadamu, au kutoka kwa binadamu kwenda kwa wanyama.

Akizungumzia mradi wa Predict, Profesa Kazwala, alisema mradi huo, unafanya utafiti wa magonjwa ambukizi ya wanyama na binadamu hapa nchini.

Alisema katika utafiti huo wanaangalia maeneo ambayo yanajulikana kuwa yapo katika eneo hatarishi katika mikoa ya Kigoma na Kagera.

Profesa Kazwala alisema Tanzania inapakana na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo inasumbuliwa na ugonjwa wa Ebola na kwamba ugonjwa huo, unatoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Mbali na Ebola, magonjwa mengine yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu ni kimeta, mafua ya ndege, homa ya bonde ya ufa na kichaa cha mbwa.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz