Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 66 ya wagonjwa wa TB Tanzania hawapati tiba

Wed, 17 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania  imesema wagonjwa wa kifua kikuu (TB) 69,818 kati 154,000 sawa na asilimia 66 hawajaanza kupata matibabu.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Julai 17, 2019 na kaimu mkurugenzi wa kitengo cha kudhibiti kifua kikuu cha Wizara ya Afya, Dk Deusdedit Kamala alipokuwa akitoa mada  katika kamati ya Bunge ya Kifua kikuu.

Katika mkutano huo uliowahusisha viongozi wa madhehebu ya dini, Dk Kamala amesema asilimia 44 ya walioanzishiwa matibabu hupona kwa asilimia 90.

"Shirika la afya Ulimwenguni linakadiria kuwa 154,000 huugua TB, Lakini asilimia 66 hawapati matibabu. Kati ya wagonjwa 69,318 sawa na asilimia 44 wanaotibiwa wagonjwa 63,000 sawa na asilimia 90 hupona," amesema Dk Kamala.

Amesema kwa takwimu za dunia,  kuna watu  bilioni mbili walioambukizwa TB lakini haijaanza kujionyesha,  kwamba kwa Tanzania wapo wagonjwa milioni 18  wasiojijua.

"Kila mwaka watu 1.7 milioni hufa kwa TB. duniani, kwa Tanzania watu wasio na Ukimwi 27,000 hufa na wakijumlishwa na wenye Ukimwi wanafikia zaidi ya 49,000," amesema.

Pia Soma

Dk Kamala ameongeza wagonjwa wengi hawapatiwi matibabu kwa kutokuwepo mwamko na uelewa kuhusu ugonjwa huo.

Amesema Serikali inatoa matibabu bure ya TB ambako mgonjwa sugu anagharimu zaidi ya Sh1 milioni kwa miezi tisa wakati ya kawaida ni Sh600,000 kwa miezi sita.

Akizungumza katika mkutano huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema wamelazimika kuwaita viongozi wa dini ili kutoa elimu kwa waumini wao kuhusu hatari ya ugonjwa huo.

"Tumewaita hapa kwa sababu mna washirika wengi wanaowasikiliza. Tunataka kuwafikishia ujumbe wa kifua kikuu.”

"Kuna maeneo ya magereza ambayo viongozi wa dini mnaweza kuingia kuhubiri, ishaurini serikali kutenga fedha. Wagonjwa wengine wapo kwenye machimbo ya madini, makazi duni, kote wanahitaji kufikiwa," amesema Ndugai.

Chanzo: mwananchi.co.tz