Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 60 ya saratani inazuilika, chukua hatua

12f91d54408a5719b958e0f576be1b1a.png Asilimia 60 ya saratani inazuilika, chukua hatua

Mon, 3 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Saratani ni mojawapo ya magonjwa ambayo serikali inayavalia njuga kuyatokomeza na kutoa wito kwa wataalamu wa afya kubaini chanzo cha ugonjwa huo kuathiri zaidi wananchi wa Kanda ya Ziwa hasa wanawake.

Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando kufanya utafiti kubaini ongezeko la saratani ya mlango wa shingo ya kizazi na matiti kwa wanawake.

HabariLEO liliwasiliana na Dk Merchades Bugimbi, daktari mwenye uzoefu katika mikoa hiyo ya Kanda ya Ziwa kujua kwa nini saratani inawasumbua zaidi wakazi wa kanda hiyo.

Dk Bugimbi alisema saratani inatajwa kuathiri zaidi wanawake katika kanda hiyo kwasababu mbalimbali.

Anasema wingi wa wananchi katika eneo hilo unaochangiwa na hamasa ya kupima afya hasa kampeni za saratani ya shingo ya kizazi na matiti kwa wanawake wa kanda hiyo ni mojawapo ya sababu za

kitakwimu kuwa na watu na wanawake ni wengi pia.

Kuna sababu kadhaa zinazotolewa na baadhi ya watu wakidai ni uchafuzi wa mazingira kutokana na uchimbaji wa madini na kutumia zebaki ambapo watu hufanya uchenjuaji wa madini kwenye mito maji hayo watu huyatumia kunywa, kuoga na matumizi mengine ya nyumbani hivyo kusababisha kuenea kwa saratani.

HabariLEO lilipouliza iwapo mapenzi umri mdogo ni sababu ya saratani ya shingo ya kizazi, Dk Bugimbi alisema visababishi vya saratani ya shingo ya kizazi ni vingi lakini virusi aina ya “Herpes” ni mojawapo ya sababu na anasema tohara kwa wanaume ni kinga iliyo

sahihi kwa wanawake dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi.

Hata hivyo, Dk Bugimbi anasema saratani inayoathiri zaidi wanawake Kanda ya Ziwa ni ya matiti.

Rais Samia aliwahi kuonesha masikitiko yake kwa ongezeko la kasi la wagonjwa wa saratani kutoka wagonjwa 1,200 mwaka 2019 hadi kufikia wagonjwa 1,500 mwaka 2021 hali inayokwamisha uzalishaji mali na kufifisha jitihada za serikali katika kuleta maendeleo.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, mwili wa mwanadamu una chembechembe hai nyingi ambazo huzaliana, kukua na kufa kwa mpangalio maalumu, chembe chembe hizo zinapobadilika, kuzaliana na kukuwa kwa utaratibu usio kawaida na kusababisha saratani.

Chembechembe za saratani hufuata mfumo usio wa kawaida zinazaliana haraka zaidi bila mpangilio na kukuwa kwa haraka zaidi na wakati mwingine kuwa na umbile kubwa zaidi, chembe chembe hizo za saratani zisipodhibitiwa au zisipotibiwa mapema zina uwezo wa kusambaa na kuota sehemu nyingine ya mwili wa mhusika.

Taasisi hiyo inasema saratani ni uvimbe unaojitokeza mahala popote katika mwili wa binadamu, uvimbe huu hauna maumivu yoyote mwanzoni.

Aidha, taasisi hiyo inasema saratani zipo za aina nyingi sana majina yake hutegemea kiungo kilichougua na aina ya chembechembe hai zilizoshambuliwa kiungo chochote kinaweza kushambuliwa.

Anatoa mfano shingo ya mfuko wa kizazi, matiti, ngozi, koo na njia ya chakula, tumbo, utumbo, kongosho, ini, kibofu cha mkojo, tezi dume, mapafu, ubongo, macho, mifupa, misuli, matezi hasa kwa watoto, damu na nyinginezo.

Ocean Road inasema hakuna sababu moja pekee ambayo husababisha saratani bali mchanganyiko wa vitu vingi vinavyomzunguka mwanadamu ikiwemo viumbe hai, kemikali na aina ya maisha anayoishi huchangia mtu kupata saratani.

Taasisi hiyo inasema saratani tofauti zina vyanzo tofauti visivyozuilika kama vile jinsia, umri, uwezekano wa kurithi na mionzi ya jua.

Taarifa ya Ocean Road inaainisha saratani zinazuilika kama vile matumizi ya kemikali au mionzi, uvutaji sigara, maambukizi baadhi ya vimelea mfano virusi, bakteria, fangasi na matu

mizi zaidi ya pombe.

Pia ulaji ovyo kama vile mafuta mengi, nyama nyekundu kwa wingi, kutofanya mazoezi, unene uliokithiri, dawa, sumu za kuulia wadudu, dawa za kulainisha nywele na wasichana kuanza ngono katika umri mdogo.

Taasisi hiyo inasema kila saratani ina dalili zake kutokana na ilipoanzia, awali saratani haina maumivu ni vigumu kugundua kama ipo ndani, uvimbe sehemu yoyote ya mwili, mafindofindo, mabadiliko ya haja kubwa au ndogo na kidonda kisichopona.

Pia dalili nyingine ni damu kutoka bila mpangilio au uchafu usio wa kawaida sehemu za siri (uke), shida kumeza au kupumua, sauti inayo kwamakwama, kuvimba mdomo au tumbo kwa watoto.

Taasisi hiyo inasema mgonjwa asipotibiwa mapema saratani huwa kubwa zaidi na kufanya kidonda, maumivu makali, kusambaa katika viungo vingine vya mwili hasa mapafu- kukohoa na maumivu, ini, kujaa tumbo, macho kuwa ya njano na maumivu, mifupa kuwa na maumivu au kuvunjika ovyo, kupoteza kiungo vya mwili.

Ocean Road inasema saratani inahakikiwa kwa njia ya kutoa kinyama au ute wa chembechembe husika na kupimwa katika maabara maalumu, vipimo vingi vya maabara vinaonesha tu mabadiliko yenye kuashiria uwezekano na siyo uhakiki.

Aidha, inasema tiba za kitaalamu zilizohakikishwa ni kama vile upasuaji, dawa za mshipa, dripu, vidonge na mionzi, tiba ya vichochezi (Homoni), tiba hizo hutumika mchanganyiko kutegemea aina ya saratani, hatua ya ugonjwa na hali ya kiafya ya mgonjwa.

Inasema tiba mpya kwa ujumla inalenga kupunguza na kuzuia uwezekano wa kupata saratani, taasisi hiyo inasema asilimia 66 ya saratani zinazuilika.

Taasisi hiyo inatoa wito kuepuka viashiria hatarishi vinavyozuilika kama vile kutovuta sigara, kuepuka unene wa kupitiliza, kufanya mazoezi mara kwa mara, ulaji bora kama vile kuepuka matumizi ya mafuta mengi na nyama nyekundu kwa wingi.

Inaitaka jamii kula matunda na mbogamboga kwa wingi, kuepuka matumizi zaidi ya pombe, kujikinga na mionzi ya jua hasa kwa watu wenye ualbino, kupima afya mara kwa mara, chanjo kwa saratani zenye chanjo mfano ya homa ya ini na mlango wa kizazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live