Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 56 ya wanaougua TB hawajaanza tiba

Thu, 6 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Imeelezwa kuwa kati ya wagonjwa wote wanaougua kifua kikuu nchini ni asilimia 44 tu ndiyo  waliogundulika na kuanzishiwa dawa, huku asilimia 56 wakiwa bado hawajaanza kupata tiba.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na mkurugenzi wa huduma za tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk Leonard Subi wakati akizungumza na wataalamu wa afya na waratibu wa kifua kikuu kutoka mikoa na halmashauri zote nchini.

Amesema  mapambano ya dhati yanahitajika  kudhibiti  kifua kikuu kwani jitihada zilizopo hazijaweza hata kuwafikia nusu ya wagonjwa wote wa TB na  wengi wao wanaendelea kuambukiza wengine.

"Kati ya Watanzania 100,000, 266 wameambukizwa kifua kikuu na hii haichagui mwanamke, mwanaume, kijana, mtoto au mzee. Ni lazima tuongeze juhudi kuwatambua wagonjwa wote ili tuweze kuwatambua na kuwapa tiba," amesema.

Amesema pamoja na juhudi zinazofanyika bado Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo ugunduzi wa kifua kikuu uko chini kutokana na kutowafikia hata nusu ya wagonjwa wote.

Ameeleza kuwa mpango mkakati uliopo sasa ni kuwagundua wagonjwa wote wa TB na kuwaanzishia matibabu.

“Mwaka 2017 wagonjwa 200 walikuwa na vimelea sugu vya TB ambao wapo katika jamii na wanaendelea kuambukiza kwa kuwa vimelea vyao havisikii tena dawa,” amesema.Meneja wa kudhibiti ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wizara hiyo, Dk Beatrice Mtayobwa amesema lengo la Serikali ni kupunguza maambukizi wa TB kwa asilimia 30 kufikia mwaka 2020.

Amesema mwaka 2016 pekee asilimia 40 ya wagonjwa wa ukimwi waliofariki dunia vifo vyao vilisababishwa na TB.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz