Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Asilimia 30 ya watu wazima wanaugua shinikizo la damu

Sat, 20 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa asilimia 30 ya watu wazima, kadirio la watatu kati ya 10 hapa nchini wana tatizo la shinikizo la damu maarufu presha.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Hospitali ya Heameda na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Hery Mwandolela wakati wa kambi ya  upimaji afya wa hiyari iliyoanza leo na inatarajiwa kumalizika Oktoba 20. 

"Kasi ya magonjwa yasiyoambukiza yanazidi kuongezeka kwa kipindi cha miaka 30 sasa, kadirio la haraka Tanzania watu wazima asilimia 30 wana tatizo hili, tafsiri yake ni kwamba kati ya watu wazima 10 watatu wana shinikizo la damu," amesema.

Dk Mwandolela amesema mgonjwa wa shinikizo la kupanda kwa damu asipotibiwa kwa muda mrefu hupata madhara makubwa.

"Kwa haraka huwezi kuona madhara lakini unapopata shinikizo la damu la kupanda  kwa muda mrefu kunakuwa na uharibifu ambao unatokea kwenye mifumo mbalimbali mwilini kama macho, kufeli kwa ini, figo, moyo na magonjwa mengine yasiyoambukiza kama saratani, kiharusi na mengineyo," amesema.

Amesema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa yakiongezeka kutokana na mfumo wa maisha na namna tunavyokula.

Akizungumzia kambi hiyo, Dk Mwandolela amesema zaidi ya watu 150 wamejitokeza siku ya kwanza.

"Mpaka sasa tumeshawapima watu 130 na kati yao wengi wamekutwa na tatizo la shinikizo la damu, tumewapatia ushauri lakini tumewaanzishia dawa ambazo watakuwa wakitumia na kwa kambi hii vipimo na matibabu ni bure," amesema.

Amesema wapo waliokutwa na tatizo la moyo, macho, uzito mkubwa na magonjwa mengine.

Mmoja kati ya wagonjwa waliopimwa katika kambi hiyo, Anyamisye Mwakasyuka mkazi wa Mabwepande amesema hakuwa akifahamu iwapo ana tatizo la shinikizo la damu lakini amepewa ushauri na dawa ili kuanza matibabu.

Naye meneja masoko kutoka hospitali ya macho ya The International Eye, Claudius Katundu amesema wamefika kwenye kambi hiyo kwa ajili ya kushirikiana na wataalamu wengine kupima macho.

"Tumekuwa tukifanya kampeni mbalimbali lakini nia kubwa ni watu waweze kujua madhara yanayoweza kuwapata wasipotibu macho lakini pia kutoa ushauri nasaha, magonjwa yanayotibika hapa tunatibu na wenye matatizo makubwa zaidi tunawapatia rufaa," amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz