Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ashauri kupunguza uvutaji sigara, pombe na chumvi

93ca6978689416c7ec4c9bfc11dae4f8 Ashauri kupunguza uvutaji sigara, pombe na chumvi

Tue, 10 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imesema kuna ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini hivyo wananchi waepuke mambo kadhaa ikiwamo kuacha kuvuta sigara, kupunguza unywaji wa pombe na matumizi makubwa ya chumvi.

Aidha, imesema imekamilisha tathimini ya mpango wa kuongeza watumishi wa afya katika vituo vya afya kote nchini na kuwataka wanasayansi waongeze kasi ya kufanya utafiti ukiwemo kuhusu dawa za asili ili kukabili maradhi hayo.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Abel Makubi aliyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Pili la Kitaifa la Kisayansi la Magonjwa Yasiyoambukiza.

Katika kongamano hilo, Profesa Makubi alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Profesa Mabula Mchembe.

Profesa Makubi alisema kuna ongezeko la hatari ya sigara kusababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama ilivyo kwa pombe na chumvi.

“Naomba nitoe mwito kwa kila mtu kuhakikisha anafanya mazoezi dakika thelathini angalau mara tatu kwa wiki ili kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Lakini pia kwa kuwa matumizi ya sigara ni hatari zaidi, nashauri watu waache kabisa kuvuta sigara,” alisema Profesa Makubi.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kila baada ya sekunde nane mtu huaga dunia kutokana na matumizi ya tumbaku na kwamba utafiti unaonesha kuwa watu wanaoitumia katika umri mdogo wakiendelea kutumia kwa zaidi ya miaka 20, hufa miaka ishirini na mitano zaidi ya wasiotumia tumbaku.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu upungufu wa watumishi wa afya nchini kama moja ya changamoto katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini, Profesa Makubi alisema pamoja na juhudi za kujenga miundombinu ya afya zikiwemo zahanati na vituo vya afya, serikali imekamilisha tathmini na ni kipaumbele chake kupeleka watumishi wa afya zaidi kote nchini kumaliza tatizo.

Alisema watumishi hao watakuwa wamepewa mafunzo ya namna ya kukabili magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kuhakikisha wanawapima watu wanaofika hospitali kwa tiba magonjwa mengine ikiwemo shinikizo la damu na sukari ili kutoa ushauri kwa watakaogundulika na maradhi hayo waanze tiba mapema.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas), Profesa Andrea Pembe akizungumza na wanahabari baada ya ufunguzi, alisema matatizo ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza katika jamii yameongezeka na ni kati ya asilimia 18 hadi 30, wakati miaka ya 1960 ilikuwa ni tatizo kwa asilimia moja.

Mgeni rasmi Profesa Mchembe katika hotuba yake iliyosomwa na Profesa Makubi, aliwataka wanasayansi nchini kuongeza kasi ya utafiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili kupata njia sahihi za namna ya kuyakabili ikiwamo matumizi ya dawa za asili zilizoonesha mafanikio katika kupunguza pumu na shinikizo la damu.

“Nchi inahitaji utafiti utakaosaidia kuboresha huduma za afya, tunataka majibu ya changamoto zetu yatokane na utafiti wetu wenyewe ingawa sisemi tuziache za wenzetu bali tuzitumie kuboresha za kwetu kwa kuwaza ‘globally’ (kimataifa) na kutenda ‘locally’ (kitaifa),” alisema Profesa Mchembe katika hotuba yake.

Alitoa mfano namna wanasayansi wa Kitanzania walivyodhibiti ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) na kutaka utafiti kama huo ufanywe kwenye dawa za asili ili kupunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Chanzo: habarileo.co.tz