Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Akumbusha jamii kujua visababishi vya lishe duni

2f233c5ab7d2d9ceee9d487ff45d8436 Akumbusha jamii kujua visababishi vya lishe duni

Mon, 8 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Kalobelo ameitaka jamii kuelewa visababishi vya lishe duni katika jamii na jinsi ya kukabiliana navyo.

Kalobelo alisema hayo wakati akifungua kikao cha wadau wa lishe wa mkoa huo kilichofanyika hivi karibuni chini ya uwezeshaji wa Mradi wa Lishe Endelevu , unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani (USAID).

Alisema ni vyema kwa kila halmashauri ya wilaya kuainisha changamoto zinazosababisha watoto chini ya umri wa miaka mitano kuwa na utapiamlo pamoja na udumavu ili changamoto hizo ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Katika kufikia malengo hayo , aliwaagiza wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha wanaandaa programu za lishe endelevu katika halmashauri zao kabla au ifikapo Novemba mwaka huu.

Pia aliwataka kuzingatia maelekezo ya serikali ya kumtengea kiasi cha Sh 1,000 kila mtoto wa umri chini ya miaka mitano kutoka mapato yao ya ndani kwa ajili ya kuboresha lishe kwa watoto hao.

Wakichangia mada katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe, aliishauri Kamati ya Lishe Endelevu ngazi ya mkoa kuweka mipango mkakati ya kuwafikia waathirika wa mimba za utotoni hususani wanafunzi.

Alisema mpango mkakati huo wa kuwafuatilia wao na watoto waliowazaa kuona afya zao ili na wao waweze kuhudumiwa kama yalivyo makundi mengine katika kupata lishe endelevu kwa ajili ya kuwaokoa watoto wao na udumavu.

Mkuu wa wilaya huyo pia alitaka kuwepo na ufuatiliaji wa Sh 1,000 zinazotengwa kwa kila mtoto chini ya umri wa miaka mitano na halmashauri za wilaya kwenye bajeti zao ili kuona matumizi yake kama yanawanufaisha walengwa badala ya kupewa taarifa na takwimu pekee.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi , Mathayo Maselle ametoa rai kwa kamati hiyo kutoa elimu ya lishe kwa wanaume ili iwasaidie kutambua aina gani ya vyakula wanatakiwa kula na kwa wakati gani, lengo ni kujenga afya bora ya miili yao na familia kwa ujumla.

Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishajimali, Dk Rozalia Rwegasira, aliwataka wadau mbalimbali pamoja na wataalamu wa afya kutoa elimu juu ya ulaji wa vyakula bora ,kula vyakula vya makundi yote matano badala ya mazoea ya kupenda kula vyakula kwa kufuata ladha pekee.

Naye Meneja wa Mpango wa Lishe Endelevu mkoa wa Morogoro, Nuhu Salehe alisema mradi huo wa miaka minne ulioanza mwaka 2019 kwenye mikoa ya Dodoma, Rukwa , Iringa na Morogoro umelenga kuisaidia serikali katika mipango ya kuimarisha lishe bora kwa kuwafikia wanawake milioni 1.5 walio katika umri wa kuzaa kuanzia miaka 15-49.

Salehe alisema mradi huo pia umelenga kupunguza udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano wapatao milioni 1.1 na kuwaandaa wasichana 330,000 wa umri balehe kuanzia miaka 15-19.

Licha ya maeneo hayo, alisema mradi unalenga pia kuzijengea uwezo halmashauri katika kutekeleza Mpango Shirikishi wa Lishe wa Taifa (NMNAP 2016-21), kuimarisha uratibu kati ya halmashauri, asasi za kiraia na sekta binafsi katika kuboresha lishe.

Nao wadau wengine akiwemo Alexander Jokoniah wa Kongano la Usagishaji Nafaka Morogoro (KUNAMO), alishauri kamati hiyo iweke kipaumbele cha kutoa elimu kwa wazalishaji wa mazao ya chakula ili kuyaweka katika ubora kabla ya kusagwa kupata unga ama mchele kwa ajili ya kuboresha lishe endelevu.

Chanzo: habarileo.co.tz