Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajira za wahudumu wa afya ngazi ya jamii zasitishwa

31875 Ajira+pic Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tamisemi, Josephat Kandege

Mon, 17 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya/Dar es Salaam. Serikali imesema imesitisha kuajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii kupitia mradi wa Global Fund na badala yake inaelekeza nguvu kuajiri watumishi kwenye sekta ya afya.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tamisemi, Josephat Kandege alisema hayo baada ya kuwapo kwa barua inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inayotoka Tamisemi ikielekezwa kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mbeya na Chunya, ikimtaka kusitisha ajira hizo.

Kandege alisema Wizara ya Afya inajenga vituo vya afya na zahanati nyingi vijijini na mijini, hivyo ina uhitaji mkubwa wa wahudumu wa afya.

“Tukiwaajiri wahudumu wa afya ngazi ya jamii huku zahanati na vituo vya afya tulivyojenga vina ubora na uwezo wa kutoa huduma kubwa ikiwamo upasuaji, ina maana tulichofanya itakuwa kazi bure,” alisema

Alipopigiwa simu ili atolee ufafanuzi suala hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile aliomba atumiwe barua hiyo na alipotumiwa hakujibu na alipopigiwa alituma ujumbe mfupi kuwa yupo kikaoni.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Chunya mkoani Mbeya, Sophia Kumbuli alisema kulikuwa na mchakato unaendelea wa kutaka kuajiri watu wa kada hiyo, lakini suala la kusitishwa hana taarifa nalo.

“Sipo Chunya kwa muda mrefu kidogo, labda hiyo barua imekuja nyuma yangu, hiyo taarifa ya kusitisha kwanza ndiyo naipata kutoka kwako (mwandishi) na mimi nitafuatilia kwa wasaidizi wangu,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz