Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aina tano za uongo ambao wagonjwa huwaambia madaktari

9842 Afya+pic TZWeb

Sun, 24 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tabia ya kutosema ukweli kwa daktari ipo kwa wengi. Huenda sababu ikawa ni aibu mathalani inapotokea mgonjwa ana tatizo nyeti la kiafya na muhudumu wake afya au daktari wake ni wa jinsia tofauti.

Lakini aibu nyingine husababishwa na tofauti ya umri na hasa inapotokea kuwa umri wa daktari ni sawa na wa mgonjwa.

Ifahamike kuwa, katika sehemu ambazo unatakiwa kuwa huru na mkweli basi ni kwenye chumba cha daktari. Kuwa mkweli kwa daktari wako kutamsaidia yeye akupe huduma bora zaidi kutokana na kile ulichokipitia wakati mfupi au siku chache kabla hujapata tatizo.

unapaswa kujua ukweli kuwa, kuficha tatizo la kiafya kwa dakitari ni hatari kwa kuwa umuhimu wa tiba unaanza tangu maelezo ya awali ya mgonjwa kabla hata ya kufanyiwa vipimo.

Yafuatayo ni mambo ambayo watu hupendelea zaidi kuwaficha madaktari na nakusihi uache leo.

Sikunywa pombe

Wagonjwa wengi hukumbwa na aibu kueleza kwa daktari kama wamekunywa pombe muda mfupi kabla ya kulazimika kwenda hospitali kwa ajili ya huduma ya matibabu ya dharura.

Wakati unafikiria kumdanganya mtoa huduma wako wa afya unapaswa kuufahamu ukweli kwamba unywaji wa pombe unaweza kutoa majibu tofauti na tatizo lako kiafya ikiwa unalazimika kufanyiwa vipimo vya aina mbalimbali.

Hivyo ni vyema kuwa muwazi kwa sababu itamsaidia daktari aanze na huduma ya kuondoa kiasi cha pombe kinachozunguka mwilini ili utakapofanyiwa vipimo, upate majibu sambamba na tatizo lako la kiafya.

Nimeacha kuvuta sigara

unaweza kudhani kama ni jambo la kawaida ili kumficha mtoa huduma wako wa afya kumficha kama unavuta sigara, kuna umuhimu mkubwa sana yeye kujua ukweli huu. Baadhi ya tiba hasa ya vidonge inaharibiwa na utendaji kazi wake mwilini na ile sumu inayopatikana kwenye moshi wa tumbaku ambayo kitaalamu inajulikana kama Nicotine. Baadhi ya dalili za matatizo mbalimbali ya kiafya dalili zake husababishwa na uvutaji wa sigara kama vile kukohoa mara kwa mara, kupungua uzito kwa kasi na maumivu makali ya kifua.

Ni vyema kumwambia daktari kuwa pamoja na dalili hizi lakini pia unavuta sigara kama una tabia hiyo. Kwa kufanya hivyo utamfanya daktari kukupangilia tiba ya tatizo lako na kuangalia uwezekano wa kukupangia tiba ya kuacha uvutaji wa sigara haraka iwezekanavyo kwa kuwa uvutaji wa sigara ni hatari sana kwa afya.

Sikufanya tendo la ndoa

Hapa ndipo kwenye tatizo kubwa wagonjwa wengi wanakuwa wagumu sana kwenye eneo hili hasa inapofika kwenye masuala ya tiba ya magonjwa ya zinaa na masuala ya afya ya uzazi kwa ujumla. Sababu kubwa hapa ni aibu.

Wengi hujikuta wanapata magonjwa ya zinaa kutokana na tabia kufanya ngono isiyo salama na mbaya zaidi kufanya ngono na washirika tofauti tofauti ndani ya kipindi kifupi.

Wagonjwa wengi huwa wazito sana kuwa wa wazi kwenye eneo hili, na wakijitahidi sana kujaribu kusema ukweli basi mgonjwa anaweza kusema “Nilifanya ngono na mshirika mmoja tu mwaka huu” nakukumbusha kuwa, daktari hayupo kwa ajili ya kukuhukumu ila yupo kwa ajili ya kukusaidia.

Hivyo kuwa muwazi kwa kumueleza idadi ya watu ulioshirikiana nao tendo la ndoa kwa muda husika kutamsaidia daktari kukupa msaada wa huduma ya magonjwa ya zinaa na afya ya uzazi kwa ujumla kutoka kwenye maelezo yako ya awali.

Sina magonjwa ya zinaa

Kama una gonjwa lolote la zinaa basi unapaswa kukubaliana na ukweli kubwa unaumwa ugonjwa wa zinaa. Lakini hata kama ulikuwa na gonjwa la zinaa hapo awali, daktari pia anapaswa kujua hilo. Unaweza ukaona aibu kulisema hilo, lakini unapaswa kujua ukweli kuwa baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kuwa hatari  kama hayakupatiwa tiba stahiki.

Pia ni vyema kufahamu kuwa hata kama ulishawahi kuwa na ugonjwa wowote wa zinaa na baada ya muda ukatoweka, upo hatarini kujirudia bila kutibiwa. Unaporudi unakuwa na hatari zaidi kwa afya ikiwemo hata kusababisha kupoteza uwezo wa kuzaa.  Kukabiliana na aibu ukiwa na daktari wako kutakusaidia kuepukana na aibu utakazokutana nazo hapo baadaye kwenye maisha yako ya ndoa.

Sina tatizo kwenye nguvu zangu za jinsia

Eneo lingine ambalo wagonjwa wangu huwa wanakuwa wagumu sana kusema ukweli ni kwenye suala zima la nguvu za jinsia. Kukosa nguvu za jinsia ni tatizo linaloathiri jinsia zote mbili. Japo imezoeleka wanaume ndio wanaopata tatizo la nguvu za kiume mara nyingi, lakini hutokea hata kwa wanawake pia kukosa nguvu za kike wakati wa kufanya tendo la ndoa. Hii inaweza kuashiria matatizo mbali ya kiafya kama vile shinikizo la damu(yaweza kuwa la juu hata la chini), kisukari na magonjwa na mengine. Hivyo ni vyema kumjulisha daktari bila kujali aibu yeyote na hasa ikitokea unalipata tatizo hili wakati ukiwa bado umri wako haujafikia uzeeni. Kwa kufanya hivyo utamsaidia daktari kukupa tiba ya uhakika inayoendana na dalili zako au kukupa msaada wa kisaikolojia.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz