Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Agha Khan, MSD sasa kununua dawa kwa pamoja

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa pamoja kati ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Taasisi ya Huduma za Afya Aga Khan Tanzania (AKHST) utasaidia kuongeza ufanisi wa huduma za afya nchini.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Desemba 20, 2018 na Mkurugenzi Mtendaji wa MSD, Lauren Bwanakunu wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya ubia kati ya taasisi hizo.

Ushirikiano huo umetajwa kuimarisha mifumo ya ugavi ili kupata bidhaa zenye ubora, kuaminika na kwa gharama nafuu.

Mkurugenzi huyo amesema ushirikiano huo utasaidia kuongeza kasi ya usambazaji dawa kwa kutumia mitandao ya ununuzi wa dawa inayotumika na taasisi ya Aga Khan ambayo ina mtandao mkubwa wa ununuzi wa dawa duniani.

"Tutatumia mitandao yao kwa kujua wapi na viwanda gani wananunua na wao pia watatumia mitandao yetu," amesema.

Amesema kwa kuagiza dawa kwa pamoja itasaidia kupunguza bei na kuwapunguzia mzigo wa gharama Watanzania.

Amesema MSD inaagiza dawa kutoka kwenye viwanda zaidi ya 130 duniani na kwamba ushirikiano huo utaongeza ufanisi katika kupata aina mbalimbali za dawa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Aga Khan Kanda ya Afrika Mashariki, Sulaiman Shahaduddin amesema hatua hiyo italeta mapinduzi katika usambazaji wa bidhaa muhimu za hospitali zikiwemo za vijijini.

"Mkataba huu utawezesha kuendeleza na kugundua masoko na kuboresha shina la ugavi wa rasilimali pamoja na kuwatambua wauzaji wakuu," amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz