Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aga Khan yatamani kumaliza tatizo la vifo vya wajawazito

49386 Kghan+pic

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kibaha. Shule ya Ukunga na Uuguzi ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU)  imesema inatamani kuona siku moja tatizo la vifo vya wanawake wanaojifungua kwenye hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini kwa sababu zinazoepukika  linakoma kabisa.

Hayo yamesemwa leo na daktari kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan Tanzania, Dk Eunice Pallangyo wakati akizungumza na watoa huduma za afya zaidi ya 50 kutoka hospitali, vituo vya afya na zahanati za Serikali, wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Lengo la kukutana ilikuwa ni kujadili masuala mbalimbali ya afya ikiwamo maadili ya kazi ili kuondoa ama kupunguza kabisa vifo vya wajawazito vinavyotokana na sababu zinazozuilika.

Dk Pallangyo amesema wanawake 556 kati ya 100,000 ya wanaojifungua wanakufa, idadi ambayo ni kubwa ikilinganishwa na maboresho mbalimbali ya utoaji huduma za afya yanayofanyika.

Amesema shule hiyo ya uuguzi na ukunga kwa kuona hilo, imeamua kuanzisha mpango maalumu wa kufanya majadiliano na wahudumu wa afya yanayojikita kwenye kutafakari namna wataalamu hao wanavyotoa huduma zao za kila siku ikiwamo jinsi wanavyoongea na wajawazito wanaofika kupata huduma pamoja na ndugu zao.

"Jinsi tunavyoongea au kuwasiliana na wajawazito na ndugu zao inasaidia kugundua matatizo yao ambayo mwisho wa siku  yanachangia vifo.”

“Hivyo tunapenda kuhimiza wahudumu wenzetu kuacha kutoa huduma kwa mazoea na pia wajue lugha mbaya inasababisha wengine kujifungulia nyumbani ama kutohudhuria kliniki mpaka siku ya uchungu maana si salama," amesema.

Akizungumzia mambo yaliyoibuliwa na baadhi ya watoa huduma za afya zaidi ya 100 waliokwisha kukutana nao, daktari huyo amesema wamegundua hata aina ya maswali yanayoulizwa wajawazito wanaofika vituoni si rafiki, kufokewa wanapochelewa bila kujua sababu ama umbali aliotoka mama husika na kujisahau kujitambulisha.

Awali, ofisa muuguzi kutoka Baraza la Uuguzi na Mkunga Tanzanim, Gustav Moyo  ambaye ni mgeni rasmi amesisitiza umuhimu wa kuboresha mawasiliano kati ya watoa huduma na wateja, kuzingatiwa maadili na hasa mtoaji wa huduma za ukunga zenye kuzingatia utu, upendo na staha.

Moyo amewataka watoa huduma kutambua ili huduma bora na salama ipatikane ni lazima kuwapo na mtaalamu aliyepitia na kuhitimu mafunzo yanayozingatia viwango wakati wa utoaji huduma na pia mwenye uadilifu.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz