Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan imesema kitengo chake cha wagonjwa wa kiharusi kimeanza kutoa huduma za dharura.
Utoaji wa huduma hiyo umelenga kuisaidia Wizara ya Afya kuokoa maisha ya wagonjwa kabla ya kuwapeleka katika vituo vya kutoa tiba vya umma.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Oktoba 26, 2019 meneja masoko na mawasiliano wa hospitali hiyo, Olayce Lotha amesema kitengo hicho kilichoanzishwa mwaka 2017 kimekuwa kikitoa huduma bure kwa wagonjwa wa dharura kabla ya kuwapeleka katika hospitali za umma.
“Kuna wagonjwa wasio na uwezo, hawa hawawezi kunyimwa huduma wanapaswa kupewa matibabu haraka. Inatakiwa wapatiwe tiba haraka iwezekanavyo kabla ya masaa matatu mpaka matano baada ya kuugua tumetoa namba ambayo ni 0782004001.”
“Tunawajibu wa kumtibu mgonjwa kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Afya. Tumeandaa upimaji wa hiari bure katika kuelekea siku ya kiharusi duniani ambayo itakuwa Oktoba 29, 2019,” amesema Lotha.
Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, Mugisha Clement amesema kitengo hicho kimesheheni wataalamu wote wa magonjwa ya ubongo, mishipa ya fahamu na moyo ambao hutoa huduma kwa magonjwa ya dharura wa kiharusi.
Pia Soma
- Siri iliyojificha ndani ya mbegu za ubuyu hii hapa
- Makosa 13 yanayoweza kukufunga kwenye uchaguzi serikali za mitaa
- Mwananchi yaiibua halmashauri Buchosa, yaahidi kujenga choo cha shule