Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afya ya mifugo inatokana na matunzo na tiba

Mon, 18 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Afya ya mifugo ni tatizo kubwa linalowakabili wafugaji wengi nchini.

Licha ya kuwapo kwa wataalamu mbalimbali katika maeneo na mikoa yote ya nchi wanaotoa huduma ya mifugo, lakini, bado kuna changamoto nyingi zinazowakumba wafugaji.

Katika sehemu ambazo mawasiliano na miundombinu ni duni, wafugaji wamekuwa wakipoteza mifugo kwa sababu pindi ugonjwa unapotokea inakuwa si rahisi kufikiwa na mtaalamu kwa wakati hivyo kusababisha mifugo kufa.

Mnyama mwenye matatizo ya kiafya

Mnyama mwenye shida ya kiafya hukosa hamu ya kula na kunywa maji, mwili kunyong’onyea na kuonekana mchovu na hutembea pole pole na kwa tabu na mara nyingi hujitenga na wenzake.

Pia, pua zake na midomo huonekana kukauka na kupunguka kwa kiwango cha uzalishaji kama vile maziwa. Kwa madume huzubaa na kuinamisha shingo chini na kukosa hamu ya kuwapanda majike wanaokuwa kwenye joto.

Mnyama mwenye afya nzuri

Mara nyingi mnyama mwenye afya nzuri huwa mchangamfu wakati wote, macho mang’avu huku mkia na masikio vikimsaidia kufukuza inzi na pia hula na kucheua, kunywa maji vizuri kila siku.

Mnyama huonyesha ushirikiano na kutembea pamoja kwenye kundi huku akitembea vizuri, anashtuka na kukimbia anaposhtuliwa na mnyama hatari anapomkaribia.

Mwili wa mnyama mweye afya nzuri una uwezo mkubwa wa kukibadili chakula anachokula, kutoa mazao ya kutosha kama vile maziwa na anaonekana mwenye nguvu na kwa wale wanaoendelea kukua wanaongezeka uzito kwa muda mfupi.

Kwa mnyama anayekamuliwa mara kwa mara kupiga kelele za kumtafuta mtoto wake, kiwele huwa kimejaa maziwa, chuchu huwa wakati mwingine hutanuka upande kwa ajili ya kujaa maziwa.

Aidha, ngozi ya mnyama husisimka mara kwa mara wadudu wapomtambaa, ngozi kuwa na ulaini unaotakiwa na manyoya hung’aa na pua na midomo huwa na unyevu unyevu wakati wote. Kwa madume, huwa wana hamu ya kuwapanda majike wanaoingia kwenye joto, miili yao hujengeka vizuri.

Kwa kawaida unapomkaribia mnyama mweye afya njema na asiye na tatizo lolote la viungo endapo atakuwa amekaa chini ni lazima atanyanyuka na ikiwa amesimama ataanza kusogea sogea kuangalia unataka kufanya nini.

Nini husababisha magonjwa kwa mifugo?

Magonjwa mengi ya mifugo husambazwa na vijidudu ambao huingia kwenye mfumo wa damu na kusababisha homa na baadaye madhara makubwa.

Magonjwa mengi ya mifugo husababishwa na vyanzo kutoka nje ya mwili wa mnyama mfano mazingira machafu anayoishi mnyama, vitu vinavyosababisha vidonda na ambavyo vimelea vinaweza kukaa.

Pia, mnyama anaweza kupata ugonjwa kutokana na hali za ndani ya mwili kama upungufu wa lishe, mfano; madini, na magonjwa ya kurithi. Upungufu wa viinilishe katika chakula cha mifugo husababisha madhara katika mwili. Madhara hayo ni kama vile majike kutopata joto mapema, ndama kuzaliwa na viungo visivyo komaa, upungufu wa uzalishaji maziwa na kiwango cha uzalishaji kushuka

Kutozingatia usafi kwenye banda la ng’ombe, pamoja na kusafisha kiwele vizuri kabla na baada ya kukamua, mkamuaji mwenye kucha ndefu na ambaye hajasafisha mikono vizuri kabla ya kumkamua ng’ombe pia ni chanzo kikubwa cha kueneza magonjwa

Cha kufanya

Pamoja na changamoto hizi, magonjwa mengi yanaweza kutibiwa kwa kutumia njia za kienyeji na dawa za kienyeji ambapo pia ni vyema wataalamu wakawafundisha wafugaji ili kujua njia hizi na kuzitumia kwa ufasaha, hivyo kusaidia kupunguza gharama za matibabu.

Wafugaji wengi wana ujuzi wa miti shamba, ambao umewafaa wengi wao kwa miaka kadhaa ambao lakini umeanza kupotea kwa kiasi kikubwa na kusababisha njia za kisasa kutumika zaidi. Ni muhimu wafugaji kuanza kurejea katika tiba za kienyeji kwani zina msaada sana hasa katika maeneo ambayo huduma za kisasa haziwezi kupatikana kwa urahisi lakini pia njia za kienyeji ni bora zaidi kiafya na kiuchumi.



Chanzo: mwananchi.co.tz