JAMII imetakiwa kufahamu namna bora ya kuzuia, kuhudumia na kutibu wenye matatizo ya afya ya akili kuepusha mateso, vifo na mfarakano katika jamii hasa wanandoa .
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, madaktari, wanasaikolojia , viongozi wa dini na taasisi zinazoshughulikia afya, wamesema kudorora kwa uchumi, matatizo kazini huchangia msongo wa mawazo ambacho pia ni kisababishi cha matatizo ya afya ya akili.
Msongo wa mawazo umefafanuliwa kwamba unaweza kusababisha mhusika kuleta madhara kwa mtu aliye karibu naye akiwamo mwenzi wake.
Mratibu wa Afya ya Akili mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili, Francis Lukuwi alisema, visababishi vikubwa vya matatizo ya afya ya akili ni ugumu wa maisha unaosababisha mtu kukata tamaa kisha msongo wa mawazo. Chanzo kingine cha matatizo ni matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema matatizo ya akili husababisha baadhi kujiua au kumdhuru mtu aliye jirani yake. Lukuwi alishauri jamii ikimwona mtu ambaye awali alikuwa vizuri kihisia na ghafla akakosa furaha na kuanza kujitenga, awahishwe hospitali kwa matibabu.
Kwa mujibu wa Lukuwi, wagonjwa kati ya 10,000 hadi 15,000 hutibiwa kila mwezi katika hospitali za Temeke, Mwananyamala na Amana. Alisisitiza kuwa mtu akiwa na matatizo hayo, hushindwa kufanya kazi hivyo kukaribisha umasikini na uhusiano mbaya na wenzake.
Msaikolojia Tiba kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Isaac Lema alishauri uwekwe mfumo wa elimu utakaowezesha kuwapo wataalamu wengi wa saikolojia kuwezesha watu wengi katika jamii kupata huduma.
Akizungumzia mauaji miongoni mwa wanandoa na uwezekano wa baadhi kuchangiwa na matatizo ya akili, Lema alisema, “Laiti wangekuwa wanafika hospitalini hayo yasingetokea.”
Akizungumza na gazeti hili kuhusu mfarakano wa wanandoa, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Mashehe ya Maadili, Amani na Haki za Binadam, Askofu William Mwamalanga alisema changamoto kubwa aliyobaini ni suala la uchumi .
“Tatizo la uchumi limeongozeka kwa wana ndoa,” alisema na kueleza kuwa, amebaini hilo kutokana na utaratibu alioweka wa kukutana na watu mbalimbali kusikiliza shida zao kila Jumamosi. “Takribani wanandoa 15 ambao nakutana nao kila siku, nimebaini kinachochangia mfarakano ni suala la uchumi,” alisema.
Akizungumzia uhusiano mbaya katika ndoa na athari za msongo wa mawazo, Mkuu wa Kitengo cha Ushauri, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Bernadeta Rushashu alisema “Wapo watu wengine wanapokuwa katika hali hiyo, huvumilia mwisho uvumilivu huwashinda na kujiua au kujeruhi wengine. Haya yote yanasababisha msongo.”
Aliendelea, “Ndoa ndiyo maisha yetu yapo pale yanategemeana. Na kazini ni sehemu mtu anakaa muda mrefu asipokuwa na amani inamletea shida, hivyo vitu vyote viwili suala la ndoa na kazi vinasababisha magonjwa ya akili.”
Mhadhiri kutoka Shule Kuu ya Elimu UDSM, Dk Lulu Mahai alisema kwenye kipato wanaume wengi ambao ni nguzo ya familia, baadhi wamekuwa hawajui wafanye nini ili kuendesha familia zao matokeo yake kunakuwa na ugomvi usiokwisha hali inayosababisha kupatwa msongo wa mawazo.
Alisema kukosekana kwa mawasiliano kwa wana ndoa au familia kunakosababisha kila mmoja kuwaza jambo lake, kuumia peke yake na matokeo yake ni msongo wa mawazo hatimaye kuwapo mgongano.
Kumekuwapo na hisia kuhusu wimbi la mauaji au kujeruhi miongoni mwa wanandoa kuwa baadhi ya wahusika wana matatizo ya afya ya akili ingawa gazeti hili halikupata takwimu au uthibitisho rasmi juu ya visababishi vya matukio hayo zaidi ya taarifa nyingi za polisi kutaja wivu wa mapenzi.
Takwimu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) zilizochapishwa na gazeti hili Februari mwaka 2018, zilisema mwaka 2016 kulikuwa na mauaji 151 baina ya wanandoa nchini; kwa maana ya ama mume kuua mke au mke kuua mume.
Wakati wa maadhimisho ya kimataifa ya afya ya akili Oktoba 10, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, Dk Matshido Moeti alihimiza serikali mbalimbali kuwekeza katika afya ya akili. Alisema duniani, mtu mmoja kati ya kila watu wanne anapata tatizo la afya ya akili katika hatua fulani ya maisha na baadhi huishia kuua au kujiua.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Daktari Bingwa wa Magonjwa na Afya ya Akili na Mkuu wa idara ya magonjwa ya akili Muhimbili-Mloganzila, Dk Fileuka Ngakongwa alisema wameboresha huduma katika hospitali za Upanga na Mloganzila kwa kuongeza idadi ya Madaktari bingwa wa magonjwa hayo.