Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afya ya akili tishio jipya kwenye ndoa

Afyaya Akili Afya ya akili tishio jipya kwenye ndoa

Mon, 6 Jun 2022 Chanzo: mwanachidigital

Miongoni mwa matukio ya kikatili yaliyo ‘masikoni na midomoni’ mwa watu tangu mwishoni mwa mwezi uliopita, ni lile la mauaji ya wenza waliokuwa na miezi mitano ndani ya ndoa mkoani Mwanza.

Tukio hilo lililoibua simanzi, lilitokea Mei 28, mwaka huu, saa tatu usiku eneo la Busweru baada ya Swalha Salum (28) kudaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi kichwani na mumewe, Said Oswayo kwa madai ya wivu wa mapenzi.

Baadaye Oswald naye alidaiwa kujiua kwa kujipiga risasi, huku mwili wake ukikutwa katika ufukwe mmoja wa Ziwa Victoria.

Mbali na tukio hilo, huko Serengeti mkoani Mara, kuliripotiwa taarifa ya mume kudaiwa kumuingiza mkewe panga sehemu za siri akimtuhumu kuwa na mwanamume mwingine.

Nako mkoani Shinyanga mwanamke anadaiwa kumkata uume mumewe kwa tuhuma za usaliti wakati huko Butiama mkoani Mara, mwanamke alidaiwa kumuua mumewe kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali kwa tuhuma zilezile za usaliti.

Mambo mengi yamekuwa yakihusishwa na matukio ya ukatili na mauaji dhidi ya wenza, ikiwamo wivu wa mapenzi, msongo wa mawazo, madeni, hasira, hali ngumu ya kiuchumi, usaliti na imani za kishirikina.

Katika matukio hayo, tatizo la afya ya akili limetajwa kuchochea watu kufikia kufanya vitendo vya ukatili, ikiwamo mauaji kwa wenza wao, bahati mbaya wengi hawajifahamu kama wana changamoto hiyo.

Kwa kawaida imezoeleka wenza wanapotaka kufunga, wengi hupima maambukizi ya VVU na magonjwa mengine ya kuambukiza. Upimaji wa afya ya akili haukuwahi kuwa katika fikra za walio wengi.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kufikia mwaka 2020, watu bilioni moja walikuwa wanaishi na magonjwa ya akili, huku wengi wakiwa na umri kuanzia miaka 15 hadi 39.

Kwa sababu ya kukithiri kwa migogoro inayosababisha hata ukatili kwenye ndoa, hivi sasa inashauriwa wenza kufanya uchunguzi wa afya ya akili kabla ya kuingia kwenye ndoa.

Mtaalamu wa afya ya akili kutoka Taasisi ya Afya ya Akili Tanzania, Philimina Scarion anasema kuna uhitaji wa nguvu kubwa kuwekezwa katika masuala ya saikolojia na afya ya akili kama inavyowekezwa katika afya ya mwili.

“Ni muda sasa kuwapo kwa vitengo vya saikolojia na afya ya akili katika kila hospitali na maeneo mbalimbali ya kijamii ili kufanya huduma hii ya saikolojia na afya ya akili iweze kutolewa kwa urahisi ndani ya jamii,” anasema.

Mkazi wa Tabata, Theodory Mushi anasema mwenendo wa matukio haya unazidi kuonyesha haja ya kulazimisha watu kupimwa akili kabla ya kuingia kwenye ndoa.

“Kinachoendelea sasa kinatufanya tuanze kuona umuhimu wa kupima afya ya akili kabla ya kuingia kwenye ndoa, maana ninachoona ndoa imekuwa taasisi hatari zaidi, ule upendo haupo,” anasema Mushi.

“Najiuliza hivi inakuwaje unamuua mtu ambaye unalala naye kitanda kimoja, ulimwambia unampenda na mkaamua kwa pamoja kuanzisha uhusiano uliowapeleka kwenye ndoa. Inawezekanaje unaamua kukatisha maisha yake.”

Ushauri wa Mushi unafanana na wa Ester Maziku kwa kusema kuna uhusiano mkubwa wa tatizo la afya ya akili na matukio ya mauaji yanayoendelea kutokea nchini.

“Unajua tangu nianze kusikia kuhusu afya ya akili ndiyo naona matukio ya aina hii yanazidi kuongezeka. Nikisoma zile dalili za mtu mwenye tatizo la afya ya akili naona ni wazi kuwa kuna shida kubwa na hatua zisipochukuliwa kwa haraka maisha ya wengi yataangamia,” anasema Maziku.

Saikolojia inazungumziaje?

Mshauri wa uhusiano, Deogratius Sukambi anasema kwa hali ilivyo sasa elimu ya masuala ya afya ya akili inatakiwa itilewe mkazo na watu wajue tatizo hili lipo na ukubwa wake.

Anasema katika ofisi yake anayotoa ushauri, kuna wastani wa kesi saba kati ya 10 zinazofika kwake kutaka ushauri wa kitaalamu kutatua migogoro ya uhusiano na ndoa.

Sukambi anasema migogoro hiyo huwa na uhusiano wa moja kwa moja, mmoja kati ya wenza ana dalili za tatizo la afya ya akili.

“Unapokuwa na migogoro ya uhusiano inayochochewa na mmoja wao au wote wawili kuwa na tatizo hili (afya ya akili), huwa sio rahisi kutatua matatizo yao kwa kuwa hayana uhusiano na madai yao,” anasema Sukambi.

“Hapa ndio utaelewa ni kwa nini migogoro hii imekuwa shida sana kutatuliwa na marafiki, ndugu, wazazi au viongozi wa dini kwa nyakati hizi kwa kuwa, wao huona ni migogoro tu ya kawaida na katika mchakato wa kuitatua wanajikuta wanaongeza tatizo,” anasema Sukambi.

“Kama unakutana na ukatili wa aina hii kwenye ndoa au uhusiano hakuna suluhisho zaidi ya kuondoka kwenye hiyo ndoa, haijalishi mchungaji anasema nini maana ukiendelea kuvumilia huyo mchungaji atakuja kukuzika. Watu tu waelewe kuwa kuna watu ni wagonjwa kiasi cha kupoteza sifa ya kuwa mume.

“Tatizo hata kwa wanawake lipo pia, lakini tunaona madhara ni makubwa zaidi kwa wanaume japo tunapoelekea hata idadi ya wanawake kuua wanaume nayo itaanza kuongezeka. Kitu pekee cha kufanya ni kukaa mbali na mtu huyo, kama sio talaka basi mtengano,” anasema Sukambi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga anasema suala la mauaji ya wivu wa mapenzi linapaswa kuchukuliwa kwa upana wake ili kulishughulikia lakini sio kwa namna moja tu.

Anasema hali hii inaweza kukomeshwa kwa kuanza kuchukua hatua pale inapojitokeza awali bila kusubiri litokee tukio kubwa zaidi.

“Ukiona mwenza wako ameanza kukutukana, kukupiga na aina nyingine zote za ukatili shughulika navyo mapema, anapoanza kukudhuru kisaikolojia hapo hapo ukatae useme ‘no’ na kama anaendelea uchukue hatua nyingine za kisheria,” anasema Anna.

“Sheria katika mataifa yote duniani hairuhusu mtu kuua, uamuzi wa aina hiyo unakupeleka kwenye mikono ya sheria na kukabiliana na adhabu mbalimbali, ikiwamo kifungo kirefu gerezani, wengine hata kupewa adhabu ya kunyongwa.”

Takwimu wagonjwa wa akili nchini

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika Oktoba 2021, Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza toka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu alisema idadi ya wagonjwa wa akili imekuwa ikiongezeka, mwaka hadi mwaka.

“Mwaka 2018 tulikuwa na wagonjwa 357,799 waliokwenda kupatiwa matibabu, mwaka 2019 walikuwa 380,000, mwaka 2020 walifika zaidi ya 500,000,” alisema Dk Ubuguyu.

Hata hivyo, takwimu za wagonjwa kwa mwaka 2020 zimejumuisha na takwimu za hospitali za kanda na Taifa.

Alisema takwimu walizonazo ni wagonjwa wanaofika hospitalini kupatiwa matibabu na kuna uwezekano walioko mitaani ni wengi zaidi.

Hali hiyo inatokana na uelewa mdogo wa jamii kuhusu magonjwa ya akili kwa kuona waliochanganyikiwa ndio wanaohitaji msaada, huku ikiacha watu wengi zaidi bila ya huduma kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Dk Ubuguyu, huduma zilizopo hazikidhi haja, licha ya kuwepo katika hospitali za rufaa na maalumu kama Hospitali ya Rufaa ya Mirembe (Dodoma), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Dar es Salaam), Hospitali za Rufaa za Kanda Mbeya na Bugando na Hospitali Maalumu ya Lutindi Tanga.

Pia, alisema kuna hospitali za mikoa takribani 20 zenye wodi za kulaza wagonjwa wa akili kama Mawenzi (Kilimanjaro), Bombo (Tanga), Morogoro, Maweni (Kigoma), Iringa na nyinginezo.

Mbali na hospitali hizo, huduma ya afya ya akili inatolewa katika hospitali za wilaya na vituo vya afya.

Madaktari wanatosha?

Kwa mujibu wa Dk Ubuguyu, hadi sasa Tanzania ina madaktari bingwa 43 wa afya ya akili wanaotakiwa kuwahudumia Watanzania wote karibu milioni 60.

“Kwa uwiano wa kimataifa, angalau daktari mmoja anatakiwa kuhudumia watu 100,000. Ndio uwiano unaotumiwa hata Ulaya, daktari mmoja mpaka madaktari tisa wanahudumia wagonjwa 100,000. Lakini kwa Tanzania uwiano ni 0.6 kwa kila wagonjwa 100,000. Maana yake, madaktari zaidi ya 40 wanaohudumia Watanzania wapatao milioni 60, kila mmoja anahudumia wagonjwa 1.5 milioni.”

Anachosema Waziri wa Afya

Jana, akizindua Baraza la Taasisi ya Taifa ya Utafiti (Nimr), Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kuna mpango wa kufanya kongamano la kitaifa kuhusu matatizo ya afya ya akili kutokana na kasi yake kuzidi kutishia.

“Hali inazidi kuwa mbaya, nataka tuwe na kongamano la kwanza la kitaifa la afya ya akili, tuangalie ukubwa wake na tunakwenda mbele kwa namna gani,” alisema Waziri Ummy.

“Changamoto kubwa nyingine ninayoifahamu hatuna wataalamu wa kutosha wa masuala haya ili kuweza kuwafikia wananchi kule chini, naona bado hospitali zetu hazina uwezo wa kutosha kutoa matibabu haya halafu bahati mbaya kuna unyanyapaa.”

Hata hivyo, aliitaka taasisi hiyo kufanya tafiti za kina kuhusu tatizo hilo ili kupata majibu yatakayoleta njia ya kukabiliana nalo.

Chanzo: mwanachidigital