Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Afya ya akili ikidorora huzaa ukatili, kujiua

67af2c873fa4b96ee9237abee7467288 Afya ya akili ikidorora huzaa ukatili, kujiua

Sun, 18 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WIKI iliyopita, dunia iliadhimisha siku ya kimataifa ya afya ya akili. Huadhimishwa kila Oktoba 10. Kulingana na ujumbe wa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, Dk Matshido Moeti, kauli mbiu mwaka huu ni ‘Wekeza katika Afya ya Akili’.

Ujumbe unahimiza jumuiya ya kimataifa na kila nchi kuongeza rasilimali fedha kwa ajili ya afya ya akili. Dk Moeti anasema ulimwenguni, mtu mmoja kati ya kila watu wanne anapata tatizo la afya ya akili katika hatua fulani ya maisha yake.

Anasema katika Kanda ya Afrika ya WHO, uwekezaji wa serikali katika afya ya akili kwa kila mwananchi ni chini ya senti kumi za dola ya Marekani.

Huduma za afya ya akili zinalipiwa moja kwa moja na wagonjwa na familia zao. Kwa kaya zenye kipato cha chini na makundi mengine duni katika jamii, gharama za huduma hizi zinaweza kuwa chanzo cha mkwamo wa kiuchumi.

Mkurugenzi huyo wa WHO wa Kanda ya Afya anasema, janga la covid-19 limeonesha namna ambavyo afya ya akili ni kiungo muhimu kwa ustawi wa kila mmoja.

Makatazo ya safari, mikusanyiko, kupoteza ajira, vifo vya wapendwa na kuendelea kuenea kwa maambukizi ya virusi vya covid, ni mambo ambayo Dk Moeti anasema yamesababisha woga, wasiwasi na sonona.

Kwa mujibu mkurugenzi huyo, kuna taarifa za ongezeko la ukatili baina ya wanafamilia na visa vya kujiua. Taarifa hiyo ya Moeti inaendelea kueleza kwamba, uhitaji wa afya ya akili Afrika ni mkubwa.

Nchi 15 barani Afrika ni miongoni mwa nchi 30 duniani ambazo zina tukio la kujiua kwa kila watu 100,000. Ingawa nchi nyingi za Afrika zimeandaa sera za kitaifa za afya ya akili huduma bado zinapatikana kwenye hospitali kubwa zilizo mijini.

Inaelezwa kwamba kuna wafanyakazi tisa wa afya ya akili kwa kila watu 100,000. Lakini barani mgawanyo huu unashuka hadi mfanyakazi 0.9 huku wengi wao wakitajwa kuwa si watalamu hali inayomaanisha kwamba, upo uhaba mkubwa wa madaktari wa akili na wanasaikolojia katika Afrika.

Hata hivyo anasema zipo hatua zinapigwa katika baadhi ya nchi ambako serikali zimekubali kugatua huduma za afya ya akili, kuondokana na utegemezi kwa taasisi kubwa chache na badala yake, kuimarisha huduma katika vituo vya afya ya msingi ngazi ya jamii.

WHO inafanya kazi na serikali kuboresha sheria zinazohusu afya ya akili na sera zinazoambatana nazo, na kujenga uwezo wa wahudumu ya afya ya msingi kuhudumia matatizo ya kawaida ya afya ya akili.

Zimbabwe ilichaguliwa kushiriki kwenye mkakati maalumu wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO kuboresha afya ya akili. Tathimini ya kitaifa ya huduma za afya ya msingi nchini Zimbabwe ilifanyika mwaka jana na mashauriano ya kuandaa mpango kazi yanaendelea, hadi sasa yakihusisha wadau zaidi ya 100.

Katika muktadha wa covid-19, Dk Moeti anasema wanafanya kazi na serikali na wadau huduma ya afya ya akili iwe mojawapo katika huduma za msingi zinazotolewa wakati wote.

Hivyo yanatolewa mafunzo ya saikolojia kwa watoa huduma wanaoona wagonjwa wa covid-19. Utafiti ulioongozwa na WHO na Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) Mashariki na Kusini mwa Afrika umeonesha kuwa watoa huduma wa afya wanapata sonona, wasiwasi na msongo, hasa wanapofanya kazi katika mazingira hatarishi ama bila kuwa na vifaa vya kukinga maambukizi.

Kutokana na hilo, WHO imeandaa mwongozo kuwawezesha watoa huduma za afya kubaini dalili za msongo kwao na kwa wenzao.

Mwongozo huu unawapa watoa huduma mbinu za kujisaidia wenyewe, mbinu za kuwasikiliza wengine na kupunguza madhara ya kiafya wapatapo msongo.

Pia mwongozo huu unatoa hatua za kupata rufaa. Utafiti mwingine wa dunia nzima ulioongozwa na WHO kuhusu afya ya akili na covid-19 Juni hadi Agosti mwaka huu unaonesha nchi 27 kati ya 28 zilileta majibu yakionesha kuwa huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia zilijumuishwa kwenye mipango ya kitaifa dhidi ya ugonjwa huo.

Lakini ni nchi 17 tu zilikuwa na fedha kutekeleza mipango hiyo. Hii inaonesha umuhimu wa kauli mbiu ya mwaka huu ya kuongeza uwekezaji kwenye afya ya akili.

WHO inatoa mwito kwa serikali, wadau na jamii kuhamasisha afua, kama vile uimarishaji wa usaidizi wa watu wa rika moja, kuwajumuisha katika jamii wagonjwa wa muda mrefu, kuwapa watoa huduma ufahamu na raslimali zitakazowawezesha kuwahudumia watu weye matatizo ya afya ya akili.

Dk Moeti anatoa mwito kwa waajiri kuwekeza kwenye mipango ya ustawi wa wafanyakazi wao na mafunzo ya awali ya saikolojia.

Anataja hatua nyingine ambazo kila mtu anaweza kuchukua kuboresha afya ya akili yake ambazo ni pamoja na kupata usingizi wa kutosha, kula chakula bora, kutotumia vileo, kufanya mazoezi.

Nyingine ni kujumuika na wengine na kuwa na mpango binafsi wa kukabili msongo na wasiwasi. “Naomba kila mmoja kuwekeza katika ustawi na afya ya akili yake na kuwa tayari kuwasaidia walio karibu yake,” anahitimisha Dk Moeti

Chanzo: habarileo.co.tz