Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Abiria wa mabasi wasiovaa barakoa watangaziwa kiama

BARAKO Abiria wa mabasi wasiovaa barakoa watangaziwa kiama

Mon, 18 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KAMATI ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mbeya ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, William Ntinika, imeanza kufanya oparesheni maalumu ya kukagua na kuwachukulia hatua abiria wote wa magari ya abiria ambao hawavai barakoa.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba lengo la hatua hiyo ni kukabiliana na maambukizo ya virusi vya corona.

Oparesheni hiyo ilianza mwishoni mwa wiki ambapo wajumbe wa Kamati hiyo walikuwa wanazunguka katika vituo mbalimbali vya magari ya abiria (daladala) na kwenye baadhi ya barabara na kukagua ili kuona kama abiria wanavaa barakoa.

Ntinika alisema kutokana na tishio la ugonjwa huo umewekwa utaratibu wa kulazimisha kila abiria wa daladala na bajaji mkoani humo kuvaa barakoa na kwamba kwa wale ambao wanakaidi watakuwa wanashushwa kwenye magari na kuchukuliwa hatua.

Alisema elimu imetolewa vya kutosha na wataalamu lakini baadhi ya watu wamekuwa wakikaidi maelekezo yanayotolewa hali ambayo inaweza kusababisha ongezeko la maambukizo ya corona.

“Tumeamua tuanze kukagua kwenye magari ili kuhakikisha wananchi wetu wanavaa barakoa, ukivaa barakoa unajikinga mwenyewe na ugonjwa huo, lakini pia kama una maambukizo unawakinga wenzio,” alisema Ntinika. Alisema Serikali imewarahisishia wananchi kwa kuruhusu hata barakoa za vitambaa zitumike ambazo gharama yake ni nafuu na hivyo hakuna sababu ya watu kutozinunua na kuvaa.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei, alisema zoezi hilo litakuwa endelevu mpaka pale ambapo wananchi wote wataanza kufuata maelekezo hayo.

Alisema wakati wa oparesheni hiyo walibaini kuwa mwitikio umekuwa mzuri kwa baadhi ya wananchi isipokuwa wachache ambao alisema wataendelea kuwashughulikia wakiwabaini.

“Wengi wanajitahidi kufuata maelekezo maana wamejitahidi kuvaa barakoa, lakini tutaendelea kufuatilia na kuwachukulia hatua wote wanaokiuka utaratibu huu,” alisema Kamanda Matei.

Alisisitiza kuwa mbali na oparesheni hiyo pia askari wa Kikosi cha Usalama barabarani, wanaendelea kufanya ukaguzi kwenye magari na kuchukua hatua ikiwamo kuwashusha abira ambao hawavai barakoa hizo.

Baadhi ya madereva na makondakta wa daladala waliishukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kuanzisha oparesheni hiyo wakidai kuwa baadhi ya abiria wamekuwa wakikaidi wanapowapatia maelekezo ya kuvaa barakoa hizo.

Mmoja wa madereva hao, Said Mussa, alisema Serikali imejitahidi kutoa elimu kwa wananchi kupitia njia mbalimbali lakini baadhi ya wananchi ni wagumu kuelewa na hivyo wanaendelea kupanda magari bila kuvaa barakoa.

Alisema kwenye maeneo mengine kama madukani na kwenye taasisi za umma watu wanafuata maelekezo ikiwamo kunawa mikono na kuvaa barakoa lakini kwenye magari wanakaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live