Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

99 wahitimu Chuo cha Sayansi ya Tiba Lugalo

62036df7eff762f8029af108e0c48cea.jpeg 99 wahitimu Chuo cha Sayansi ya Tiba Lugalo

Sat, 6 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WANAFUNZI 99 wamehitimu mafunzo yao ya Stashahada ya Ofisa Tabibu na Stashahada ya Uuguzi na Ukunga katika Chuo cha Kijeshi cha Sayansi za Tiba Lugalo jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Hospitali ya Lugalo, Brigedia Jenerali Freddy Kivamba alisema hayo katika mahafali hayo ambayo ni ya 15 kwa kozi ya Stashahada ya Ofisa Tabibu na ya 18 kwa kozi ya Stashahada ya Uuguzi na Ukunga.

Alisema wahitimu hao wanapomaliza kozi hizo wanakwenda kusaidia jamii katika hospitali mbalimbali nchini.

Alisema ingawa ni chuo cha kijeshi, kipo huru kwa ajili ya kusaidia umma wa Watanzania kwani wanatibu bila kuwa na mipaka na kwamba asilimia 80 ya wanaotibiwa katika hospitali hiyo ni raia wa kawaida.

Akizungumzia tabia za ukosefu wa maadili ya kazi kwa wahudumu wa afya alisema ni tabia ya mtu kwa kuwa miiko ya kidaktari inafundisha jinsi ya kufanya kazi kwa uadilifu. Alisema inapotokea hali ya ukosefu wa maadili, bodi ya matibabu inachukua hatua kwa mhusika.

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho cha Kijeshi cha Sayansi na Tiba, Kanali Sisco Kalongola, alisema idadi ya wanafunzi wote tangu kilipoanza ni 560 hivyo kina mchango kwa taifa katika taaluma ya afya kwa kuongeza idadi ya wataalamu hao wa afya.

Aliwataka wahitimu kufanya kazi kwa bidii ikiwa ni pamoja na kujiendeleza zaidi kielimu. Aliwaasa waliobakia chuoni kujifunza kutoka kwa wenzao kwa kusoma kwa bidii ili kufika mbali zaidi.

Alisema kwa mwaka mpya wa masomo 2021/22 chuo hicho kimeongeza kozi moja ya Stashahada ya Ofisa Tabibu meno na kinywa ambayo imeanza ikiwa na wanafunzi 18.

Wakati huo huo, alisema chuo katika mwaka wa masomo 2020/21 kimetunukiwa tuzo ya utendaji bora, mazingira, mafunzo na ufundishaji hivyo kuwa kati ya vyuo viwili bora vya afya nchini vilivyo chini ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Chanzo: www.habarileo.co.tz