Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

98,000 kufanyiwa tiba ya kinywa na meno

A056a946057b69e8c026549fbaa05582 98,000 kufanyiwa tiba ya kinywa na meno

Mon, 15 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

JUMLA ya watu 98,000 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ya kinywa na meno bure katika mikoa zaidi ya 20 nchini, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Afya ya Kinywa na Meno ambayo kilele chake ni Machi 20 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa yake kwa vyombo vya habari nchini, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima matibabu hayo ni sehemu ya utafiti na tiba unaofanywa na serikali.

Waziri Gwajima alisema katika nchi zilizoendelea zimefanya mapinduzi makubwa ya kuzuia magonjwa ya kuoza meno kwa kuweka madini ya fluoride kwenye maji ya kunywa, chumvi, maziwa pamoja na dawa za meno.

Alisema kwa hapa nchini nguvu kubwa zimeelekezwa katika kuhimiza matumizi ya dawa za meno zenye madini ya fluoride.

“Nitoe rai kwa wananchi wahakikishe wanapiga mswaki kwa usahihi angalao mara mbili kwa siku kwa kutumia dawa ya meno yenye madini ya fluoride na tusisahau matumizi ya vyakula bora kwa ustawi wa afya zetu za kinywa na meno," alisema.

Alisema hapa nchini, takwimu zinaonesha idadi ya wagonjwa wa kinywa na meno waliohudhuria katika vituo vya kutolea huduma za afya mwaka 2019 ni 676,139.

“Idadi hii huenda isiakisi ukubwa halisi wa tatizo lililopo kwani bado uelewa wa wananchi kuhusiana na afya ya kinywa na meno bado upo chini na ni wachache wanaohudhuria katika vituo vya kutolea huduma za afya,” alisema.

Alisema kwa muktadha huo, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imefanya utafiti wa kitaifa wa afya ya kinywa na meno nchini ili kuweza kujua hali halisi ya afya ya kinywa na meno katika jamii.

Dk Gwajima alisema matokeo ya utafiti huo upande wa matibabu yanaonesha huduma ya kung'oa meno inaongoza huku huduma ya kuziba meno ikiwa chini sana.

“Hii imetokana na wananchi wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu afya ya kinywa na meno hivyo kuchelewa kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu. Nawaasa wananchi wanapokuwa na matatizo ya meno na fizi kuwahi hospitali ili muweza kupata matibabu stahiki,” alisema.

Waziri Gwajima alisema pamoja na hayo serikali imeendelea kutenga bajeti katika eneo hilo la kinywa na meno ambapo kuanzia mwaka wa fedha wa 2018/2019 hadi 2020/2021 kiasi cha Sh bilioni 1.4 kilitengwa kila mwaka kwa ajili ya kuimarisha huduma za kinywa na meno ikiwemo vifaa tiba madawa yakuzibia meno na kuongeza huduma hasa za maabara ya meno bandia kuanzia hospitali za rufaa za mikoa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz