Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

80% visababishi upofu vinazuilika

D890ab4d2a2b3d824df78641e15953a4.jpeg Uoni hafifu unazuilika

Fri, 6 Aug 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Asilimia 80 ya visababishi vya uoni hafifu na kutoona vinaweza kuzuilika; Imesema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Saitoke Laizer, alibainisha hayo katika ufunguzi wa kikao cha wadau kujadili uboreshaji wa huduma za macho.

Alisema kutokuwepo kwa huduma za afya ya macho zinazoridhisha ni miongoni mwa visababishi hivyo na kwamba, kuna upungufu wa wataalamu wa macho kwa asilimia 62.

Kwa mujibu wa Dk Laizer, takwimu zilizopo nchini zinabainisha kuwa, takribani watu milioni moja hadi 2.8 wana uoni hafifu na wengine hawaoni kabisa na kuwa, asilimia 80 ya visababisha matatizo vya magonjwa ya macho ni vile vinavyoweza kuzuilika.

Alisema miongoni mwa visababishi vikubwa ni pamoja na huduma za afya nchini kuwa zisizotosheleza mahitaji hali inayosababishwa kwa kiasi kikubwa na upungufu wa wanataalamu wa macho.

Alisema nchini Tanzania kuna asilimia 38 ya wataalamu wa macho hivyo kuna upungufu kwa asilimia 62.

“Hali ilivyo sasa hazikubaliki na hazibariki na ndio maana tumekaa hapa ili tujiulize na kutafakari ili tuje na mikakati kuhakikisha tunabadilisha hali hii,” alisema.

Alisema pamoja na upungufu huo vyuo vinavyozalisha wataalamu hao vimeendelea kupungua ingawa mahitaji yanaongezeka.

Mtaalamu huyo alisema kwa sasa hakuna vyuo vinavyotoa mafunzo ya utaalamu kwa ngazi ya stashahada wala astashahada (cheti), hivyo uzalishaji wa wataalamu wa macho kuwa mdogo.

“Kitendo cha vyuo kuwafundisha wataalamu wa ngazi za juu, kimesababisha kutokuwepo kwa wataalamu hao katika ngazi ya chini na hivyo, kusababisha upungufu unaowafanya wagonjwa kutembea umbali mrefu kutafuta huduma,” alisema.

Mkurugezi wa Shirika la Sightsaveres, Dk Godwin Kabalika, alisema matumaini yake ni kuona kile kitakachojadiliwa na kukubaliwa na wadau, kinatekelezwa ili kuongeza njia za kuzuia viashiria vya uoni hafifu na kuona.

Naye Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa an Serikali za Mitaaa (TAMISEMI), Dk Ntuli Kapologwe, alisema yeye na wadau wenzake watatafsiri na kuandaa mpango mkakati kwa ajili ya utekelezaji wa uboreshaji katika huduma za macho nchini.

Chanzo: www.habarileo.co.tz