Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

62% warudi dozi ya pili chanjo ya corona

Cff416d6c80ca0570c3ecfe944439396.jpeg 62% warudi dozi ya pili chanjo ya corona

Wed, 15 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Asilimia 62 ya Watanzania waliochanja chanjo dhidi ya corona ambao wanatakiwa kuchanja mara mbili, wamefanya hivyo nchini ili kujikingana ugonjwa wa Covid-19.

Aidha, imebainika kuwa katika Watanzania waliochanjwa, hakuna madhara makubwa yaliyojitokeza kwao, badala yake yako madhara madogo kama vile kuumwa kichwa.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam na Dk Florian Tinuga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alipotoa mada katika mkutano uliondaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la uhudumia Watoto (UNICEF), ambao ulikuwa mahususi kuzungumzia chanjo dhidi ya Covid-19.

Dk Tinuga alisema kuwa hadi takwimu zilizokusanywa hadi kufikia Desemba 12, mwaka huu, zinaonesha kuwa asilimia 62 ya watu waliojitokeza kupatiwa chanjo ambayo inachanjwa mara mbali, wamerudi kupata chanjo ya pili kama inavyotakiwa. “Hili ni jambo zuri sana kwa sababu linaonesha kuwa mwamko wa watu kuchanja sasa uko juu.

Na hili limefanikiwa kwa sababu kuna mfumo mzuri wa uhamasishaji. Kwanza, tunawapa ushauri wanapofika kuchanjwa,” alieleza Dk Tinuga. Alifafanua kuwa baada ya kuchanjwa mara ya kwanza, wahusika hupewa tarehe ya kurudi na hukumbushwa siku mbili kabla ya tarehe husika, na kama ikitokea siku hiyo imepita, hukumbushwa tena.

Lakini pia amesema wanawatumia wahudumu wa afya katika ngazi ya jamii wanaosaidia jamii kuchukua hatua ya kwenda kuchanja mara ya pili kwa wale waliopigwa chanjo inawayowataka kuchanjwa mara mbili. Dk Tinuga alisema hadi Desemba 12, mwaka huu, waliochanja ni watu 1,217,628 sawa na asilimia 2.11 ya Watanzania takriban milioni 57.6, huku idadi hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 60 ya chanjo zilizopokelewa.

Alisema kwa Tanzania kuna aina tano za chanjo zilizoidhinishwa nchini ambazo ni Janssen, Sinopharm, Pfizer, Moderna na Sinovac, lakini hadi sasa tatu ndizo zinatumika ambazo ni Janssen, Sinopharm na Pfizer. Kati ya hizo, chanjo ya Janssen au maarufu kwa jina la J&J hutolewa mara moja tu, wakati nyingine mtu hupaswa kuchanjwa mara mara mbili.

“Madhara yatokanayo na kuchanja ni madogomadogo ndiyo maana watu wanarudia kuchanja ambapo marudio ya chanjo hiyo ni kati ya siku 21 hadi 28 baada ya kuchanja,” alieleza Dk Tinuga. Aliongeza, “Madhara hayo madogo ni ya kawaida kama kizunguzungu, kichwa kuuma na kesi nyingi zilizoripotiwa zilikuwa ni kati ya masaa 24 hadi 48 na tatizo linakuwa limekwisha na mrejesho tulikuwa tukipata kutoka wahusika au wataalamu wa afya kupiga simu.”

Dk Tinuga alisema tokea kuzinduliwa kwa chanjo nchini dozi za chanjo 4,421,540 zimetolewa kwa wananchi, katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zipatazo 6,784, ambavyo ni vya binafsi na vya umma, ambako vinatolewa katika maeneo yanayotolewa chanjo kwa watoto. Akizungumzia mafunzo katika utoaji wa chanjo, ni kwamba chanjo hizo zinapunguza makali ya hatari za ugonjwa huo wa Covid-19, wananchi wana uelewa na wanauliza maswali kuhusu chanjo hizo na kwamba hazina madhara makubwa kwa wale waliochanjwa.

Alisisitiza kuwa lengo la serikali ni kuona asilimia 60 ya Watanzania wanapata chanjo, kwani ndio kiwango ambacho kitaifanya jamii iwe salama na ugonjwa huo kulingana na udhibiti unaokubalika kimataifa. Akizungumzia changamoto zilizojitokeza awali hadi wananchi kusita kuchanja, Profesa Deodatus Kakoko kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), alisema awali kulikuwa na imani potofu juu ya chanjo hizo, lakini baada ya kuanzishwa mkakati shirikishi na harakishi watu wanajitokeza kuchanja kwa wingi.

“Tunaendelea kupambana na imani potofu kwa kutoa elimu nchi nzima kupitia mpango shirikishi na harakishi ambapo tumezunguka mikoa yote nchini na tunaendelea kuzunguka, tunawatumia watu wenye ushawishi kutoa elimu ya umuhimu wa kuchanja, viongozi wa dini na viongozi wa serikali kuanzia kitogoji hadi mkoa na mpango huu umeleta matokeo chanya,” alisema.

Profesa Kakoko alisema vyombo vya habari vina wajibu wa kuendelea kuhabarisha umma taarifa sahihi na umuhimu wa chanjo kwakua taarifa potofu zinasambaa kwa kasi kuliko taarifa sahihi. Mwenyekiti wa (TEF, Deodatus Balile aliwaomba waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi juu ya faida ya kuchanja na madhara ya kutochanja na waendelee kutoa elimu sahihi juu ya ugonjwa huo kwa kutoa makala na vipndi vya redio, luninga na mitandao ya kijamii ili kueleimisha Watanzania.

“Tukiamua kuibadilisha jamii na kuingia kwenye njia stahiki inawezekana, hivyo tutumie kalamu zetu kuandika habari sahihi kwani Covid-19 ipo na inaangamiza dunia, tusijilinganishe na wengine kuwa nchi fulani wamekufa wengi sisi hatujafa wengi mapambano yapo palepale,” alisema Balile.

Naye Dk Alex Mphuru kutoka UNICEF, alisema chanjo hizo zimepitia taratibu zote zinazokubalika kisayansi na pia zimeidhinishwa na mamlaka husika nchini. Rais Samia Suluhu Hassan alizindua rasmi kampeni ya taifa ya chanjo ya Covid-19, Julai 28, mwaka huu, na alikuwa wa kwanza kuchanjwa akiuhakikishia umma wa Watanzania kuwa chanjo hizo ni salama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live