Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, Profesa Mohamed Janabi amesema hadi sasa watu 60 wamepata huduma ya kuwekewa puto ili kupunguza uzito.
Profesa Janabi amesema kuwa kati ya watu hao, ni mtu mmoja tu lilimshinda, akatolewa na kwamba hilo ni jambo la kawaida. “Kuwepo kwa huduma ya kupunguza uzito na kupunguza mafuta mwilini ni sehemu ya utalii wa matibabu hivyo tunatarajia kupata watu wengi zaidi,” alisema.
Profesa Janabi anasema utoaji huduma hiyo unahusisha uingizaji wa mrija wa puto kupitia mdomoni, hali itakayopunguza kiwango cha chakula kwa mhusika. “Tutaweka kwa miezi nane, tutaingiza kupitia mdomoni hadi kwenye tumbo hakuna upasuaji, tutatumia mitambo ifike mahali pake tutajaza dawa linapunguza ukubwa wa tumbo, ukila kidogo utashiba hivyo tunategemea uzito utapungua,” alisema.
Profesa Janabi amesema gharama ya huduma hiyo nje ya nchi inategemea na nchi na kwamba, India ni Sh milioni 15 hadi 20 na Ulaya milioni 30 kwenda juu lakini hapa nchini ni Sh milioni 4 hadi milioni 4.2.