Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

561 wapimwa bure magonjwa ya moyo

561f8efc29fa431a7dcc39fc0cbcbd20 561 wapimwa bure magonjwa ya moyo

Sun, 7 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WATU 561 wamepimwa viashiria vya magonjwa ya moyo bila malipo katika upimaji maalumu, uliofanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Upimaji huo ulioenda sambamba na utoaji wa matibabu na kupewa rufaa kwa wale waliokutwa na matatizo, ulifanyika kwa siku mbili katika viwanja vya Mbagala Zakheem wilayani Temeke kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari hizi katika viwanja hivyo, Mwenyekiti wa Wanawake wa JKCI ambaye pia ni daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi, Anjela Muhozya alisema katika upimaji huo pia walitoa elimu ya lishe bora kwa afya bora ya Moyo.

Dk Anjela alisema kati ya watu 561 waliowapima, asilimia 80 walikutwa na shinikizo la juu la damu na kati ya hao asilimia 50 walikuwa wanajijua kuwa na tatizo lakini hawakuendelea na huduma za matibabu kutokana na sababu mbalimbali za maisha, asilimia 30 hawakuwa wanajijua kabisa kama wanatatizo hilo hawa walianzishiwa matibabu.

Waliokutwa na matatizo, asilimia 40 walikamilisha huduma ya matibabu katika viwanja hivyo hii ikiwa ni pamoja na kupewa dawa na ushauri ; na asilimia 20 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na Hospitali ya Temeke.

“Kati ya watu tuliowapima, asilimia 10 hawakuwa na tatizo lolote la kiafya, ila uzito wao ulikuwa mkubwa, kitu ambacho ni hatari kwa afya ya moyo. Hawa tumewapa ushauri wa kubadili mfumo wa maisha katika ulaji wao wa vyakula pamoja kufanya mazoezi mara kwa mara,” alisema Dk Anjela.

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Godwin Gondwe aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa moyo wao wa upendo wa kuwafikiria wananchi wanyonge na kwenda kuwapa huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo yoyote yale.

“Ninawashukuru sana kwa upendo wenu wa kuwafuata wananchi wanyonge na kuwapa huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo kama tunavyofahamu matitabu haya yanagharama. Kwa kuwafuata kwenu wananchi hawa wameweza kuokoa fedha ambazo wangelipia hospitali na kwenda kuzitumia katika matumizi yao ya kila siku.

“Pia Ofisa Ustawi wa jamii ameweza kuwasikiliza watu wenye shida za kijamii na kuwapa maelekezo ya jinsi gani wataweza kufika JKCI na kupata matibabu. Hii itawasaidia kutoogopa kufika pale kwa ajili ya kutibiwa kwa kuwa hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu,” alisema.

Gondwe alisema wilaya yake itaendelea kushirikiana na JKCI, kuhakikisha wananchi wanyonge wanafikiwa na wataalamu wa taasisi hiyo. Aliwaomba wananchi wa Temeke kutumia fursa hiyo ya upimaji wa afya zao bila malipo.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi alisema amefika katika viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kuwaunga mkono wanawake wa taasisi hiyo kwa kufanya upimaji kwa wananchi.

“Kama mnavyoona tunafanya upimaji kwa wanawake na wanaume na wale ambao wamekutwa na matatizo wameanzishiwa matibabu kwa kupewa dawa na wengine watakuja JKCI kwa ajili ya matibabu ya kibingwa… taasisi yetu itaendelea kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa na kupata elimu ya magonjwa hayo ambayo siyo magonjwa ya kuambukiza na kama mtu atakuwa na uelewa nayo anaweza kuyaepuka,” alisisitiza Profesa Janabi.

Mkazi wa Mbagala Kibondemaji, Musa Kitimla alisema alisikia katika redio kuna huduma za upimaji wa moyo ambao utafanyika kwa muda wa siku mbili katika viwanja vya Mbagala Zakheem, akaona ni muhimu kufika hapo kwa ajili ya kupima afya yake.

“Namshukuru Mungu nimefika hapa na kupata huduma mbalimbali za kupima afya na majibu yangu yameonekana sina tatizo lolote lile. Nitaendelea kuichunga afya yangu ili iendelee kuwa salama. Ninawasihi wananchi wenzangu wakisikia mahali kuna upimaji wa aina hii waende kwani licha ya kupima afya zao watapata ushauri pia," alisema Kitimla.

Upimaji huo ulihusisha upimaji urefu, uzito, shinikizo la damu, sukari, virusi vya Ukimwi na kupewa ushauri wa lishe bora. Kwa waliokutwa na matatizo ya moyo, wamepewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika taasisi hiyo na Hospitali ya Temeke ili wafanyiwe uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz